Siku ya pili mgomo Kariakoo, wafanyabiashara wamtaka Rais Samia

Dar es Salaam. Wafanyabiashara eneo la Kariakoo wameendelea na msimamo wa kutofungua maduka, wakimtaka Rais Samia Suluhu Hassan kwenda kusikiliza malalamiko yao.

Wameeleza wamechoshwa na matamko ya viongozi walio chini yake, wakidai hakuna utekelezaji wa yaliyofikiwa na kikosi kazi kilichoundwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwaka 2023 walipogoma.

Mgomo umeingia siku ya pili leo Juni 25, 2024, licha ya Serikali kupitia Waziri wa Uwekezaji na Mipango, Profesa Kitila Mkumbo kutangaza kusitisha ukaguzi wa risiti za mashine za kielektroniki (EFD) uliokuwa ukifanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia mkoa wa kikodi Karikaoo.

Waziri Mkumbo alisema jana Juni 24, 2024 jijini Dodoma kwamba wanaandaa utaratibu mzuri wa utekelezaji wa suala hilo.

Profesa Mkumbo alisema katika kikao cha viongozi wa wafanyabiashara na Serikali kilichofanyika siku hiyo wamekubaliana kuwapanga machinga ili kutoingilia ufanyaji biashara wa wenye maduka na kuhakikisha kila anayefanya biashara analipa kodi kama ilivyokubalika.

Mgomo huo unaendelea wakati ambao mikoa ya Mbeya, Mwanza na Iringa imeungana na wafanyabiashara wa Kariakoo kupaza sauti zao.

Katika eneo la Kariakoo tangu alfajiri hadi saa 3.30 asubuhi maduka mengi yalisalia kuwa yamefungwa, huku wauzaji hawapo tofauti na jana walipokuwa nje ya maduka yao.

Nassor Ally, mfanyabiashara wa Kariakoo amesema Rais pekee ndiye anayeweza kutatua matatizo yao.

“Mawaziri wamekuja hapa, Waziri Mkuu amekuja hapa hakuna kitu, imeundwa kamati hakuna kilichofanyika tukakiona, aje Rais atusikilize labda yeye atatuelewa kwa sababu walio chini yake wameshindwa,” amesema Ally.

Amesema tamko kuzuia kamatakamata siyo mara ya kwanza linatolewa.

“Faini Sh15 milioni, mtu ana mtaji wa shilingi ngapi, watu wanaruhusu mianya ya rushwa, hakuna mtu anaweza kulipa Sh15 milioni kama faini na badala yake unataka mazungumzo pembeni, kwa nini tulipe hela ambayo tunajua haiingii kwenye mfuko wa Serikali?” amehoji.

Mfanyabiashara Mahmoud Mussa amewalalamikia polisi akidai wamegeuka kuwa maofisa tathmini na ukaguzi, hivyo kuwa kero.

“Mtu unamkagua mzigo anakupa risiti unasema risiti haiendani na mzigo, wewe ndiyo umemuuzia, umetumia kigezo gani kusema thamani ya mzigo haiendani na mzigo, inakera, polisi wasimame kwenye kazi zao na si kuingilia biashara,” amesema Mussa.

Baadhi ya machingwa wakiendelea na biashara zao leo.

Tofauti na jana wafanyabiashara ndogondogo maarufu machinga waliotumia fursa ya kufungwa maduka kufanya biashara, leo wanaeleza kukosa bidhaa kutokana na wamiliki wa maduka kuyafunga.

“Serikali iwasikilize yaishe, aje Rais wanayemtaka hali ni mbaya, kuna wafanyabiashara wengi kutoka nje wako hapa kutoka Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo- DRC) na Zambia wamekwama hawajapata mzigo, sisi wenyewe unapata mteja hauwezi kwenda kuchukua mzigo tunakosa hela,” amesema Mussa Juma.

Amesema kufunguliwa  maduka ndiko kunachangamsha biashara kwa kuwa wanaishi kwa kutegemeana na hasa wanapopata wateja wanaoshindwa kuwahudumia.

Mgomo unaendelea licha ya jana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akiwa Kariakoo aliwataka wafanyabiashara warejee katika shughuli zao.

Muuza nguo za ndani, Lucky Isack amesema mgomo unaiathiri zaidi Serikali kwa kupoteza mapato.

“Jana tumekaa tukaondoka Serikali haijaingiza kodi yoyote,” amesema.

Baadhi ya maduka yakiwa yamefungwa Kariakoo jijini Dar es Salaam. Picha na Aurea Simtowe

Wafanyabiashara wa simu wameendelea na shughuli zao kama kawaida baada ya maduka kufunguliwa.

Muuza simu Mtaa wa Msimbazi, Asha Salum amesema wamefungua kwa sababu kodi ya pango inakaribia kuisha wanahitaji kulipa, hivyo wakifunga hawatapata pesa za kulipia.

“Malalamiko yaliyotolewa ni ya msingi na yanatugusa wote lakini kwa upande wetu ni ngumu kwa sababu tunahitaji kulipa kodi inayoisha mwezi huu, nikifunga sitaingiza pesa yoyote kwa sasa,” amesema.

Amesema maduka yao tofauti na wauza nguo wao wanachangia watu zaidi ya wanne, hivyo ni vigumu kufunga.

Related Posts