TETESI ZA USAJILI BONGO: Simba yatua kwa Pedro Miguel

KLABU ya Simba imeanza kumfuatilia kiungo wa Petro Luanda ya Angola, Pedro Pessoa Miguel ili kuiongezea nguvu timu hiyo msimu ujao.

Nyota huyo anayecheza kiungo mkabaji na ushambuliaji, inaelezwa Simba itakutana na ushindani kwani timu za Saudi Arabia na Ureno zinamuhitaji pia baada ya kudumu Petro kwa miaka mitano tangu 2019.

KLABU ya Singida Black Stars iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa kiungo, Aziz Andambwile kutoka Fountain Gate.

Nyota huyo wa zamani wa Mbeya City, inaelezwa tayari amefikia makubaliano hayo na kikosi hicho chenye makazi yake mjini Singida.

LICHA ya viongozi wa KenGold kumuhakikishia kipa wa timu hiyo, Paul Kamtewe kubakia msimu ujao, lakini mwenyewe bado hajaamua juu ya hatma yake. Kipa huyo aliyewahi kuichezea Kagera Sugar na Stand United, huku akiipandisha KenGold Ligi Kuu Bara, amepewa nafasi ya kubaki msimu ujao japo anasikilizia ofa mbalimbali zilizopo baada ya Biashara, Mbeya City na Pamba Jiji kumuhitaji.

BEKI Mkongomani wa Simba Queens, Ruth Ingosi inaelezwa yupo kwenye hatua nzuri ya kujiunga na Rivers Angels FC ya Nigeria.

Inaelezwa beki huyo hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba Queens msimu ujao na hiyo ni kutokana na ushindani aliokutana nao kwenye eneo la ulinzi ambalo Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ na Violeth Nickolaus.

ALIYEKUWA kocha wa Yanga Princess, Charles Haalubono anatarajia kujiunga na Zesco Ndola Girls ya nchini kwao Zambia. Kwa sasa kocha huyo raia wa Zambia yupo nchini humo baada ya kutemwa na Yanga Princess mara baada ya msimu kumalizika huku timu hiyo ikimaliza nafasi ya tatu Ligi Kuu ya Wanawake.

MSHAMBULIAJI aliyemaliza mkataba ndani ya Kagera Sugar, Moubarack Amza, raia wa Cameroon yupo kwenye mazungumzo na Namungo ambayo kama mambo yakienda sawa basi msimu ujao atakuwa mchezaji wa timu hiyo.

Mwanaspoti limepata taarifa kutoka kwa rafiki wa karibu na mchezaji huyo kuwa mazungumzo yomefikia pazuri na huenda akajiunga nao.

RAPHAEL Daud ambaye msimu uliopita alikuwa na kikosi cha Ihefu, inaelezwa kwamba amepata ulaji Namungo FC baada ya mazungumzo baina yake na viongozi kwenda vizuri.

Kiungo huyo ambaye amewahi kuzitumikia Mbeya City na Yanga, anachosubiri hivi sasa ni utambulisho na kuanza kazi.

Related Posts