Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
Katika mfumo wa afya wa Tanzania, watoa huduma za afya wanakutana na changamoto nyingi za kimaadili wakati wa kufanya maamuzi ya kutibu wagonjwa. Changamoto hizi, ambazo mara nyingi huleta mitanziko (dilemma), zinaweza kusababisha vifo kwa wagonjwa hasa pale wanapokataa matibabu. Ili kukabiliana na hali hii, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Idara ya Falsafa na Taaluma za Dini, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Oslo cha Norway, kimezindua Kamati ya Kwanza ya Maadili ya Kitabibu nchini Tanzania.
Kamati hii ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa miaka mitano unaojulikana kama ETHIMED, ambao ulianza mwaka 2022 na unatarajiwa kumalizika mwaka 2026. Kamati hii inalenga kuwasaidia watoa huduma za afya kukabiliana na mitanziko ya kimaadili wanayokutana nayo wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa.
Kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, uzinduzi wa kamati hii umefanyika Februari 5, 2024, katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya. Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Dk. Godlove Mbwanji, anasema kuwa kuundwa kwa kamati hiyo ni msaada mkubwa kwa watoa huduma za afya hasa wakati wa kufanya maamuzi ya kutibu wagonjwa.
“Kamati ya maadili ya kitabibu iliyoundwa hapa ni ya kwanza kuanzishwa nchini na hospitali yetu imepata bahati kwani ndiyo ya kwanza kuwa na kamati hii,” anasema Dk. Mbwanji na kuongeza kuwa:
“Watoa huduma za afya wamekuwa wakikutana na mitanziko mbalimbali wakati wa kufanya maamuzi ya matibabu. Sasa mara nyingi wataalamu wanapokutana na changamoto hizo kila mmoja anahangaika kujua afanye nini. Kuna masuala ya kimaadili ambayo yanapaswa kuzingatiwa ili kuhakikisha maamuzi yanayofanywa hayaleti madhara kwa mgonjwa au mtoa huduma,”.
Maadili na Ufanisi Katika Huduma za Afya
Lucas Kitula ni Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Falsafa na Taaluma za Dini na Mratibu wa mradi wa ETHIMED, alisema kuanzishwa kwa kamati hiyo ni mwanzo mzuri katika kuhakikisha elimu ya maadili ya kitabibu inafikia hospitali nyingine nchini.
“Mitanziko ya kimaadili ipo sana kwenye hospitali zetu. Kuanzisha kamati hii hapa Mbeya ni hatua ya kwanza, kwani kama tutapata fedha, tutazifikia hospitali nyingi zaidi. Hii kamati itasaidia wahudumu wa afya kukabiliana na mitanziko wakati wa kufanya maamuzi ya utoaji huduma kwa wagonjwa,” anasema Kitula.
Kitula anasema Mradi wa ETHIMED mbali na kuanzia Mbeya lakini unalenga kupanua wigo wake kwenye hospitali nyingine nchini.
“Mbali na kuanzishwa kwa Kamati hii, tutakuwa tunafanya semina kwa ajili ya kufuatilia maendeleo na kuhakikisha yale tuliyofundisha yanatekelezwa ipasavyo,” aliongeza Kitula.
Mchango wa Vyuo Vikuu katika Kuimarisha Maadili ya Kitabibu
Dk. Michael Lyakulwa, Mkuu wa Idara ya Falsafa na Taaluma za Dini kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema kuwa mradi huo utasaidia kutatua mitanziko mbalimbali ya kimaadili wakati wa kutoa matibabu kwa wagonjwa.
“Sisi kama idara na chuo kwa ujumla, wajibu wetu ni kuhudumia jamii. Mradi huu umetusaidia kuona ni kwa namna gani wataalamu wetu wa afya wanaweza kufanya maamuzi pindi wanapopata mitanziko wakati wa utoaji huduma,” anasema Dk. Lyakulwa.
Aidha, anabainisha kuwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya ni ya kwanza kuwa na kamati hii ya maadili ya kitabibu na kwamba wanatarajia Wizara ya Afya itawaunga mkono kuhakikisha kamati hizi zinaanzishwa katika hospitali zote nchini ili kusaidia watoa huduma za afya kukabiliana na mitanziko katika kutoa huduma kwa wagonjwa.
Mafunzo na majukumu ya Kamati
Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Falsafa na Taaluma za Dini kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Maadili ya Kitabibu-Chuo Kikuu cha Oslo, Shija Kuhumba, anasema mafunzo hayo yanalenga kuangalia namna kamati inavyopaswa kuwa na majukumu yake.
“Huu ni mwendelezo wa kile tulichofanya mwaka jana wa kutoa mafunzo ambapo sasa tumenzisha kamati ambayo kazi yake kuu itakuwa ni kutafakari mitanziko inayotokea katika utendaji kazi. Mfano; mgonjwa kukataa tiba, hali hii huwapa wakati mgumu watoa huduma za afya katika kufanya maamuzi ya kutibu wagonjwa. Hivyo, kwa kuwa na chombo hiki kutasaidia kutoa majibu ya changamoto ikiwamo ushauri,” anasema Kuhumba.
Uzoefu wa Kimataifa
Dk. Berit Hofset Larsen, mtaalamu wa maadili ya kitabibu kutoka Chuo Kikuu cha Oslo nchini Norway, anasema kuundwa kwa kamati hiyo kutasaidia kuepusha mitanziko mingi inayojitokeza wakati wa utoaji huduma za afya kwa watumishi.
“Tunafurahi kuona kwamba kamati hii imeanzishwa hapa nchini na jukumu letu ni kusaidia kutoa mafunzo na uzoefu wetu. Tunaamini kuwa huu utakuwa msaada mkubwa kwa watoa huduma za afya hapa Tanzania,” anasema Dk. Larsen.
Kwa kumalizia, uzinduzi wa Kamati ya Maadili ya Kitabibu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya ni hatua kubwa katika kuhakikisha watoa huduma za afya wanapata msaada wa kufanya maamuzi yenye kuzingatia maadili. Hii itasaidia kuboresha huduma za afya nchini na kupunguza mitanziko ya kimaadili inayowakabili watoa huduma za afya.