Dar es Salaam. Wanafunzi 100 kutoka shule za sekondari nchini, wameanza kunolewa kupitia programu ya uongozi kwa vijana (Beginit), iliyotajwa kuwa chachu ya mabadiliko katika uongozi wa kijamii hapo mbeleni.
Wadau wa maendeleo wanaoendesha mradi huo, wamebainisha kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali kutoa mafunzo ya uongozi kwa vijana lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kutambua na kutumia fursa mbalimbali.
Akizungumza leo Jumanne, Juni 25, 2024 wakati wa kufungua mradi huo hapa nchini, Mkuu wa Mradi wa Beginit, Elena Tropinova amesema programu hiyo ilianza kwa miaka mitatu ikishirikisha nchi za Tanzania, Nigeria na Afrika Kusini.
Amesema pamoja na kufundishwa mambo mbalimbali kuhusu uongozi, wanafunzi hao wanakutanishwa na wenzao kutoka nchi mbalimbali na kujifunza kupitia mitandao ya ana kwa ana ikiwamo Zoom.
“Tumelenga kuibua vipaji vya uongozi lakini kuendeleza mabadiliko chanya katika uongozi. Tunaangalia namna ya kuwafikia vijana wenye umri wa miaka 15 na 16 wanafikiria nini kuhusu malengo yao ya baadaye na namna ya kubadilisha mazingira yao kwa mtazamo chanya,” amesema Elena.
Amesema mpaka sasa Tanzania wamewafikia vijana 100 na wanatarajia kufikia mwakani wawe na vijana 200 kwenye program hiyo, “tuna jumla ya vijana 500 katika nchi zote 5 za mradi huu wa Diginity.”
Mtaalamu Mwandamizi wa Programu ya Beginity, Yersain Kabdrashev amesema programu hiyo inawaandaa vijana wa baadaye nchini kujitambua na wanaanza nao wakiwa bado wadogo wakiwa shuleni.
“Hawa tunaamini wana karama ya uongozi, tunawajenga wajitambue na watambue uongozi ni nini. Kwanza kujua namna ya kushiriki mambo mbalimbali katika jamii na namna gani wanaweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii inayowazunguka na dunia kwa ujumla,” amesema.
Yersain amesema wamekuwa wakitumia mifano kadhaa ya viongozi mashuhuri duniani walioleta mabadiliko katika programu hiyo ili kuhakikisha wanafahamu na kujifunza wangali wadogo.
“Rais Samia Suluhu Hassan ni Rais wa kwanza mwanamke Tanzania ni mabadiliko makubwa na tunamtumia kama mfano kwao na wale wa nchi zingine. Hatujamuacha nyuma mtoto wa kiume tunaenda nao wote sambamba, wajitambue na tunahitaji kujenga kizazi kipya na malengo yetu kuweka ufahamu wa uongozi wa kijamii ili kutatua matatizo yetu kwa ujumla,” amesema.
Wakielezea manufaa ya mafunzo hayo, wanafunzi hao wamesema wameweza kujitambua na kujua namna ya kuwasilisha mawazo yao kwa viongozi maeneo yanayowazunguka.
Mwanafunzi Shule ya Sekondari Temeke jijini Dar es Salaam, Meura Moses amesema amefaidika na programu hiyo kwa kuwa imempa kujiamini na kuweza kusimama mbele ya watu wengi na kujieleza.
“Pia hii project imeniwezesha kuwa na uwezo wa kuongea na watu wazima, kijiji chetu ninachoishi mwenyekiti wetu na diwani nimeweza kuwapa mawazo yangu ambayo kwa sasa wanayafanyia kazi, kiufupi imetuletea manufaa mengi makubwa,” amesema Moura.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Temeke kidato cha tatu, Leonard Charles amesema programu hiyo itamsaidia kuwa kiongozi na mwanajamii bora baadaye kwa sababu wamekuwa wakijifunza mambo mengi ya kuongoza watu na kuwa viongozi bora baadaye.
“Inatuelekeza jinsi ya kutumia mtandao wa intaneti, huko nakutana na watu tofauti itanisaidia katika mipango yangu ya kusoma mbele, pia tunaenda kukutana na watu mbalimbali hata nikimaliza kidato cha nne ninaweza kuendelea mtandaoni ili niweze kufika nchi hizo zingine,” amesema Leonard.
Mwakilishi wa Kampuni ya Indrive, Abdul Mwanja amesema faida wanazopata kwenye kampuni hiyo wanarudisha kwa jamii na imerudisha kwa kuwawezesha vijana wadogo kwenye njia tofauti.