Watoto wachanga 337 wapoteza maisha Geita ndani ya miezi mitano

Geita. Upungufu wa wataalamu wenye sifa, uhaba wa vifaa tiba, kushindwa kupumua na  ubovu wa barabara  vimetajwa sababu zilizochangia vifo vya watoto wachanga 337 kuanzia Januari hadi Mei 2024 mkoani Geita.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Herman Matemu amesema hayo jana Juni 24 2024  wakati akiwapokea madaktari bingwa 35 waliofika mkoani humo kutoa huduma za kitabibu kwenye hospitali za wilaya katika halmashauri sita za Geita kwa  siku tano.

Amesema sababu hizo pia zimechangia vifo vya uzazi kwa kinamama 24 kwa kipindi kama hicho na kuwataka watumishi wa sekta ya afya ambao hospitali zao zinafikiwa na madaktari hao bingwa kutumia fursa hiyo kujengewa uwezo, kujifunza mbinu mpya ili baadaye wawasaidie wananchi wenye matatizo kiafya.

 “Uwepo wa madaktari hawa katika hospitali zetu ni fursa nzuri kwa wataalamu kujifunza mbinu mpya za utoaji wa huduma za matibabu, natoa rai kwa madaktari wetu watakaoshirikiana moja kwa moja na hawa madaktari bingwa kutoa huduma watumie nafasi hiyo kujifunza ili watakapoondoka wabakie na ujuzi,” amesema Matemu.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Omari Sukari amesema mkoa huo wenye wakazi milioni 2.9 una vituo vya kutolea huduma 247 na kwa miaka mitatu iliyopita vituo vipya 63 vimefunguliwa na 27 kati ya hivyo vinatoa huduma ya upasuaji.

Omari amesema katika mkoa huo, kina mama 120,000 hujifungua kwa mwaka.

Akitoa takwimu za miaka mitatu nyuma, Dk Omari amesema kwa mwaka 2021 kina mama 63 walipoteza maisha, mwaka 2022 (  57), mwaka jana 55 na mwaka huu kuanzia Januari hadi Mei waliopoteza maisha ni 24.

Kwa upande wa watoto, amesema mwaka 2022 vifo vilikuwa 905, mwaka 2023 vifo 817 na mwaka huu 2024 kwa kipindi cha Januari hadi Mei watoto wachanga 337 wamepoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kushindwa kupumua, kuzaliwa na uzito pungufu isivyo kawaida.

Amesema vifo hivyo vimeendelea kupungua kutokana na Serikali kuboresha huduma za afya ikiwamo ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa magari ya wagonjwa.

Related Posts