Arusha. Mahakama ya Rufani imebariki adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela kwa Omary Said, mkazi wa Morogoro aliyehukumiwa kwa kosa la kukutwa na vipande viwili vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola 15,000 za Marekani.
Hii ni rufaa yake ya pili kukwaa kisiki, kwani alipohukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, alikata rufaa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, ambako pia aligonga mwamba.
Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali rufaa hiyo baada ya kuona haina mashiko na kusemaa kwamba adhabu iliyotolewa ilikuwa sahihi.
Rufaa hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro wa Novemba 9, 2022 katika rufaa ya jinai namba 49/ 2022.
Awali, Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, kwenye kesi ya uhujumu uchumi namba 10/2020, mrufani huyo alisomewa shtaka la kukutwa na nyara za Serikali, kinyume na kifungu cha 86 (1) (2) (b) na (3) ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, namba 5 ya mwaka 2009 kama iliyorekebishwa mwaka 2016.
Kifungu hicho kilisomwa na kifungu cha 57 (1) na 60 (2) vya Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kiuchumi na Kuratibu, Sura ya 200 (EOCCA).
Ilidaiwa alikutwa na meno hayo ya tembo yenye uzito wa kilo 10.3 yenye thamani ya Dola 15,000 za Marekani, bila kuwa na kibali au leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Mrufani alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
Ilielezwa mahakamani hapo na Ofisa wa Wanyamapori kutoka Kikosi cha Kudhibiti Ujangili (KDU), Dar es Salaam, David Marwa kuwa Desemba 2, 2017 walipata taarifa kuna mtu anauza meno ya tembo katika Kijiji cha Mvuha, Morogoro na walipewa jukumu la kwenda kumkamata.
Alieleza Mahakama kuwa waliweka mtego wa kumkamata mrufani kwa kujifanya wanunuzi na walipofika kijiji hapo walikubaliana wakutane Shule ya Sekondari Mvuha ambapo walikwenda na askari wenzake kupitia gari binafsi.
Alidai walijificha kwenye kichaka karibu na shule hiyo na alikubaliana na mrufani huyo bei kuwa nini Sh250,000 kwa kila kilo moja na kufanikiwa kumkamata, akiwa ameweka meno hayo kwenye mfuko.
Rufaa hiyo ya jinai namba 31/2023 ilisikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na Jaji Rehema Mkuye, Lucia Kairo na Lameck Mlacha, waliotoa uamuzi huo juzi Jumatatu Juni 24, 2024.
Mrufani aliwasilisha hoja 11 za rufaa, ikiwemo kudai kusomewa shtaka kwa lugha ambayo hakuielewa, hukumu kutokana na shahidi wa kwanza ambaye hakushuhudia upekuzi wala ukamataji wake, kuwepo kwa mkanganyiko wa mashahidi juu ya uwekaji wa namba kwenye vielelezo.
Alidai mashahidi wa Jamhuri hawakuwa wa kuaminika, walikuwa na ushahidi uliopishana na kuwa mashahidi wa Jamhuri hawakuthibitisha pasipo shaka kosa hilo.
Mrufani huyo alijitetea mahakamani hapo peke yake huku Jamhuri ikiwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili Upendo Shemkole.
Wakili Shemkole aliieleza Mahakama sababu tatu kati ya alizowasilisha mrufani hazina misingi wala hoja kisheria, hivyo kuomba Mahakama iziondoe.
Kuhusu hoja ya pili kwamba cheti cha ukamataji kilifikishwa na kutiwa saini katika Kituo cha Polisi Mvuha, alidai ni suala dogo ambalo haliwezi kubadili ukweli kwamba mrufani alikamatwa akiwa na meno ya tembo.
Alieleza kwamba mrufani alikamatwa baada ya kuwekwa mtego na shahidi wa kwanza na tatu wa Jamhuri na askari wanyamapori na polisi wengine, hivyo sababu zisizoeleka haziwezi kufanya cheti cha ukamataji kuwa haramu.
Kuhusu hoja ya kutothibitishwa kwa kesi hiyo bila shaka, Wakili huyo alieleza kuwa mrufani alikamatwa akiwa na meno hayo ya tembo aliyokuwa anahitaji kuuza na kupitia mashahidi wa Jamhuri walithibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.
Baada ya kujibu hoja zote tisa za rufaa, mrufani huyo alidai mashtaka hayo yaliandaliwa kumtia hatiani bila sababu halali na kuwa alikamatwa tangu mwaka 2017 na kuwekwa rumande hadi 2020 bila dhamana na kuomba Mahakama kuchunguza sababu zake na kumtendea haki.
Majaji walianza na msingi wa pili wa cheti cha kukamata ambacho kilijazwa na kusainiwa kituo cha polisi, kushindwa kujaza na kusaini cheti cha kukamata mahali, linaweza kutajwa kama sababu dhaifu.
Walieleza kusaini cheti cha kukamata kuna kanuni iliyoandaliwa na Mahakama chini ya kifungu cha 38 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, bado ni halali, huku wakinukuu kesi ya Mahakama ya Rufaa.
Wanaeleza katika mazingira ya kesi hiyo, ushahidi wa shahidi wa kwanza haupaswi kusomwa kwa kutengwa na ushahidi wa mashahidi wengine hasa wa shahidi wa tatu ambaye aliieleza Mahakama mrufani aliwapeleka msituni umbali wa kilomita tatu kabla hajaenda kuchukua meno hayo.
Walieleza shahidi wa kwanza, alieleza alimuona mrufani akiwa amefungwa pingu, huku akiwa na mfuko nyuma yake ambapo baada ya kufika Kituo cha Polisi Mvuha alijaza hati ya kukamata.
“Tunadhani kilichofanywa na shahidi wa kwanza ndicho ambacho ofisa yeyote wa polisi mwenye busara angefanya kwa mahali pa kukamatwa kuwa eneo la msitu halikuwa jambo la kufaa kujaza na kusaini hati ya ukamataji, tunatupa hoja hii,” wameeleza.
Kuhusu hoja ya kushindwa kumwita shahidi wa kujitegemea kwa sababu matukio yalitokea msituni na hakuna mtu mwingine aliyepita wakati huo, wakili wa Jamhuri alikubaliana na shahidi wa tatu kuwa haikuwa rahisi kupata shahidi wa kujitegemea wakati huo.
Walisema kushindwa kupata shahidi wa kujitegemea hakukuwa na ukiukwaji wa kifungu wa sheria, bali hakukuwa na watu mahali pa kukamatwa na kuwa kifungu tajwa kinasomwa pamoja na kifungu cha 106 (1) (b) cha Sheria ya Wanyamapori.
Walileza vifungu hivyo huwapa maofisa hao uwezo wa kuingia, kupekua na kukamata bila hati au shahidi wa kujitegemea, isipokuwa pale ambapo kuna nyumba ya makazi.
Kuhusu hoja ya kesi kutothibitishwa pasipo kuacha shaka, walieleza wanakubaliana na Wakili wa Serikali, kwamba kulikuwa na ushahidi uliomtia hatiani mrufani kwa kosa aliloshitakiwa nalo kwa kuzingatia ushahidi wa mashahidi na vielelezo vilivyotolewa.
Baada ya kupitia hoja zote, majaji hao walikataa hoja hizo za rufaa na kuwa kwa kuzingatia waliyopitia hawaoni sababu za msingi za kubadilisha uamuzi wa Mahakama kwa sababu kesi hiyo ilithibitishwa bila mashaka yoyote na kutupilia mbali rufaa hiyo.