AMREF yaipongeza NMB kuchangia Sh60 milioni uzazi ni maisha Z’bar

SHIRIKA la AMREF Health Africa – Tanzania, limeipongeza Benki ya NMB kwa kuchangia vifaa tiba vya Sh. 20.17 milioni katika mwaka wa mwisho wa Kampeni ya Uzazi Salama ijulikanayo kama Uzazi ni Maisha, hivyo kufanya mchango wa jumla wa benki hiyo kufikia Sh. 60.17 milioni katika kipindi cha miaka mitatu tangu kampeni hiyo ianze mwaka 2022. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Uzazi ni Maisha inaendeshwa na AMREF kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar – kupitia Wizara ya Afya, ilizinduliwa mwaka 2022 na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ikilenga kukusanya Sh. bilioni moja ama vifaa tiba vyenye thamani hiyo kwa ajili ya kusambaza katika Vituo vya Afya 28, Zanzibar.

Waziri wa Afya Zanzibar, Nasoro Ahmed Mazrui (katikati), akikagua kitanda cha kujifungulia akina mama wajawazito mara baada ya kupokea sehemu ya msaada wa vifaa tiba kutoka kwa Meneja wa Biashara wa Benki ya NMB Zanzibar, Naima Said Shaame (wapili kulia), wakati wa hafla ya kupokea msaada wa vifaa tiba vilivyotolewa na wadau wa sekta ya afya ikiwemo NMB. Hafla hiyo ilifanyika jijini Zanzibar Juni 24, 2024. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Habiba Hassan Omari na wa pili kushoto ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa AMREF Tanzania, Dk. Serafina Mkuwa.

Kupitia Uzazi ni Maisha – kampeni iliyohusisha Matembezi, Mbio Fupi na Ndefu (Wogging – Walk-Jog-Run), imeingia katika mwaka wa tatu na mwisho, ambako imekusanya takribani pesa taslimu na vifaa tiba vya Sh. 743.5 milioni, kati ya hizo Sh. 60 milioni zikitolewa na Benki ya NMB pekee.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kwa Waziri wa Afya wa Zanzibar, Bw. Nassor Ahmed Mazrui, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkaazi wa AMREF Health Africa – Tanzania, Dk. Serafina Mkuwa, amesema kuwa bado kuna ahadi mbalimbali za jumla ya shilingi Mil. 900 kutoka kwa wadau tofauti.

Waziri wa Afya Zanzibar, Nasoro Ahmed Mazrui (katikati), akipokea sehemu ya msaada wa vifaa tiba kutoka kwa Meneja wa Biashara wa Benki ya NMB Zanzibar, Naima Said Shaame (kulia), wakati wa hafla ya kupokea msaada wa vifaa tiba vilivyotolewa na wadau wa sekta ya afya ikiwemo NMB. Hafla hiyo ilifanyika jijini Zanzibar Juni 24, 2024. kushoto ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa AMREF Tanzania, Dk. Serafina Mkuwa.

“AMREF tunaishukuru sana Serikali ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya kwa kufanikisha makusanyo haya, na wakati tukiwaomba wadau ambao hawajatimiza ahadi zao kufanya hivyo kabla ya mwisho wa mwaka, tunaiomba tena Serikali kusaidia gharama za kuingiza nchini ‘mobile van’ 10 zilizoko jijini Nairobi, Kenya.

“Shukrani zetu za dhati ziwafikie watu binafsi, taasisi, mashirika, kampuni na wadau wa afya walioguswa na kampeni yetu ya kuokoa maisha ya mama na mtoto, kiasi wakakubali kuchangia pesa na vifaa tiba hivi na vingine ambayo tumeshakabidhi, vinavyoenda kusaidia huduma za uzazi kote Zanzibar,” alisema.

Katika mahojiano maalum baada ya makabidhiano hayo, Dk. Serafina aliipongeza na kuishukuru NMB kwa kuchangia vifaa tiba vya Sh. 20.17 milioni vilivyotolewa katika hafla hiyo, na kufanya mchango wao wa jumla kufikia Sh. 60 milioni baada ya awali kuchangia Sh. 40 milioni katika mwaka wa kwanza.

“Kipekee na kwa dhati tunapenda kuishukuru Benki ya NMB kwa mchango wao mkubwa walioutoa katika kampeni yote ya Uzazi ni Maisha Wogging, ni msaada muhimu unaoenda kuchangia pakubwa lengo letu la jumla la kukusanya vifaa tiba kwa ajili ya Vituo vya Afya Teule 28.

“Tunawashukuru kwa sababu NMB imekuwa bega kwa bega sio tu na AMREF Health Africa, bali na Wizara ya Afya pia, tangu siku ya mwanzo wa kapeni hii mwaka 2022 na naamini hata sasa tunapoelekea kuhitimisha kampeni hii mwaka huu, ushirikiano wao nasi utaendelea,” alisisitiza Dk Serafina.

Kwa upande wake, Meneja wa Biashara wa NMB Zanzibar, Naima Shaame, alisema vifaa tiba walivyokabidhi kwa Amref Health Afrika – Tanzania, nayo kuvikabidhi kwa Waziri wa Afya wa Zanzibar, ni vitanda vya kujifungulia 11, mashuka 250 na mizani za kupimia uzito 30.

“Katika mwaka wa kwanza wa kampeni hii, NMB tulichangia vifaa tiba vyenye thamani ya Sh. 40 milioni, tukisukumwa na ukweli kwamba afya ni miongoni mwa sekta za kipaumbele kwa benki yetu na leo hii tuko hapa kukabidhi msaada wa Sh. 20.17 milioni kuokoa maisha ya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

“Tunawashukuru AMREF na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia Wizara ya Afya kwa ushirikiano waliotuonesha, tulivutiwa na malengo yao, na kutokana na kutambua wajibu wetu kwa jamii inayotuzunguka, tukawiwa kuchangia vifaa hivyo kwa ustawi wa afya ya kina mama Zanzibar.

“AMREF Health walipotuomba, tuliona ni fursa ya kuendeleza Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), tukajitosa kuhakikisha mama na mtoto wanabaki salama. NMB, siri ya mafanikio yetu ni mwananchi na tunamuangalia mteja tangu akiwa tumboni, tunapomtunza mama, tunalea mteja wetu wa baadaye,” alisema Naima.

Related Posts