Arusha. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hali ya uchumi nchini inazidi kuwa mbaya na watu wengi wakipitia ugumu wa maisha.
Kimesema wakulima wanakabiliwa na changamoto za kupanda kwa gharama za pembejeo na soko la mazao yao kutokuwa na bei nzuri, huku wanakutana wakikabiliwa na ukosefu wa malisho na huduma za mifugo kuwa ghali.
Hayo yalisemwa leo Jumatano Juni 26, 2024 na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwenye mkutano wa Operesheni +255 Katiba Mpya Kanda ya Kaskazini, uliofanyika Dongobesh wilayani Mbulu, mkoani Manyara.
Amesema wafanyakazi wa Serikali na sekta binafsi, wengi wanalalamikia kupanda kwa gharama za maisha, huku mishahara yao ikibaki palepale au kupanda kidogo pamoja na mfumuko wa bei nao ukiendelea kuathiri uwezo wa kununua bidhaa na huduma muhimu.
Pia, amesema biashara nyingi zimeathirika kutokana na hali hiyo, huku baadhi ya wafanyabiashara wakiamua kufunga shughuli zao kutoka na kupanda kwa gharama za uendeshaji.
Hivyo, chama hicho kimeungana na wafanyabiashara nchini waliofunga biashara zao wakielezea kukerwa na usumbufu wa kodi, na kuwataka wafanyabiashara wote nchini kuungana na wenzao hadi Serikali iwasikilize.
Akitolea mfano wafanyabiashara wa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, Mbowe amesema ndiyo wanaoongoza kuiingizia mapato Serikali kwa kuwa wanafanya biashara na wenzao kutoka nchi mbalimbali kila siku.
“Sasa wanasema kuliko waendelee kufanya biashara, ni heri wafunge maduka. Amekwenda mkuu wa mkoa badala ya kuwasikiliza, anawatisha. Kariakoo maokoto ya kodi wanayotoa nchi hii ni makubwa,” amesema Mbowe.
Amesema kilio kikubwa cha wafanyabiashara ni mitaji yao inaisha kwa sababu ya kodi, “mfano mfanyabiashara ana mtaji wa Sh5 milioni halafu anatozwa faini Sh15 milioni, anazitoa wapi ili akalipe hiyo faini?
“Jana walifunga Mbeya, Mwanza, leo Arusha, Iringa na kwingine wamefunga. Mimi nawaambia wafanyabiashara wote nchi hii hadi Dongobesh mnaosumbuliwa na TRA fungeni maduka mpaka Serikali iwapigie magoti,” amesema Mbowe.
Mbowe ameitaka Serikali itimize wajibu wake, isiwabebeshe mzigo wafanyabiashara, iache kununua mashangingi yanayogharimu fedha nyingi ambazo zingeweza kwenda kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
“Kila gari moja hugharimu Sh500 milioni na kwa mwaka Serikali inanunua magari ya Sh800 bilioni kwa kodi za wananchi, huku wananchi wakiishi maisha magumu,” amedai Mbowe.
“Nawaomba sana, haitoshi kulalamika, inapaswa tuchukue hatua hakuna lugha inayoweza kuongezeka zaidi ya kuiondoa CCM madarakani, kwani kodi hizo zinawafanya muwe masikini,” ameongeza.
Amesema kilio cha wananchi kinatokana na kuongozwa na watu ambao hawakuwachagua na sasa wako Dodoma kutunga sheria na baadhi yao ni mawaziri.
Amesema ukienda kwenye mataifa yanayojitambua, Serikali zake zina wajibu wa kuhakikisha kila mwananchi anapata kazi ili apate kipato halali.
Amesema Serikali inaposhidnwa hilo, humlipa mwananchi mshahara ili ihakikishe ana kazi halali na analipa kodi, hali ambayo ni tofauti na Tanzania.
“Ndipo tunapoona tofauti baina ya nchi hizo za Ulaya na za Afrika Tanzania ikiwamo ambayo tayari imetimiza miaka 60 ya uhuru lakini watu wake bado ni hohehahe,” amesema Mbowe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema hali mbaya ya uchumi imesababisha vijana wengi kuwa walevi na wananchi wamepoteza matumaini.
Amesema Chadema ikipewa ridhaa ya kuongoza nchi, ndani ya miaka 10 itarekebisha hali ya uchumi.
“Hii nchi inahitaji miaka 10 kurekebishika, Watanzania wanaweza kuishi maisha mazuri kuliko watu wa Sweden au Uingereza ambao hawana rasilimali kama tulizonazo Tanzania,” amesema Lema.
Amesema Tanzania inaweza kujikomboa kwa kuwa inamiliki madini ya almasi, dhahabu, rubi, Tanzanite, gesi na madini mengine mengi yenye thamani kubwa.
Ametoa rai kwa wananchi kuacha kunung’unika pembeni, bali uchaguzi ukiwadia, wafanye uamuzi ulio sahihi.