DNA ya damu kwenye jambia yafanana na mate ya mshtakiwa wa tatu kesi ya Milembe

Geita. Vipimo vya vinasaba vilivyofanywa na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali vimebaini kuwa mpanguso (swab) wa damu kutoka kwenye mpini au mshikio wa jambia lililotumika kumuua Milembe Suleman (43)  ina uhusiano na mpanguso wa vinasaba vya mate vya mshtakiwa wa tatu Genja  Pastory.

Katika kesi hiyo, ushahidi uliotolewa leo Jumatano Juni 26, 2024 na shahidi wa 26 ambaye ni mkemia kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ally Kanenda ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Geita kuwa alipokea vilelezo vinne kutoka Polisi Geita, vikihitaji uhusiano wa chembechembe za urithi wa vinasaba.

Ameieleza Mahakama kuwa katika uchunguzi  wa awali, vielelezo vyote viligawanyika katika maeneo manne ambayo ni pamoja na uchenjuaji wa vinasaba kutoka kila kielelzo.

Eneo la pili ni uchunguzi wa kutambua wingi wa vinasaba baada ya uchenjuaji, kuongeza eneo linalotumika kwa binadamu katika uchambuzi wa vinasaba pamoja na uchambuzi wa eneo lililoongezwa kwenye vinasaba.

Kanenda amedai matokeo ya awali yalibaini katika kielelezo A, mpanguso wa damu kutoka kwa Milembe kimedhihirisha ni cha mmiliki mmoja mwenye jinsi ya kike.

Kielelezo B, mpanguso wa damu kutoka kwenye jambia kimedhihirisha kuwa ni cha mmiliki mmoja mwenye jinsi ya kike huku kielelezo C, mpanguso wa damu kutoka kwenye mpini wa jambia kimedhihirisha kuwa ni cha mmiliki mmoja mwenye jinsi ya kiume.

Akiongozwa na wakili kutoka ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Merito Ukongoji, shahidi huyo amesema kielelezo D cha mpanguso wa mate ya mtuhumiwa Genja Pastory (mshtakiwa wa tatu), kimedhihirisha kuwa ni cha mmiliki mmoja wa kiume.

Katika hitimisho la uchunguzi, Kanenda imebainisha kuwa katika kielelezo A, mpanguso wa damu kutoka kwa marehemu Milembe umedhihirisha kuwa na uhusiano wa mpangilio wa vinasaba na kielelezo B kutoka kwenye mpanguso wa damu uliopo kwenye jambia.

“Lakini pia Mheshimiwa Jaji, kwenye kielelezo C, mpanguso wa damu kutoka kwenye mpini wa jambia kimedhihirisha kuwa na uhusiano na mpangilio wa vinasaba vya kielelezo D ambacho ni mate ya mtuhumiwa Genja Pastory,” amedai shahidi huyo.

Shahidi mwingine ambaye ni askari Polisi Brandino Chang’a aliyekuwa kwenye kituo cha Polisi Nyakalilo Wilayani Sengerema, ameieleza Mahakama kuwa akiwa kazini, alipigiwa simu na Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mwanza akimtaka kwenda kukamata watuhumiwa waliopo kata ya Ilenza.

Amedai baada ya kupewa maelekezo hayo alitumia wasiri wake kujua alipo mtuhumiwa Genja Pastor na mwenzake Pastory na kupata taarifa kuwa anapatikana Kijiji cha Igego.

“Baada ya kupata taarifa kutoka kwa msiri wangu niliwachukua askari wenzangu na kwenda Ilenza na kupitia msiri wangu tulielezwa mtuhumiwa yupo kwenye saluni tulimkamata na kurudi kituoni na kwenye mahojiano alimtaja mtu aitwaye Pastory kuwa walishirikiana kwenye mauaji pamoja na Cecilia aliyekuwa mganga wa kienyeji,” amesema.

Baada ya kumkabidhi mtuhumiwa kwa Koplo Michael kwa ajili ya maelezo ya onyo, walianza safari ya kwenda kumkamata Pastory na Cecilia na walipofika kwa Pastory, hawakumkuta na kwenda kwa Cecilia aliyedai watuhumiwa hao wawili walifika kwake na kuchukua dawa ya kujitibu kwa lengo la kuondoa mkosi baada ya kufanya mauaji.

Shahidi huyo amedai siku iliyofuata, Mei 6, 2023 saa tatu asubuhi alipigiwa simu na viongozi wa Kijiji cha Iyenza wakitoa taarifa kuwa mtuhumiwa waliyekuwa wakimtafuta wamemuona amejinyonga kwenye msitu wa Bulindi.

Hata hivyo kulingana na muda, kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Juni 27, 2024 na upande wa mashtaka utaendelea kutoa ushahidi wake.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni, Dayfath Maunga (30), Safari Labingo (54), Genja Pastory, Musa Lubingo (33) na Ceslia Macheni (55), ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kumuua Milembe Seleman.

Related Posts