Mwanza. Wakati matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wasichana na watoto yakishamiri nchini, wadau wa masuala ya jinsia wametaja sababu nne zinazochangia mabinti kutopaza sauti na kuripoti vitendo hivyo katika mamlaka zinazohusika.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni wiki moja tangu Jeshi la Polisi mkoani Mwanza litoe taarifa ya kumshikilia na kumhoji aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahya Nawanda kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Mwanza.
Akizungumza leo Jumatano Juni 26, 2024 wakati wa hafla ya kuwajengea uwezo walimu tarajali kuhusu mbinu za ufundishaji na ujifunzaji zinazozingatia usawa wa kijinsia yanayofanyika Chuo cha Ualimu Butimba jijini Mwanza, mwalimu tarajali wa chuo hicho, Elizabeth Richard amesema baadhi ya mabinti wanakosa ujasiri, hawajitambui na kutojua thamani yao.
Huku akitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi yao kutoweza kujisimamia, Elizebth amesema ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ukatili, jamii inapaswa kumjengea uwezo ili atambue thamani yake, kuwa jasiri na mwenye uwezo wa kutatua changamoto zinazomkabili, ikiwemo ukatili wa kijinsia.
“Tuwaambie kwamba wana thamani na wajitambue, ili kuwasaidia kufika mbali, kuzishinda changamoto na kutimiza ndoto zao,” amesema Elizabeth.
Akiunga mkono sababu zilizotolewa na Elizabeth, mwanafunzi wa chuo hicho, Mapato Mgasa amesema sababu hizo zinachangia watoto wa kike kuathiriwa wa ukatili, ikiwemo kukumbana na ubaguzi kwenye uchaguzi wa serikali za wanafunzi katika taasisi za elimu hata wanapofika ofisini hushawishika na kuingia majaribuni kwa waajiri.
“Jamii inapaswa kuwajengea uwezo watoto wa kike wa namna ya kukabiliana na vishawishi wanapoona dalili tofauti, vinginevyo hata jitihada zinazofanyika kuwakwamua kiuchumi, kijamii na kielimu zinaweza zisifanikiwe,” amesema Mgasa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake Waelimishaji Afrika (Fawe) Tawi la Tanzania, Neema Kitundu, utoaji wa mafunzo kwa walimu tarajali na wakufunzi ni miongoni mwa njia inayotumika kujenga jamii inayotambua changamoto anazokumbana nazo watoto na namna ya kumsaidia.
Kitundu amesema kupitia kujenga uwezo kwa walimu tarajali na wakufunzi hao, wanafunzi watafunguka matatizo na ukatili wanaopitia katika familia na jamii zao, ili kurahisisha ufuatiliaji na uchukuaji hatua dhidi ya watu wanaotuhumiwa kutenda ukatili huo.
“Leo tumewajengea uwezo utakaowasaidia na kuwakomboa wanafunzi dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji. Pia watatoa elimu kwa wanafunzi wao ili wajiheshimu, kujitambua, kujithamini na kujua madhara ya tamaa ili wasikumbane na vitendo vya ukatili na udhalilishaji,” amesema Kitundu.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Mkuza Mitaala Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA), Given Mbakilwa amesema usawa na ukatili wa kijinsia ni miongoni mwa maneno yaliyojumuishwa kwenye maboresho ya mtaala wa elimu wa mwaka 2023, ili kuanza kujenga uelewa kwa wanafunzi kuhusu ukatili kuanzia ngazi ya awali.
“Tumegundua watoto wengi wanafanyiwa ukatili wa kijinsia, lakini wanaogopa kutoa taarifa kwa sababu pengine aliyefanya ni mwalimu anayeogopeka kwa hiyo anahofia hatima yake, kwa hiyo tunawajengea kwanza ule uwezo wa wao kujiamini na kujua njia mbadala za kujiepusha nao,” amesema Mbakilwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Dawati la Jinsia Chuo cha Ualimu Butimba, Lilian Nyaga amesema; “tunafurahi kupata mafunzo haya ambayo yatatusaidia kuboresha utendaji kazi wetu. Mwanzoni wanachuo walikuwa hawajui jinsi ya kupata msaada wa vitendo vya ukatili wa kijinsia, lakini baada ya elimu hii wataweza kuzungumza kwa uwazi na kujua pa kupeleka shida zao.”
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 ya ufanisi katika usimamizi wa hatua za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini imeonyesha (bila kutaja idadi) matukio ya ukatili yameongezeka kwa asilimia 80 katika kipindi cha miaka mitano (2018 hadi 2022).