Hoja saba zapata majibu Bunge likipitisha bajeti

Dodoma. Sh49.35 trilioni za bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 zimeidhinishwa rasmi na Bunge, miongoni mwa wanufaika wakiwa wakandarasi wa ndani na wastaafu waliopunjwa kutokana na kikokotoo kipya.

Serikali kwa mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai mosi, itashughulikia ‘wapigaji’ serikalini kwa kuzungumza na vyombo vinavyohusika na maadili, huku suala la upungufu wa sukari likitarajiwa kuwa historia mwakani.

Hoja hizo ambazo ni miongoni mwa saba za wabunge zilizohitaji majibu ya Serikali zimejibiwa leo Juni 26, 2024 na mawaziri wanne; Dk Mwigulu Nchemba (Fedha), Profesa Kitila Mkumbo (Mipango na Uwekezaji), Innoncent Bashungwa (Ujenzi) na Deogratius Ndejembi (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu).

Hoja zingine zilizojibiwa na mawaziri hao ni matumizi ya Dola ya Marekani, pendekezo la tozo ya Sh385 kwenye kilo ya gesi kwenye magari, na matumizi ya malipo kwa mfumo wa kidijidali.

Bajeti hiyo imepita kwa kura 362 kati ya 381 waliokuwemo bungeni, sawa na asilimia 92.3. Haopakuwa na kura za hapana na wasiokuwa na uamuzi walikuwa 18.

Akizungumzia tozo ya Sh385 kwenye gesi, ambayo ililalamikiwa na wabunge wengi kwamba itasababisha mfumuko wa bei na kuongeza gharama za maisha, Dk Mwigulu amesema hatima ya pendekezo hilo itajulikana kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha utakaowasilishwa bungeni Juni 27.

“Serikali imepokea maoni ya wabunge na wataalamu wanaendelea kukamilisha sheria ya kodi na tozo, hivyo suala hilo litafanyiwa kazi kwa uzito,” amesema Dk Mwigulu.

Kuhusu kubana matumizi ya Serikali, Dk Mwigulu amesema ameelekeza kukatwa fedha za mafuta ya magari ya Serikali kwa ajili ya kujenga vituo vya gesi katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na wataendelea kujenga vituo hivyo kwenye miji mingine nchini.

Amesema katika kipindi cha mpito kuelekea matumizi ya gesi, watatumia mafuta na gesi kwenye uendeshaji wa magari ya Serikali.

Kuhusu ‘upigaji’ fedha za umma, Dk Mwigulu amesema si kitu cha kupuuza na kwamba, wameendelea kuongea na vyombo vinavyosimamia maadili kuhakikisha wanakomesha masuala ya upotevu wa fedha wakati wa makusanyo.

“Mengine huwa yanaanzia ngazi ya kijiji, watu wanachukua mashine za POS wanakusanya wanapotea, wengine wanachukua kingine kinaenda serikalini na kingine kinapita njia hizo nyingine. Tumeyapokea hayo yote na tunafanyia kazi,” amesema.

Akizungumzia madeni ya wakandarasi na wazabuni, Dk Mwigulu amesema hilo wanaliandalia mpango mahususi na kwamba, wataenda kuwalipa wanaowadai na hasa wakandarasi wa ndani.

“Na siyo kwamba sasa hivi ndiyo tunaanza, kiporo chake kilikuwa kikubwa. Kuna watu walishasahau kama kuna siku watalipwa fedha hizi. Rais akasema walipeni hawa ili fedha ziongezeke katika mzunguko. Tulianza na Sh200 bilioni, mwaka uliopita Sh400 bilioni  na mwaka huu tulikuwa na Sh600 bilioni,” amesema.

Amesema wanatengeneza mpango na ukishamalizika watakaa na kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na kuwaeleza.

Amesema hoja zilizotolewa na wabunge kuhusu Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2024 zikitekelezwa ni dhahiri zitaathiri matumizi ya Serikali na bajeti za kisekta.

Dk Mwigulu amesema wamekaa na watalaamu na kukubaliana kubana matumizi kufidia fedha ambazo walishazipanga katika wizara za kisekta, hatua inayolenga kuhakikisha miradi ya maendeleo haikwami.

Amesema suala la ununuzi wa magari kwa watumishi wanaostahili kuwa nayo, linafanyiwa kazi kuhakikisha halileti usumbufu katika utekelezaji.

“Kwa mfano askari anayefanya doria huwezi kumweleza nenda na gari lako, lakini upande wa hoja ya watumishi kupata magari yao itakuwa kando. Tumeangalia hata wale ambao wako ‘field’, jambo hili linafanyiwa kazi na wenzetu walioko utumishi pamoja na ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi ili kupata utaratibu ambao hautaathiri shughuli za Serikali,” amesema.

Hata hivyo, Dk Mwigulu amesema amemwelekeza Mlipaji Mkuu wa Serikali kuwa kwenye takribani Sh129 bilioni zilizoelekezwa katika ununuzi wa magari, akate zaidi ya asilimia 50,  wabakize Sh50 bilioni zipelekwe maeneo yenye uhitaji.

Amesema kulikuwa pia na Sh67 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya magari hayo ambazo nazo zitatakiwa kukatwa zaidi ya asilimia 50 na ameagiza kukatwa asilimia 50 ya gharama za fedha ambazo zilikuwa zitumike kwa ajili ya mafuta.

Amesema watakata katika fedha za matumizi ya kawaida kwa ajili ya kupeleka kwenye miradi ya maendeleo.

“Fedha hizi zitakwenda katika miradi ya maendeleo ambayo itaathirika na marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2024, zitakwenda katika miradi ya maji, umeme na mingine,” amesema.

Dk Mwigulu amesema mawaziri waliopita wa fedha waliwahi kutoa malekezo juu ya katazo la matumizi ya dola katika manunuzi nchini.

Hata hivyo, amesema wanapoanza kutekeleza hilo mwaka huu wa fedha watatengeneza kanuni na wataweka adhabu kwa sababu sheria ipo inayosema Shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali inayotumika ndani ya nchi.

“Tuache kuifuatilia dola inavyoenenda tunaposema tutumie fedha ya Tanzania pia tunataka nukuu ya fedha kwa Kitanzania,” amesema.

Kuhusu uchumi wa kidijitali, Dk Mwigulu amesema suala la fedha mtandao (cashless) ni muhimu ambalo wanaendelea nalo.

“Sisi ndani ya Serikali tutaongeza jitihada za kujenga mifumo. Tukishamaliza tutaenda kwa utaratibu kwa ulazima wa kisheria. Kwanza ni kutoa elimu na kujenga mifumo ili tutakaposema nchi nzima tuhamie kwenye utaratibu huo tuwe tumeshamaliza,” amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kwa mwaka ujao wanatarajia mahitaji ya Tanzania ya sukari yataakuwa tani 650,000 kwa mwaka.

Amesema mwaka jana kabla ya mvua za El Nino, Tanzania ilishapiga hatua kwa kuzalisha tani 460,000 kwa mwaka, lakini kutokana na mvua uzalishaji viwandani uliyumba hadi tani 392,704.

Amesema kutokana na uwekezaji unaoendelea nchini na kama hakutajitokeza changamoto za El Nino hadi Julai 2025 uzalishaji utafikia angalau tani 520,000 na lengo la Serikali ni kufikisha tani 700,000 mwaka 2025/26.

Profesa Mkumbo amesema lengo la kulinda viwanda vya sukari liko palepale ili ifike mahali nchi iweze kujitegemea na kuuza nje.

Waziri amesema wanafanya uwekezaji mkubwa katika eneo hilo ikiwemo kuweka Sh7.2 bilioni kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora za miwa.

Amesema wametenga Sh12.5 bilioni kwa ajili ya miundombinu ya umwagiliaji wa mashamba ya miwa hasa katika bonde la Kilimanjaro.

Amesema hivi sasa kampuni ya saba kutoka Ethopia inafanya upembuzi yakinifu katika bonde la Kilombero ili kukuza umwagiliaji katika eneo hilo.

“Hii itakuwa ni hatua kubwa katika kuongeza uzalishaji, tumegawa kitalu kipya bure hekta 400 kwa wakulima waweze kuzalisha. Kwa hiyo, mtu anayesema hatua zote tulizozichukua hivi karibuni lengo lake ni kukatisha tamaa wawekezaji katika sekta ya sukari, hajui alisemalo,” amesema.

Amesema Serikali pia imesamehe kodi Sh240 bilioni kwenye viwanda vya sukari nchini ili kuweka mazingira mazuri ya wao kuwekeza.

“Sisi tunaamini kuwa kwa jitihada hizi ifikapo mwaka kesho suala la sugar gap (upungufu wa sukari) litakuwa historia,” amesema.

Kuhusu uagizaji wa sukari, Profesa Kitila ni lazima Serikali ichukue hatua ya kulinda walaji katika soko huria kwa sababu zinapokosekana bidhaa inayolaumiwa huwa ni Serikali.

“Hatua hizi hazilengi katika kudhoofisha uzalishaji katika sekta ya sukari, bali Serikali inachukua hatua za msingi za kulinda walaji dhidi ya mabavu ya soko huria. Serikali ni mwekezaji katika sekta ya sukari nchini huwezi kutegemea ijihujumu yenyewe,” amesema.

Amesema uwekezaji wa Serikali katika viwanda vyote vya sukari ni takribani Sh4.4 trilioni.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Deogratius Ndejembi amesema kikokotoo kilikuwa kilio kikubwa kwa wafanyakazi na wabunge,  wakitaka kuongezwa mafao ya mkupuo na Rais Samia Suluhu Hassan alikisikia.

Juni 13, 2024, Serikali iliongeza kikokotoo cha mafao ya mkupuo kutoka asilimia 33 hadi 40 kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na 33 hadi asilimia 35 kwa wale wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Ndejembi amesema katika kutatua changamoto hiyo walitenga Sh155 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/25.

Amesema fedha hizo zinakwenda kutumika katika kunyanyua kiwango cha kutoka asilimia 33 hadi 40 kabla ya Julai 2022 na kutoka asilimia 33 hadi asilimia 35.

Amesema Serikali itaendelea kuangalia ni namna gani inarejea katika asilimia 50, kama ilivyoombwa na wabunge na vyama vya wafanyakazi nchini.

“Hao wanaokwenda kulipwa siyo wale wanaokwenda kustaafu Julai mwaka 2024, wanakwenda kulipwa wote hata wale waliostaafu Julai 2022,” amesema.

Amesema wastaafu 17,068 waliostaafu kuanzia Julai 2022 wanakwenda kulipwa mapunjo yao ya asilimia saba na wale waliokuwa wakipata asilimia 33 watalipwa mapunjo yao ya asilimia mbili.

Waziri Bashungwa amesema walishakaa na Waziri wa Fedha na benki nchini kuangalia namna ambavyo Serikali itashirikiana nazo kupunguza hatari ya mikopo (risk portfolio) inayoenda kwa wakandarasi wazawa.

“Jambo hili tutalisimamia, tutakaa na mabenki tuweze kukubaliana namna ambavyo makandarasi wanaweza kuanza kazi wakapata advance payment (malipo ya awali) lakini pale Serikali inapochelewa kuwalipa, basi mabenki yetu yaweze kuwarahisishia malipo kwa kutumia security (dhamana) ya mikataba tunayoingia nao,” amesema.

Related Posts