Dar es Salaam. Wadau wa biashara na wanasiasa, wametaja mambo manne ambayo Serikali ya Tanzania ikiyatekeleza kwa ufanisi huenda ikapunguza changamoto ya migomo ya wafanyabiashara inayojitokeza mara kwa mara, hasa eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Mambo hayo ni kuangalia upya sheria ya kodi, kupunguza kodi, kufanya majadiliano, Serikali kuyashughulia mambo wanayokubaliana na wafanyabiashara kupitia vikao vinavyoketi baina yao kwa nyakati tofauti.
Wadau wameelea hayo leo Jumatano Juni 26, 2024 wakati wakichangia mjadala wa Mwananchi X space (zamani Twitter) uliokuwa na mada ya ‘Nini kifanywe, ili kumaliza kero za wafanyabiashara nchini’.
Ushauri umekuja ikiwa leo imeingia siku ya tatu tangu wafanyabiashara wa Kariakoo wagome kufungua maduka, wakieleza kukerwa na usumbufu wanaoupata kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Licha ya Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kutangaza kusistishwa kwa ukaguzi wa risiti za kieletroniki (EFD), wafanyabiashara hao wameendelea kusimamia msimamo wa kutofungua maduka.
Mgomo sasa umeenea katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Dodoma, Iringa, Mtwara, Kigoma na Mbeya na wafanyabiashara wa maeneo hayo, wamefikia uamuzi huo kwa madai ya utitiri wa kodi na tozo huku wakishinikiza mazingira mazuri ya biashara.
Akichokoza mjadala huo, Mhariri wa Uchumi gazeti la Mwananchi, Ephrahim Bahemu ameishauri Serikali kufanya majadiliano na wafanyabiashara, ili kuleta maelewano yatakayohakikisha changamoto za migomo haitokei tena.
“Kikubwa ni maelewano kati ya Serikali na wafanyabiashara, ni muhimu kufanya majadiliano ya pamoja ili kumaliza tatizo hilo. Vitu vingine vinavyolalamikiwa vipo katika sheria ya kodi,” amesema Bahemu.
Bahemu amesema ukiona watu wanaopiga kelele katika kodi basi ipo juu, akifafanua dawa siyo kusitisha ukaguzi wa risiti, bali kuipunguza ili kuwapa unafuu wafanyabiashara.
“Serikali iweke kodi ambayo wafanyabiashara watailipa bila kupata maumivu, ili mwisho Serikali ikusanye kodi kwa ufanisi kwa ajili ya maendeleo ya utekelezaji wa bajeti.
“Serikali ipitie upya kodi wanazolalamikia wafanyabiashara, kwa uchambuzi wangu mdogo ni tatizo la kodi, lakini likiangaliwa upya litaondoa changamoto hii,” amesema Bahemu.
Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude, amesema mazingira ya biashara na kodi yana changamoto, hivyo Serikali inapaswa kushughulikia kwa wakati waliokubaliana na wafanyabiashara, kisha kutoa mrejesho.
“Kodi inapaswa kulipwa ili tupate huduma za jamii, afya, shule, sasa tusipoilipa tutalazimika kukopa,” amesema Mkude.
Hata hivyo, Mkude amesema sheria ya kodi haijawahi kuwa nyepesi dunia kote, akiwataka wafanyabiashara kuwa na watalaamu watakaowasaidia katika kuichambua.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, kodi ni mchakato wa siasa na changamoto zake kamwe haziwezi kuisha kwa haraka.
Kwa upande wake, Makamu mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (bara), Isihaka Mchinjita ametaka mazungumzo yaliyofanywa kati ya viongozi wa Serikali na wafanyabiashara yaakisi uwazi, si kutafuta baadhi ya viongozi waliorubuniwa.
“Serikali ifanye majadiliano yenye uaminifu na wafanyabiashara, si kutoa zinazolenga tu kumaliza mgomo wa wafanyabiashara, wanataka mgomo kuisha.
“Tunamtaka Kamishna wa TRA kufumua uongozi mzima wa Mkoa wa kikodi wa Kariakoo na kuhamisha wafanyakazi wote wa taasisi hiyo na kuwapeleka wengine kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam,” amesema.
Naibu Spika wa Bunge la Wananchi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Lumola Kahumbi amedai sheria za kodi zilizopo zimepitwa na wakati, zinawafilisi wafanyabiashara, lakini pia zinatoa mwanya wa mazungumzo na kutengeneza mazingira ya rushwa.
“Mimi nilijua suala la mgomo limekwisha maana viongozi wa kuu wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliingilia kati, lakini umetokea tena. Sheria ya kodi iandikwe upya na kufuata taratibu zote, ikiwemo kuwashirikisha wadau,” amesema Kahumbi.
Naibu Katibu Mkuu (Bara) Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Eugen Kabendera, amesema kukiwa na mazingira na sheria rafiki itakayowavutia mfanyabishara kulipa kodi kwa urahisi.
“Kwa mgomo huu unaonyesha wafanyabiashara wetu wamechoka kunyanyaswa, Chauma tunatamani kuona Rais Samia Suluhu Hassan awe na sikio la kusikia kilio cha wafanyabiashara hawa,”
“Serikali iwe na sikio sikivu, maana mambo yakiendelea wafanyabiashara watahamia nchi nyingine ambako hakuna mgomo. Huu mgomo una sauti na picha kubwa wasiposikiliza kwa wakati…” amesema Kabendera.
Akichangia mjadala huo, Dk Faraja Krisomus, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ameshauri kurekebisha sheria zinazolalamikiwa na wafanyabishara. Amesema mwaka jana wafanyabiashara walikutana na Waziri Mkuu na walitaja changamoto zikiwemo za kisheria, lakini hazijafanyiwa kazi.
“Jambo jingine ni kutengeneza mfumo mzuri wa kulipa kodi, ili tozo zote zinazohusika na biashara zao zitozwe na TRA badala ya kusumbuliwa na kila taasisi. Tozo zote zikishatozwa na TRA na kupelekwa hazina, hizo taasisi zipewe mgawo wao kutoka hazina.
“Serikali iwatafutie njia nzuri zaidi wamachinga ya kufanya biashara zao badala ya kuwaruhusu kupanga biashara zao pembeni au nje ya maduka makubwa ya wafanyabiashara,” amesema Dk Kristomus.
Mwananchi wa kawaida, Dk Shimmy Sima, akichangia mjadala huo amesema ‘maana halisi ya Serikali kusitisha ukaguzi wa risiti, maana yake wafanyabiashara wanakwepa kodi. Wanakwepa kodi kwa sababu siyo rafiki.
“Mtu hana sababu ya kutolipa kodi kama ni rafiki kwake, wengi wana shida na kodi kubwa, Serikali irudi kukusanya kodi kidogo ili kila Mtanzania ajivunie kuilipa,” amesema.