Mbowe, Semu wachaguliwa kuiongoza TCD

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Sambamba na Mbowe, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kituo hicho.

Mbowe anashika nafasi hiyo akimrithi, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliyemaliza muda wake.

Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatano Juni 26, 2024 na Mkurugenzi wa TCD, Bernadetha Kafuko inaeleza viongozi hao wamepatikana baada ya uchaguzi.

Inaeleza uchaguzi huo umefanyika katika mkutano mkuu wa TCD uliofanyika leo Jumatano, jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, imeelezwa vyama vya Chadema, ACT Wazalendo, CUF na NCCR Mageuzi vimeshiriki.

Kwa mujibu wa Katiba ya TCD, viongozi hao waliochaguliwa watatumikia nafasi hizo kwa kipindi cha mwaka mmoja, kisha watachaguliwa wengine.

“Uenyekiti wa TCD unapatikana kwa mzunguko wa vyama na sasa imefika zamu ya Chadema kuongoza uenyekiti. Chadema tunapokea wajibu wakati ambao Taifa linahitaji kuwa na uchaguzi huru na wa haki.

“Tutaweka kipaumbele hoja ya kuendelea kuunganisha vyama na wadau kuwezesha chaguzi za 2024 na 2025 zinakuwa huru na haki,” amesema John Mnyika, katibu mkuu wa Chadema.

Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo-Bara, Isihaka Mchinjita amewapongeza Mbowe na Semu akisema: “Ni matarajio yetu kuwa mtakiongoza kituo hiki kuwa chemchem ya kupigania demokrasia ya kweli nchini. Ninawatakia kila la kheri.”

Naye Kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amewapongeza viongozi hao kwa kuchaguliwa na kusema: “Pongezi zangu za dhati kabisa kwa Mbowe kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa wa TCD. Hii ni imani kubwa viongozi wenzako wamekupa. Vilevile nampongeza Semu kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti. TCD ipo kwenye mikono salama kabisa. Hongera sana Profesa Lipumba kwa kumaliza muda wako wa Uongozi.

Related Posts