Mfanyabiashara akutwa amefia ndani Arusha

Arusha. Mfanyabiashara, Shangwe Julius (35) amekutwa amekufa ndani ya nyumba yake iliyopo kata ya Olgilai, Wilaya ya Arumeri, mkoani Arusha.

Mfanyabiashara huyo wa bidhaa za kilimo amekutwa amekufa ndani ya nyumba yake, huku baadhi ya wakazi wakidai kifo hicho kimesababishwa na matumizi makubwa ya pombe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo amethibitisha kutokea kwa kifo hocho na kusema chanzo halisi bado hakijafahamika.

“Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi wake, bado chanzo halisi kilichomuua mtu huyo hakijafahamika,” amesema kamanda Masejo.

Baba mdogo wa marehemu, Charles Hoseah amesema aliamka asubuhi kwenda kwenye shughuli zake na aliporudi saa sita mchana alimuulizia mwanawe (marehemu), lakini   kila mtu alikana kumuona kwa siku hiyo kama ilivyokuwa kawaida yake kutembea kwa majirani kusalimia watu asubuhi.

“Nilishangaa hadi saa sita kutokuonekana, hii inamaanisha hajaamka, hivyo niliamua kugonga mlango wake kumuamsha bila mafanikio, hadi hofu ikaanza kuniingia ndio nikampigia mwenyekiti aje atusaidie.

“Mwenyekiti alipokuja tulianza kugonga na watu wakaongezeka bila mafanikio kabla ya kukubaliana kuvunja mlango ndio tukamkuta kitandani amelala,” amesema na kuongeza;

“Hata hivyo katika kumgusa ndio tukaona hapumui na amepoa sana, ikiwa ni moja ya ishara kuwa amefariki,” amesema Hoseah na kuanza kulia.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kiutu kilichoko kata ya Olgilai, Saimon Naftali amesema alipigiwa simu na baba mdogo wa marehemu kuwa kuna tukio lisiloeleweka baada ya kumuamsha mwanawe bila mafanikio.

“Niliwahi eneo la tukio na kuungana na watu niliowakuta kugonga mlango wa nyumba ya marehemu bila mafanikio, hata dirisha lililoko karibu na kitanda chake lakini hakuna jibu ndio nikaamuru mlango uvunjwe na kumkuta amelala kitandani akiwa hapumui na amepoa sana” amesema mwenyekiti huyo.

Baada ya kuona hali hiyo, Naftali amesema aliamua kupiga simu polisi na walipofika walithibitisha kuwa amefariki baada ya kumpima na kuondoka na mwili wa marehemu.

Naftali ametumia nafasi hiyo kuwataka vijana waliofikia umri wa kuoa wafanye hivyo, ili kupunguza vifo kama hivyo.

“Vijana waoe, maana si ajabu hata huyu jamaa aliumwa usiku bila mtu wa nje kujua, lakini angekuwa na mke karibu angegundua na kutoa taarifa kwa ajili ya msaada,” amesema.

Related Posts