Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imemuamuru meneja mkuu wa kampuni ya uchimbaji madini ya African Barrick Gold Mine Ltd (ABG), kuilipa fidia ya Sh150 milioni familia ya Chacha Kiguha, mkazi wa Kijiji cha Nyamwaga, wilayani Tarime, kwa madhara iliyoyapata kutokana na shughuli za mgodi.
Awali, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza iliamuru maneja huyo kuilipa familia hiyo ya watu sita, Sh50 milioni kila mwanafamilia kwa madhara iliyoyapata kutokana na shughuli za mgodi ulio jrani na makazi yao.
Uamuzi huo uliotokana na kesi ya madai iliyofunguliwa na wanafamilia Chacha, mkewe Neema Chacha, na watoto wao wadogo Bhoke na Kiguha wakisimamiwa na baba yao; pamoja na Motongori na Surati, wakisimamiwa na mama yao.
Mahakama ya Rufani katika hukumu inayotokana na rufaa iliyokatwa na meneja huyo, imempunguzia fidia kutoka Sh50 milioni mpaka Sh25 milioni kwa kila mwanafamilia.
Uamuzi umetolewa na majaji watatu, Agustine Mwarija (kiongozi wa jopo), Abraham Mwampashi na Zainabu Muruke, katika hukumu ya Juni 14, 2024.
Hukumu hiyo imechapishwa katika mtandao wa Mahakama Juni 24, 2024.
Katika kesi ya msingi wanafamilia walidai kampuni hiyo ilikiuka wajibu wake wa uangalifu na kuwasababishia maradhi ya kifua, masikio, matatizo ya upumuaji na ngozi kutokana na moshi, milipuko ya baruti na vumbi kutoka mgodini.
Kutokana na maradhi hayo, Chacha na mkewe walidai wamekosa kipato kwani hawawezi kufanya shughuli za kiuchumi. Waliiomba Mahakama iamuru walipwe fidia ya jumla ya Sh600 milioni, kwa wanafamilia wote sita.
Mahakama Kuu katika hukumu iliyotolewa na Jaji Lameck Mlacha Agosti 3, 2016 ilikubali madai na ushahidi wao.
Iliamua mdaiwa alikuwa na wajibu wa kuhakikisha wadai hawadhuriki na shughuli za mgodi, na alikiuka wajibu huo.
Aliamua wanafamilia hao walipwe fidia ya madhara ya jumla ya Sh300 milioni, ikiwa ni Sh50 milioni kila mmoja.
Pia, aliamuru walipwe riba ya asilimia saba ya kiasi hicho kwa mwaka kuanzia tarehe ya hukumu mpaka tarehe ya kukamilisha malipo yote.
Maneja wa ABG hakuridhika na hukumu, alikata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga hukumu na tuzo ya fidia, akitoa sababu tisa za rufaa.
Mahakama ya Rufani katika hukumu imesema hakuna ushahidi unaothibitisha moja kwa moja kuwa maradhi ya tatizo la mfumo wa upumuaji, masikio na ugonjwa wa ngozi, yaliyodaiwa na wanafamilia hao yalisababishwa na shughuli za mgodi huo.
Badala yake Mahakama imesema madhara pekee yaliyothibitika iliyopata familia hiyo kutokana na shughuli za mgodi ni usumbufu.
Katika kuamua iwapo matatizo ya maradhi kwa wanafamilia yalisababishwa na shughuli za mgodi au la, Mahakama ilirejea na kuzingatia ushahidi wa mashahidi wawili wa pande zote.
Mashahidi hao ni Dk Nego Nyakeboko, aliyekuwa Mganga wa Wilaya (DMO) Tarime, aliyekuwa shahidi wa tatu upande wa mdai, aliyewatibu wanafamilia hao katika ya mwaka 2012 na 2013, na Dk Nicholas Mboya, aliyekuwa shahidi wa pili upande wa utetezi.
Kwa mujibu wa Dk Nyakeboko, Chacha alilalamikia matatizo ya kifua, masikio na mafua, lakini alipofanyiwa vipimo hakuwa na kifua kikuu (TB).
Mtoto Bhoke alikuwa akisumbuliwa na kikohozi, matatizo ya kupumua na upele mwilini, lakini pia alipomfanyia vipimo hakuwa na TB.
Watoto Motongori na Surati walilalamika maumivu ya kifua na walipewa matibabu ya pumu, baadaye walikuwa wakilalamika homa, mafua na matatizo ya kifua.
Baadaye walirejea hospitalini kwa matatizo yaleyale na ili kubaini chanzo cha maradhi hayo alipowahoji walieleza walikuwa wakiishi jirani na eneo la mgodi.
Hivyo alihisi kwa sababu ya ugonjwa wa mzio (allergy) kutokana na vumbi kutoka mgodini aliwashauri kuhama eneo hilo.
Kwa mujibu wa Dk Mboya vyeti vya matibabu vya wadai, maelezo ya maradhi yaliyokuwa yakiwakabili kila mmoja hayakuwa yamerekodiwa, hivyo madai kwamba ugonjwa wa kuvimba mapafu ulikuwa umesababishwa na moshi kutoka mgodini hayakuwa yamethibitishwa.
Kutokana na ushahidi huo, Mahakama imesema ushahidi uliowasilishwa hautoshi kuunganisha matatizo ya kiafya yaliyolalamikiwa na wanafamilia hao yalitokana na shughuli za mgodi huo na siyo jambo lingine.
Mahakama imesema ni mtizamo wake kwamba, kwa kuendesha shughuli za mgodi na hususan vumbi na milipuko ya baruti karibu na nyumba ya wanafamilia hao walio na umiliki wa eneo hilo kuliwaathiri.
“Hakuna ubishi kwamba wajibu rufaa waliathirika na kelele na ni dhahiri uendeshaji wa shughuli za mgodi ulisabisha utoaji vumbi ambalo kutokana na ukaribu wa mgodi na makazi ya wajibu rufani, vumbi liliwasababishia usumbufu,” inaeleza Mahakama ya Rufani.
“Hivyo, ingawa madai ya wajibu rufaa kwamba shughuli za mgodi ziliwasababishia maradhi hayakuthibitika, Mahakama inaamua shughuli hizo za mgodi ziliwasababishia adha, hivyo mrufani kuwajibika kuwalipa fidia ya madhara ya jumla,” imesema mahakama.
Mahakama pia, imesema Chacha alifanya uzembe uliochangia madhara ya usumbufu kwani alijenga jirani na eneo lenye leseni ya mgodi.
Mahakama imesema kanuni ni kwamba, pale mchango wa uzembe wa upande fulani unapokuwepo, kiwango cha fidia ya madhara ya jumla kinachotolewa kwa upande huo kinapaswa kupunguzwa kutegemeana na kiwango cha uzembe wake.
“Kwa kutambua asili ya madhara aliyoyapata mjibu rufani wa kwanza na familia yake, na kwa kuzingatia kiwango cha mchango wa uzembe wake, tunaona fidia ya Sh25 milioni kwa wajibu rufani kitakidhi haki ya kesi,” imesema Mahakama.
“Hivyo mrufani anaamriwa kulipa jumla ya Sh150 milioni pamoja na riba ya asilimia saba kwa mwaka kutoka tarehe ya hukumu ya mahakama ya awali mpaka tarehe ya kukamilisha malipo yote ya tuzo,” inasema hukumu.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa, mrufani aliwakilishwa na mawakili Faustin Malongo na Carolina Kivuyo. Wajibu rufani walijiwakilisha wenyewe pasipo wakili.
Kesi hiyo ilitokana na mgogoro wa malipo ya fidia ya ardhi baina ya Chacha na uongozi wa kampuni ya Barrick.
Kampuni hiyo ilipewa Leseni Maalumu ya Madini (LMM) katika vijiji vitano wilayani Tarime, mkoani Mara, kikiwemo Kijiji cha Nyamwaga, anakoishi Chacha na familia yake.
Katika uthamini uliofanywa na kampuni hiyo kwa wamiliki wa maeneo yaliyoathiriwa na leseni hiyo, Chacha alikataa kupokea fidia ya Sh1.7 milioni, kwa kuwa hakuamini kuwa angeweza kupata eneo lingine kwa fedha hiyo.
Hivyo, Chacha aliamua kujenga nyumba na kuishi katika eneo hilo lililokuwa linabishaniwa fidia na kampuni iliendelea na shughuli za mgodi.
Mwaka 2013 Chacha na mkewe walifungua kesi ya madai dhidi ya meneja mkuu wa kampuni hiyo.