Dar/Mikoani. Saa 53 za mgomo wa wafanyabiashara ulioanza eneo la Kariakoo Dar es Salaam kabla ya kusambaa maeneo kadhaa nchini umeathiri mapato ya kada tofauti katika mnyororo wa biashara.
Mgomo huo ulioanza alfajiri ya Jumatatu Juni 24, eneo la Kariakoo, hadi jana ulisambaa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mbeya, Mwanza, Iringa, Dodoma, Arusha, Mtwara na Songwe.
Umeiathiri Serikali iliyokosa mapato kutokana na biashara. Kwa takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwaka 2023 wastani wa makusanyo ya mkoa wa kikodi Kariakoo ulikuwa Sh14.16 bilioni ambayo ni sawa Sh472 milioni kwa siku.
Siyo Serikali pekee, bali wafanyabiashara pia wamekosa mapato, makuli, watoa huduma mitandaoni, mama na baba lishe, wenye huduma za kifedha na wasafirishaji wa mizigo.
Makali ya mgomo eneo la Kariakoo yamepungua Juni 26, kuanzia saa 5.00 asubuhi baada ya kikao cha wafanyabiashara na viongozi wao.
Baada ya kikao hicho wengine walikwenda kufungua maduka, huku wengine hawakufanya hivyo.
Katika mkutano uliodumu kwa dakika 30, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana aliwapa mrejesho wa kikao kilichofanyika jijini Dodoma kilichowakutanisha viongozi wa wafanyabiashara na wale wa Serikali.
Kikao hicho kiliwaacha baadhi yao njiapanda baada ya Mbwana kuwaeleza hatawalazimisha kufungua maduka kwani uamuzi ni wao.
Kwa kauli hiyo, wapo walioendelea na biashara, huku wengine wakiahidi kufungua Juni 27. Mbali ya hayo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Juni 26, 2024 amekutana na kuzungumza na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.
Msemaji wa wasafirishaji wa mizigo kwa malori, James Haule amesema tangu mgomo ulipoanza upatikanaji wa mizigo umekuwa hafifu, hivyo ameshindwa kujaza lori kwa safari ya mkoani.
“Tangu Jumatatu tunakuja kupiga picha hapa, hakuna mizigo kwa sababu tunaowategemea watupe hela nao wamekwama huko sokoni, hawana kitu cha kusafirisha,” amesema Haule.
Msafirishaji mwingine, Jackson Samson amesema leo Juni 26 ni siku ya tatu hajaweza kufikisha mizigo nusu ya lori, hivyo kushindwa kuondoka.
Anaeleza kwa kawaida saa 10 hutosha kujaza gari na wakati mwingine mizigo hukosa nafasi.
Mwendesha toroli eneo la Kariakoo, Adam Ngoteji amesema mgomo umeawathiri kwa kiasi kikubwa kwani alikuwa anaingiza Sh20,000 kwa siku lakini kutokana na mgomo hajafanya kazi kwa siku mbili.
“Wengine tunategemea maduka haya kupata fedha, mteja anunue ubebe mzigo, lakini Jumatatu na Jumanne sijafanya kazi. Nina familia imebidi nitumie akiba niliyojiwekea kuacha nyumbani wale,” amesema Ngoteji.
Baadhi ya watoa huduma za kifedha Kariakoo pia wameeleza kuathiriwa na mgomo huo.
“Wateja wamepungua, tulipohitaji kutoa au kuweka pesa sisi mawakala wadogo ilibidi kwenda benki kwa sababu mawakala wakuu na wao wamefunga, hivyo hatukuweza kuingiza kipato kama tulivyozoea,” amesema Nusrat Yahaya, mtoa huduma za kifedha.
Dereva wa gari ndogo ya kubeba mizigo maarufu Kirikuu, Yohana Mazinde amesema mgomo umesababisha asimamishe huduma kwa kukosa wateja.
Amesema kwa kawaida wanunuzi wa bidhaa wanaosafirisha kwenda mikoani ndio huwabebea mizigo kuipeleka eneo la Jangwani ili kupakia kwenye malori.
“Tunategemea maduka kufanya kazi, hakuna kinachotoka wala kuingia ni ngumu kuingiza chochote. Tulioumia ni sisi watu wa kipato cha chini na siyo wafanyabiashara,” amesema Yohana.
Mwendesha guta, Ramadhan Salum amesema alikuwa na uwezo wa kuingiza hadi Sh50,000 kwa siku kwa kubeba mizigo kutoka Kariakoo kupeleka Jangwani lakini mgomo umesababisha aambulie Sh10,000 kwa siku.
Kwa upande wao, baba na mama lishe wamelazimika kupunguza kipimo cha chakula kutokana na wateja kupungua, huku wengine wakilazimika kurejea na chakula nyumbani siku ya kwanza ya mgomo.
“Jumatatu sikujua kama kuna mgomo nilikuja na chakula nilikaa hadi saa 10.00 jioni mwisho nikakibeba nyumbani, hasara hiyo,” amesema Hadija Nyinge.
Nao wauza mifuko wameeleza wamekuwa wakizunguka pasipo kuuza chochote kutokana na mgomo huo.
Dereva wa bajaji, Ali Thabiti amesema kufungwa maduka eneo la Manzese hadi TipTop kumesababisha wakose wateja kwa sababu hutegemea kuwarudisha nyumbani wachuuzi wanaofika kununua mahitaji.
Naye Salim Said, ambaye ni fundi wa mizani amesema kwa siku mbili za mgomo biashara yake imekuwa ngumu kwani baadhi ya wateja huenda kwake kutengeneza na kupima bidhaa.
Mgomo jijini Mbeya ulioanza jana Juni 25, 2024 umesababisha ongezeko la bei ya bidhaa.
Miongoni mwa bidhaa zilizopanda bei ni vifaa vya shule, huku wanafunzi wakitarajiwa kufungua Jumatatu Julai Mosi.
Ezra Mdamu, mkazi wa jijini Mbeya amesema wafanyabiashara wadogo wanatumia fursa ya mgomo kujinufaisha kwa kuongeza bei ya bidhaa.
Amesema daftari lililokuwa likiuzwa Sh500 linauzwa Sh700, huku soksi za Sh1,000 sasa zinauzwa Sh2,000.
Wafanyabiashara kutoka nchi jirani wanaotegemea kununua bidhaa kwa bei ya jumla kwenye maduka yaliyopo soko kuu la Halmashauri ya Mji wa Tunduma walijikuta njiapanda kutokana na kushindwa kununua bidhaa.
Mfanyabiashara kutoka nchini Zambia, Julita Nsamweya amesema amelazimika kutumia gharama kubwa kununua bidhaa kwa wafanyabiashara wadogo ambao bei zao si sawa na zile za maduka ya jumla.
“Tunategemea maduka ya Tunduma kujumua mizigo lakini leo imekuwa kero kwetu mzigo wa Sh1.2 milioni unauziwa Sh1.5 milioni ni hasara kubwa,” amesema.
Mgomo umeendelea licha ya Jumatatu, Juni 24, Waziri wa Uwekezaji na Mipango, Profesa Kitila Mkumbo kutangaza kusitisha kazi ya ukaguzi wa risiti za kielektroniki (EFD) na ritani za kodi iliyokuwa ikifanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kupitia Mkoa wa Kikodi Karikaoo.
Serikali imefikia hatua hiyo ikiandaa utaratibu mzuri wa utekelezaji wa suala hilo.
Profesa Mkumbo alisema katika kikao cha viongozi wa wafanyabiashara na Serikali kilichofanyika, wamekubaliana kuwapanga machinga ili kutoingilia ufanyaji biashara wa wenye maduka na kuhakikisha kila anayefanya biashara analipa kodi kama ilivyokubalika.
Kabla ya mgomo huo, kulisambazwa vipeperushi kwenye mitandao ya kijamii. Hata hivyo, viongozi wa wafanyabiashara walisema hawakuutangaza.
Wafanyabiashara wamekuwa wakilalamikia kukamatwa na maofisa wa TRA na pia faini ya Sh15 milioni kwa ambaye hatatoa risiti ya EFD.
Imeandikwa na Aurea Simtowe, Devotha Kihwelo, Tuzo Mapunda, Mintanga Hunda (Dar), Saddam Sadick (Mbeya), na Denis Sinkonde (Songwe)