Nairobi. Siku moja baada ya maandamano, machafuko na umwagaji damu nchini Kenya, Rais William Ruto alihutubia Taifa akitoa ujumbe ulioonyesha hasira na hisia kali kwa maandamano hayo.
Ruto aliyechaguliwa mwaka 2022 akiahidi kupunguza ufisadi, kuimarisha uchumi unaoyumba wa nchi na kusaidia maskini, sasa anakabiliwa na upinzani mkubwa ambao haujawahi kutokea dhidi ya muswada wa sheria ya fedha anaosema ni sehemu muhimu ya mpango wake wa kujenga Taifa.
Katika maandamano ya jana Juni 25, 2024 idadi kubwa ya vijana walivamia eneo la Bunge na kuchoma sehemu ya majengo yake.
Bado haijajulikana idadi rasmi ya watu waliouawa katika maandamano hayo, kwani wakati taarifa zikieleza kuwa watu waliofariki ni watano, Rais wa Chama cha Madaktari wa Kenya Simon Kigondu, amesema takribani watu 13 waliuawa katika maandamano hayo.
Akizungumza na Shirika la habari la AFP, ofisa mmoja wa Hospitali ya Taifa ya Kenyatta ya Nairobi amesema madaktari wanawatibu watu 160, baadhi yao wakiwa na majeraha madogo na wengine wakiwa na majeraha ya risasi.
Sababu ya machafuko hayo ni waandamanaji wengi wao wakiwa vijana wakijulikana kwa jina la ‘Gen Z’ wamekasirishwa na muswada mpya wa fedha ambao Rais Ruto anasema ni muhimu, ili kupunguza deni kubwa la Serikali.
Katika muswada huo wa fedha wa mwaka 2024, Serikali ya Kenya inakusudia kukusanya dola bilioni 2.5 (Sh323 bilioni) zaidi kupitia kodi zilizoboreshwa kuanzia mwaka wa fedha wa Julai.
Juni 25, maandamano hayo ya kitaifa chini humo yakiwa na kaulimbiu ‘Kataa Muswada wa Fedha 2024’ yaliendelea kwa siku ya tatu.
Maandamano hayo yalifanyika zaidi katika kaunti 25 nchini humo na baadhi ya waandamanaji kulivamia jingo la Bunge la nchi hiyo lililokuwa na ulinzi mkali.
Wakati Bunge likiwa limeshapitisha muswada huo, waandamanaji wanasema bado kuna muda wa kumzuia Rais kutia saini muswada huo kuwa sheria.
Waandamanaji hao wamesikika wakisema, “Hasira ni ya asili.”
Mmoja wa maelfu ya waandamanaji, Hanifa Farsafi ameiambia Al Jazeera kuwa, “Hakuna anayeliongoza hili, kila mtu anatoka nje kwa sababu tumechoka.
“Watu wamechoka, watu wana njaa, watu hawana kazi na Serikali inaendelea kutusukumia kodi za kikatili. Hakuna anayefadhili harakati hizi za maandamano. Huwezi kufadhili hasira kubwa kiasi hiki. Hasira ni ya asili.”
Akihutubia Taifa jana, Rais Ruto alisema maandamano hayo halali dhidi ya sera zake yametekwa nyara na kundi la wahalifu waliopangwa, akionya kuwa Serikali yake itatumia njia zote zinazopatikana kuzuia kurudiwa kwa vurugu, “kwa gharama yoyote ile.”
“Matukio ya leo (jana) yanaashiria hatua muhimu juu ya jinsi tunavyoshughulikia vitisho kwa amani yetu. Tutahakikisha hali kama hii haitarudiwa tena,” alisema.
Ujumbe wa Rais Ruto ulikuwa jaribio la kuchukua tena udhibiti baada ya siku za maandamano ya barabarani yaliyokuwa na idadi kubwa ya watu, huku yakikabiliwa na polisi waliowadhibiti na kusababisha watu watano kufariki na mamia kujeruhiwa.
Ili kuonyesha msisitizo wa kauli zake, wajeshi sasa wametumwa kukabiliana na waandamanaji ambao jana walivamia eneo la bunge, na kuwasha moto sehemu ya jengo hilo.
Licha ya kuonyesha ujasiri wa Serikali yake, bado baadhi ya watu wanaomzunguka Ruto wana hofu kwamba mambo yanaweza kuwa magumu katika utawala wake.
Tayari wito kutoka mataifa na jumuiya za kimataifa umetolewa kuhimiza utulivu.
Marekani na Umoja wa Afrika wamehimiza utulivu na mazungumzo kati ya pande zote, ili kufikia suluhisho.
Nacho Chama cha Waandishi wa Habari Afrika Mashariki (IPAEA) kimelaani kulengwa kwa waandishi wa habari katika maandamano hayo.
Kauli ya IPAEA imekuja wakati mwandishi wa kujitegemea, Collins Olunga akiwahamishwa hospitalini baada ya kugongwa na kopo la gesi ya machozi kwenye mkono wake wa kulia.
Kikundi hicho kilikuwa kinathibitisha ripoti nyingine za mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari.
“IPAEA inahimiza vyombo vya sheria vya Kenya kuwaachia waandishi wa habari wafanye kazi zao bila vurugu, unyanyasaji au kuingiliwa na kuheshimu haki ya uhuru wa kujieleza iliyoainishwa katika katiba ya Kenya,” chama hicho kilisema.
Daktari afariki kwa majeraha ya risasi
Vyombo vya habari vya ndani vimetangaza kuwa daktari alikuwa akijitolea kusaidia waandamanaji walioumia Jumanne amefariki kwa majeraha ya risasi.
Ripoti zinasema Margaret Oyuga, alipigwa risasi na maofisa wa polisi wakati wa maandamano na kuongeza kuwa alifariki dunia alipokuwa akiwahishwa hospitalini.
Akiizungumzia hotuba ya Ruto, Martin Mavenjina wa Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya amesema Serikali inajaribu kupunguza lawama za vurugu.
Amesema vurugu za mauaji “hazifikii viwango vinavyokubalika kimataifa vya utekelezaji wa sheria,” aliiambia Al Jazeera.
“Unaposikia Rais akisema kuwa maandamano haya ya amani yalitekwa nyara, ni mbinu tu ya Serikali kuelekeza mbali umakini kutoka kwao.
“Lakini tangu mwanzo vijana wengi Wakenya kote nchini wameandamana kupinga mapendekezo haya ya kikatili kutoka kwa Serikali,” amesema Mavenjina.
Kwa upande wake, Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amelaani ukandamizaji wa mauaji dhidi ya waandamanaji na ametoa wito wa kuondolewa kwa muswada wa fedha.
“Nimesikitishwa na mauaji, kukamatwa na kizuizini na upelelezi unaofanywa na polisi dhidi ya vijana wanaotaka kusikilizwa kuhusu sera za ushuru zinazowaibia sasa na siku zijazo.
“Kila maoni tofauti yamekataliwa na kudhihakiwa na maofisa wa Serikali na wanasiasa wa chama tawala na sauti hizo za upinzani sasa zinanyamazishwa kwa ukatili na mauaji,” amesema Odinga katika taarifa yake.
Teknolojia ilivyosaidia maandamano
Kwa mujibu wa mtandao wa Nation, utofauti wa maandamano hayo na mengine yaliyowahi kufanyika nchini huo, ni namna yalivyoratibiwa kwa njia ya mitandao ya kijamii, mpango uliowezesha maelfu ya waandamanaji kujumuika pamoja kwenye maandamano hayo.
Moja kati ya majukwaa ya kidijitali muhimu yaliyoratibu maandamano hayo ni ‘Zello’, programu ambayo huraisisha mawasiliano ya moja kwa moja, kushirikiana taarifa za maandamano na hata kuwasiliana na huduma za dharura.
Kila aliyetaka kujiunga na maandamano hayo alipaswa kupakua programu maalumu na baadaye kupewa kiungo muhimu ya kujiunga na kampeni hiyo ya kukaataa muswada wa sheria ya Fedha 2024.
Waringa Njehia, mtengenezaji wa maudhui mtandaoni aliisifu programu hiyo kwa kuwezesha waandamanaji kufahamu walipo polisi na maeneo hatarishi.
Njehia amesema, ‘Kwenye programu ya Zello, unachagua watu takribani watano kuwapa maagizo. Sauti zao lazima ziwe za kufahamika sana. Umakini wa Kizazi Z ni wa ajabu na mapinduzi haya yanategemea sana teknolojia.
Mwanaharakati mwingine, anayejulikana kwa jina la barabarani ItsMoran, anabainisha kuwa programu hiyo haiitaji mtu kuweka namba yake ya simu baada ya kujiandikisha.
Programu ya Zello tayari ina eneo la kukaataa muswada wa sheria ya fedha 2024 na hiyo ndio wanaandamanaji hutumia kuwakwepa polisi. Unaweza pia kutumia programu hiyo kuzungumza na familia yako.
Pia wapo wenye makundi sogozi ya WhatsApp zaidi ya 50 kwa ajili ya kujadili mabadiliko na kuratibu maeneo ya makutano kwenye maandamano hayo.
Zana nyingine inayotumiwa wakati wa maandamano ni programu ya Briar ambayo ina ujumbe ulioundwa kwa ajili ya wanaharakati.
Muandamanaji mwingine aliyejitambuliwa kwa jina la Phil ameiambia Daily Nation kuwa programu ya Briar ni moja ya programu bora licha ya kufanya kazi taratibu.
Imeandikwa kwa msaada wa Mashirika ya habari