Ruto asikia kilio cha Gen Z, aurudisha Muswada bungeni

Nairobi. Baada ya wiki mbili za maandamano na ghasia nchini Kenya, hatimaye Rais wa nchi hiyo, William Ruto ametangaza kuondoa Muswada wa Fedha wa mwaka 2024, akisema licha ya kuwa na nia njema, wananchi wameonyesha kuukataa.

Maandamano hayo yalishika kasi jana Jumanne Juni 25, 2024 baada ya waandamanaji kuvamia majengo ya bunge, dakika chache baada ya wabunge kupitisha ongezeko la kodi linalotafuta kuongeza dola 2.7 bilioni za ziada.

Katika maandamano ya jana Juni 25, 2024 idadi kubwa ya vijana walivamia eneo la Bunge na kuchoma sehemu ya majengo yake, muda mfupi baada ya wabunge kupitisha muswada huo.

Licha ya kutokuwepo kwa idadi kamili ya vifo, lakini inakadiriwa zaidi ya watu 20 wameuawa kwa kupigwa risasi huku wengine zaidi ya 160 wakilazwa hospitali kwa kujeruhiwa.

Waandamanaji hao waliapa kuendelea na maandamano yao leo Jumatano kama kilio chao hakitasikilizwa.

Akihutubia Taifa kupitia mtandao wa Youtube kutoka Ikulu ya Nairobi leo Jumatano Juni 26, 2024, Rais Ruto ametangaza kuuondoa muswada huo, akitaka wananchi watoe maoni zaidi ya jinsi ya kuiendesh nchi hiyo.
 

“Kutokana na hali hiyo na kufuatia majadiliano tuliyofanya na kusikiliza kwa makini kwa wananchi wa Kenya waliosema kwa sauti kwamba hawautaki muswada huu, ninaamua kuwa hiyo sitasaini muswada huu wa mwaka 2024 na utaondolewa,” amesema.

Amesema ametoa uamuzi huo kwa kukubaliana na wabunge walioupigia kura hivyo, “utakuwa ni uamuzi wa pamoja.”

“Kutokana na hilo, kunatakiwa kwetu kama Taifa kupiga hatua kutoka hapa na kusonga mbele. Hivyo napendekeza kuwepo na majadiliano kama Taifa kwenda mbele,” amesema.

Amewapongeza wabunge walioupigia kura ya ndio muswada huo, akisema ulilenga kutatua kero za wananchi na ulikuwa sahihi, akisema kuwa waliwashirikisha wananchi.

“Hata hivyo, yaliyotokea ni ushahidi kwamba wananchi wanataka tufanye marekebisho zaidi.

“Kwa kuwa ninaendesha Serikali na ninaongoza watu na watu wamesema, nawashukuru kwa wabaunge waliopigia kura muswada huo na baada ya kupitishwa kwa muswada huo, tumeshuhudia hisia tofauti kuonyesha kutoridhishwa na muswada, hali iliyosababisha kupoteza maisha ya watu, uharibifu wa mali.

“Kwa niaba ya wabunge hawa na mimi mwenyewe natoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao,” amesema.

Baada ya kuondolewa kwa muswada huo, Rais Ruto amewataka Wakenya kushirikiana na kujadiliana namna ya kuendesha nchi kwa pamoja.

“Tunaendeshaje mambo ya nchi pamoja, tunalipaje deni la Taifa kwa pamoja, tunawezaje kuendesha bajeti pamoja na kama nilivyoeleza Jumapili iliyopita, nitawahusisha vijana wa Taifa letu, kusikiliza maawazo yao, mapendekezo yao, mawazo yao, malalamiko yao ili kujua tunakwendaje mbele.

“Tunapendekeza wadau, sekta mbalimbali, kutoka saasi za kiraia, asasi za kidini na mashirika kuzungumza maendeleo ya nchi yetu,” amesema.

Pia, Rais Ruto ametangaza kubana matumizi kuanzia katika ofisi yake, mhimili wa utawala, Bunge na Mahakama.

“Ninaagiza kuchukuliwa kwa hatua ya upunguza matumizi ya Ofisi ya Rais na kuendelea kwa utawala wote kupunguza matumizi, usafiri, ukarimu, magari, matengenezo na matumizi mengineyo.

“Hiyo pia itakwenda kwa Bunge na Mahakama kuhakikisha kwamba tunapunguza matumizi na matumizi yaamuliwe na wananchi wa Kenya.

“Nimejadiliana na wadau wengi, kuhakikisha tunachukua Taifa lote kwenda kwenye maendeleo ya nchi yetu,” amesema. 

Malengo ya Muswada wa Fedha

Kuhusu bajeti ya mwaka 2024/25, amesema, Hazina walipendekeza Sh4.18 trilioni na kwamba muswada wa fedha wa 2024 ulilenga kuifanya bajeti kuwa shirikishi kwa wananchi kwa kupunguza kodi ya ongezeko la thamani.

Amesema katika muswada huo, awali walipanga kuweka kodi za Sh346 bilioni, lakini baada ya majadiliano bungeni, kodi zilipunguzwa hadi Sh200 bilioni.

“Nawashukuru wabunge waliosimama nyuma yangu na waliopiga kura ya ndiyo kwa muswada huo, kwa kujitambulisha vipaumbele vya Taifa letu kwa sababu nilipopeleka mapendekezo hayo bungeni na baraza la mawaziri tulikuwa na viupambele vya Taifa,” amesema.

Amesema muswada huo ulipanga kutenga Sh10 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa mbolea, Sh18 bilioni kwa ajili ya kuajiri walimu 46,000 wa shule za awali.

“Tunajua kwamba elimu ni suala muhimu na kwamba hakuna mwanafunzi anayetakiwa kwenda shule isiyo na mwalimu au walimu wa kutosha,” amesema.

Ameendelea kueleza kuwa, muswada huo pia ulitarajiwa kuajiriwa walimu 29,000.

“Tulikuwa pia tunalenga, kutokana na programu ya kuunganisha maeneo ya vijiji kwa barabara tulitenga Sh14.5 bilioni kwa kila jimbo kwa ajili ya kuungansiha.

“Kwa sababu tulijua kwamba kuna watu wanaweza kushindwa kwenda hospitali kwa kukosa fedha za matibabu, tulitenga Sh6 bilioni kuwezesha bima ya afya kwa wote na kuweka magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, kisukari, na kiharusi wapate matibabu.

“Tulipanga pia kutenga fedha kwa ajili ya wakulima wa kahawa, tulitenga pia fedha kwa wakulima wa miwa ili watoke kwenye madeni, tulipanga pia kwa wafugaji wa ngombe wa maziwa,” amesema.

Awali, Ruto alianza kwa kueleza hali ya uchumi aliyoikuta wakati anaingia madarakani mwaka 2022, akisema alirekebisha ikiwa pamoja na kupunguza deni la Serikali.

“Uchumi wetu umepitia changamoto kubwa ukifuatiwa na ongezeko la bei za bidhaa, bei ya juu ya mafuta, kushuka kwa sarafu wa Kenya na kukua kwa deni la Serikali kulikuwa kunatishia uchumi wa Kenya.

“Utawala wangu umefanya kazi kwa bidii, kwa hiyo leo bei za bidhaa muhimu kama unga umeshuka kutoka Sh240 kwa kilo mbili kwa Sh100, tumekuja na pembejeo kwa wakulima na mvua inayotolewa Mungu.

“Katika kipindi hicho tumepunguza bei ya mbolea kutoka Sh7, 500 hadi Sh2, 500, bei za petroli nazo zimeshuka kutoka Sh217 hadi Sh187 kwa lita. Shilingi imepanda kulinganisha dola ya Marekani kutoka 165 hadi asa Sh120,” amesema.

Kuhusu deni la Serikali amesema Serikali imelipunguza na kutengeneza fursa kwa ajili ya vijana.

“Umma unapaswa kujua kwamba, katika kila Sh700 tunazokusanya kama kodi tunatumia Sh61 kulipa deni la Serikali. Tumelipa deni la Kenya Eurobond iliyokopwa mwaka 2014 deni la Dola 2 bilioni lililokuwa limetufunga shingoni. Tumelipa Sh500 milioni wiki iliyopita.

“Leo mzigo wa deni la Kenya limeshuka na linahimilika na tumetoka kwenye mzigo na kulinga uhuru wetu,” amesema.

Ameendelea kusifia utendaji wa Serikali yake akisema hata pato la Taifa (GDP) limekuwa kwa asilimia 5.6 na kuifanya Kenya kuwa miononi mwa nchi 27 zenye uchumi unaokua kwa kasi duniani.

“Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 9 na 8 mwaka uliopita hadi asilimia 5 hadi Aprili mwaka huu,” amesema.

Imeandaliwa kwa msaada wa Mashirika ya Habari.

Related Posts