Sekondari ya wasichana Kyela kuleta tumaini jipya kwa wananchi

Mbeya. Wazazi na wananchi katika Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya wamesema hofu ya usalama kwa watoto wao wa wasichana waliokuwa wakifuata elimu maeneo ya mbali itatoweka baada ya kukamilika kwa ujenzi wa sekondari maalumu ya wasichana wilayani humo.

Shule hiyo ambayo ni ya mchepuo wa sayansi, imejengwa katika kijiji ya Busale wilayani humo ikigharimu Sh4.1 bilioni hadi kukamilika kwake na kuanzia mwezi ujao (Julai) itaanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano, huku wale wa kidato cha kwanza wataanza kupokelewa Januari, 2025.

Beatha Gibson, mkazi wa kijiji hicho, amesema kwa muda mrefu wamekuwa na kilio cha kupatikana kwa shule ya wasichana, hivyo ujenzi wa shule hiyo utarejesha matumaini kwao.

Amesema mara kadhaa wamekuwa wakisikia vitendo vya ukatili kwa wanafunzi wa kike, hali iliyokuwa ikiwapa wasiwasi, hivyo wanaishukuru Serikali kwa kukamilisha shule hiyo.

“Watoto wetu wanakumbana na changamoto nyingi huko nje, kipekee tunaishukuru Serikali kwa ujenzi w shule hii ambayo ipo jirani, watoto wetu watasoma karibu na usalama wao utakuwa mkubwa,” amesema Beatha.

Kwa upande wake, Charles Godwine amesema Serikali ijitahidi kuweka huduma muhimu na vifaa vya kutosha vya kufundishia shuleni hapo.

“Tunajua shule ni ya mchepuo wa sayansi, kimsingi tuone maabara na vifaa vyake, walimu wenye sifa, lakini waimarishe ulinzi, ili watoto wetu wasome katika mazingira mazuri,” amesema Godwine.

Akizungumza na Mwanachi kwa njia ya simu leo Juni 26, 2024, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Florah Angelo amesema pamoja na kuwapo shule hiyo, matarajio yao ni kuona Kyela inapiga hatua kiuchumi.

Amesema mpakas sasa, Sh3.1 bilioni zimetumika katika kukamilisha baadhi ya maeneo, ikiwamo madarasa manane, bweni, bwalo, jengo la utawala na maabara ambapo hadi kukamilika itagharimu Sh 4.1 bilioni.

“Kyela inakwenda kujulikana zaidi, hii ndio shule pekee maalumu mkoani hapa ya wasichana pekee, uchumi wa wananchi utapaa na tumejipanga kimkakati” amesema Florah.

Amesema kwa sasa shule hiyo inaweza kuchukua wanafunzi 600, lakini mpaka ikikamilika kanisa itachukua wanafunzi 1,000.

Related Posts