SIMBA inaendelea kusuka kikosi chake kimyakimya huku ikielezwa kwamba kati ya mastaa 12 wa kigeni waliomaliza na kikosi hicho msimu wa 2023-2024, ni nyota watatu tu wanaobaki kwa ajili ya msimu ujao.
“Je wanaokuja wataweza kweli!” Hilo ndilo swali unaloweza kujiuliza kuhusiana na timu hiyo kwa msimu ujao. Katika wachezaji hao watatu wa kigeni wanaobaki anaongezwa Aubrin Kramo ambaye alijiunga na timu hiyo msimu wa 2023-2024, lakini hakucheza mechi za mashindano kutokana na kuuguza majeraha ya muda mrefu, jina lake likawekwa kando. Kwa sasa amepona na anarudi kukiwasha.
Mbali na wachezaji wa kimataifa, pia Simba imepitisha fagio kwa wazawa ikianza na nahodha John Bocco, Kennedy Juma, Shaban Chilunda, huku Shomari Kapombe aliyekuwa akitajwa pia kwamba angeachwa akiongezewa mwaka mmoja. Wazawa wengine wanaodaiwa huenda wakaagwa ni Abdallah Hamis na Jimmson Mwanuke aliyepelekwa kwa mkopo Mtibwa Sugar.
Kitendo hicho kinadhihirisha kwamba Simba inajengwa na viongozi wamekubali kuanza upya kwani kati ya wale inaoachana nao wapo waliokuwa wakitengeneza kizazi cha dhahabu.
Simba ambayo ilimaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita, tayari imetangaza kuachana na wachezaji watatu wa kigeni ambao ni Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’, Luis Miquissone na Henock Inonga aliyeuzwa FAR Rabat ya Morocco.
Wengine wa kimataifa ambao wanatajwa kwamba muda wowote watapewa mkono wa kwaheri ni Clatous Chama aliyeitumikia timu hiyo kwa misimu minne na nusu. Mbali na Chama pia inaelezwa kuwa Sadio Kanoute, Willy Onana, Babacar Sarr, Pa Omar Jobe, Freddy Koubalan nao wataagwa kwa lengo la kupisha usajili mpya.
Wakati ikielezwa nyota hao wanaachwa mastaa wanaosalia ndani ya timu hiyo kwa upande wa wachezaji wa kigeni ni Kramo, Ayoub Lakred, Fabrice Ngoma na Che Malone Fondoh.
Mwanaspoti limethibitishiwa na mtu kutoka ndani ya Simba kwamba kiungo mkabaji, Kanoute, amemaliza mkataba na hajataka kubaki, hivyo timu hiyo ipo kwenye mchakato wa kumalizana na Augustine Okejepha anayekipiga Rivers United ya Nigeria kwa lengo la kuziba pengo lake.
“Kanoute ameshamaliza mkataba na sisi, na hayupo kwenye mipango yetu msimu ujao ndio maana unasikia tetesi nyingi za usajili wa kiungo mkabaji kutoka mataifa mbalimbali na huenda leo (jana Jumanne) au kesho (leo Jumatano) akawa miongoni mwa majina yatakayotangazwa kuachana na timu hii,” alisema.
Simba kuanzia 2017 ilianza kujengwa kwa ajili ya kufanya vizuri zaidi ndani na nje ya nchi ambapo ilifanikiwa kwa takribani misimu minne mfululizo.
Kikosi cha Simba kilitawala Ligi Kuu Bara na kubeba ubingwa mara nne mfululizo 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021 kabla ya watani zao wa jadi Yanga kujibu mapigo mara tatu kuanzia 2021-2022, 2022-2023 na 2023-2024.
Mbali na kufanya vizuri katika michuano ya ndani, Simba imetikisa Afrika kwa kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho mara tano katika misimu sita iliyopita. Upande wa Ligi ya Mabingwa ni 2018-2019, 2020-2021, 2022-2023 na 2023-2024 wakati Kombe la Shirikisho ikiwa 2021-2022.
Kwa wale waliocheza robo fainali hizo zote waliobaki ni Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Mzamiru Yassin na Aishi Manula ambao nao hawana muda mrefu sana watafikia ukomo.
Chama na Luis nao walikuwa sehemu ya mafanikio hayo Simba huku nyota hao wawili wakifunga mabao muhimu zaidi ikiwemo lile la Machi 16, 2019 Simba ilipofuzu robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga AS Vita mabao 2-1. Chama alifunga bao la ushindi dakika ya 90.
Pia Simba ilipozitesa timu vigogo Afrika zilipokuja Uwanja wa Benjamin Mkapa. Luis anakumbukwa zaidi kwa bao safi alilofunga Al Ahly kwenye Ligi ya Mabingwa katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mkapa na vijana hao wa Msimbazi wakaibuka na ushindi wa bao 1-0. Kuondoka kwao kunaacha mtihani kwa wanaokuja kurithi mikoba kama wataweza kuipa Simba katika mafanikio zaidi ya hayo kwani hivi sasa klabu hiyo malengo ni kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wakati majina hayo yakitajwa kukatwa ndani ya Simba, majina mapya yanayoingia ni pamoja na Joshua Mutale ambaye inaelezwa amesaini mkataba wa miaka miwili akimudu kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji. Mwingine ni kiungo mshambuliaji kutoka Mashujaa, Omary Abdallah Omary.
Pia yupo beki wa kati raia wa DR Congo, Nathan Idumba Fasika anayecheza Valerenga ya Norway kwa mkopo akitokea Cape Town City ya Afrika Kusini. Wapo pia Yusufu Kagoma, kiungo mkabaji kutoka Singida Fountain Gate na Lameck Lawi ambaye licha ya Simba kumtambulisha kuwa mchezaji wake Coastal Union usajili wake umeingia doa timu yake ikikanusha kumalizana na Mnyama.
Kipa wa zamani wa Simba, Steven Nemes amesema uamuzi wanaoufanya Simba ni sahihi kwa sababu timu waliyokuwa nayo misimu miwili mfululizo imeshindwa kuthibitisha ukubwa wa chapa hiyo huku akitaja kwamba walikuwa na wachezaji wengi ambao hawana uwezo wa kuichezea Simba.
“Simba huwezi kuifananisha na Yanga ambao wanafanya maboresho maeneo machache sana na wanaweza wasisajili msimu huu bado wakawa bora. Ukiangalia hata wao walipambana kwa misimu minne baadaye wakatulia na kuamua kufanya uamuzi mgumu ambao umewapa faida,” alisema.
“Wengi hawataweza kuielewa Simba kwa sasa, lakini baada ya miaka miwili au mmoja baadaye watakuwa bora na wataleta ushindani kwa timu zilizoimarika sasa Yanga na Azam FC.”
Katika hatua nyingine, wachezaji wa Simba wamedai kupigiwa simu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ akiwataka wote kufika Dar es Salaam ifikapo kesho.
Mwanaspoti lilizungumza na wachezaji zaidi ya watano wa klabu hiyo ambao wamepokea wito wa Mo Dewji kuwataka wawepo Dar.
“Tajiri ametupa taarifa ya kila mmoja kuwepo Dar es Salaam kwa tarehe aliyoitaja, kwani kuna vitu vingi vitatakiwa vifanyike kutokana na kambi ambayo tutakwenda kuweka nje,” alisema mmoja wa wachezaji hao anayecheza nafasi ya beki.
Wakati huohuo, inaelezwa kuwa kati ya wachezaji iliowasajili Simba, winga Joshua Mutale amekuwa wa kwanza kutua Dar kwa Air Tanzania akitokea kwao Zambia. Hivi karibuni, Mwanaspoti liliripoti juu ya Mutale kusajiliwa Simba kwa mkataba wa miaka miwili.