Vifaa tiba, dawa za Sh100 milioni zatua kambi ya matibabu kibingwa Arusha

Arusha. Serikali kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imetoa vifaa tiba na dawa zenye thamani ya Sh100 milioni kwa ajili ya kambi ya madaktari bingwa na wabobezi, inayoendelea jijini Arusha.

Aidha, kutokana na wingi wa wagonjwa waliojitokeza, madaktari na wataalamu wa afya 100 wanatarajiwa kuwasili jijini hapa kuungana na wengine 450 ambao wanaendelea kutoa huduma hiyo.

Hayo yameelezwa leo Jumatano, Juni 26, 2024, na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, wakati akipokea dawa hizo ambazo ilikuwa ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa siku ya kwanza ya kambi hiyo, Juni 24, 2024.

Amesema wamekubaliana kuongeza idadi ya madaktari, kuongeza dawa na kuweka uratibu mzuri kwa ajili ya wazee, watoto na wajawazito.

Siku ya uzinduzi wa kambi hiyo, akizungumza na wananchi wa Arusha kupitia simu ya Makonda, Rais Samia aliahidi kusaidia kambi hiyo katika mahitaji.

Leo ikiwa ni siku ya tatu, gari la MSD liliwasili viwanjani hapo kutoa dawa hizo na Makonda amesema kutokana na wingi wa watu na mwitikio mkubwa, dawa hizo zitawasaidia wanaohitaji matibabu.

“Kwa lugha nyepesi ni kwamba ule msemo wa kila atakayefika hapa akipimwa ugonjwa utakaobainika atapata dawa, sasa ndiyo hizi dawa zinakuja ikiwa ni sehemu ya kutimiza ahadi ya Rais aliyosema atatushika mkono,” amesema RC Makonda.

Amewaomba wananchi waendelee kuwa wavumilivu kwa kuwa safari ya ya matibabu si nyepesi.

“Kwenye matibabu yoyote yale ni eneo muhimu sana la kuwa mtulivu, kwani linahitaji utaalamu unaomtegemea Mungu. Tukifanya haraka kwenye tiba tunaweza kupewa dawa ambazo si za ugonjwa tulionao, tunaweza kupimwa kipimo cha ugonjwa ambacho siyo ugonjwa unaotusumbua na mwishowe tukapata madhara badala ya kupona,” amesema Makonda.

Amesema mpaka leo, wagonjwa 6,434 wamehudumiwa na siku ya kwanza ya kambi hiyo juzi walihudumiwa wagonjwa 2,034, jana wagonjwa 4,400 na leo wanaamini idadi hiyo itavuka.

Amesema madaktari na wataalamu wa afya 100 wataungana na wenzao 450 wanaoendelea kutoa huduma hiyo uwanjani hapo.

“Hapa nimeshaongea na RMO, tunatafuta mabanda na madaktari wengine, ili tuongeze kasi ya kuwahudumia. Hatutaki hata mmoja akose hii huduma. Kipekee tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kuna gari linakuja lina dawa za thamani ya Sh100 milioni kupitia Mamlaka ya Dawa (MSD).

“Tumepata vijana wanaotoka Marekani wanaosoma udaktari na uuguzi zaidi ya 20, tunaongeza nguvu, ili muhudumiwe kwa haraka zaidi,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Peter Kisenge amesema asilimia zaidi ya 40 ya wagonjwa waliotibiwa katika kambi hiyo wamebainika kuwa na tatizo la kupanuka misuli ya moyo na moyo kushindwa kufanya kazi.

Aidha, asilimia 35 ya wagonjwa waliofanyiwa vipimo uwanjani hapo wamepewa rufaa na wanaandaliwa utaratibu wa kupelekwa JKCI jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata huduma zaidi. Amesema kati ya wagonjwa 200 waliowahudumia Jumatatu ya wiki hii, asilimia 35 wamepewa rufaa hiyo na wanatarajiwa kwenda kufanyiwa vipimo na matibabu JKCI.

“Wananchi wengi wanakabiliwa na changamoto ya mishipa ya damu kupanuka kutokana na shinikizo la juu la damu, shida ya umeme wa moyo pamoja na changamoto ya moyo kutokufanya kazi kwa ufanisi,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba na Mifupa ya Muhimbili (MOI), Dk Lemery Mchome, amesema mpaka sasa wagonjwa 650 wa mifupa wamepatiwa matibabu.

Related Posts