Morogoro. Jumla ya waelimishaji 20 wa ujasiriamali kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), wamepewa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wa kufundisha wajasiriamali nchini.
Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha wajasiriamali hao kuzalisha bidhaa zenye ubora ili kuziwezesha kuingia kwenye ushindani wa soko ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Juni 25, 2024 na Meneja Utafiti na Mafunzo kutoka TBS, Hamis Sindi.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwafundisha wawakilishi hao ili wakawe walimu wa wajasiriamali.
“Mafunzo haya yamefadhiliwa na Jumuiya ya watu wa Ulaya kupitia (Unido), wafaidika wa mradi huu ni pamoja na TBS na Sido, kila upande umeleta watu ambao wanafundishwa ili wakafundishe wajasiriamali Tanzania nzima,” amesema Sindi.
Amesema kupitia mafunzo hayo washiriki watapitia vitini vya mafunzo vilivyoandaliwa.
Sindi amesema wajasiriamali wametambuliwa kama washiriki wakuu kwenye ujenzi wa uchumi wa nchi, hivyo kuna ulazima wa kuwapatia mafunzo kusudi bidhaa zao zinazozalishwa ziwe na ubora na zitakubalika kwenye masoko ya ndani na nje nchi.
“Kwa hiyo upande wa Sido, hawa ndio walezi wakubwa wa wajasiriamali tunataka ifike wakati wanapokuja kuchukua nembo za ubora bidhaa zao nazo zikidhi ubora unaotakiwa,” amesema Sindi.
Amesema mjasiriamali anapoanza biashara yoyote, kuna mambo ya msingi ya kitaalamu anayopaswa kuyazingatia hasa kwa zile za usindikaji.
“Lakini pia katika kilimo lazima mkulima afahamu na kuzingatia kanuni bora za kilimo, haya ni matakwa ya muhimu kuyajua ili wanapozalisha wazalishe vitu vyenye ubora na kukidhi matakwa ya viwango vinavyohusika,” amesema Sindi.
Naye Steven Bondo, Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo na Usimamizi kutoka Sido, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wajasiriamali kupata alama ya viwango.
“Lakini wakati wa makubaliano tumepata changamoto nyingi ambazo wajasiriamali hukumbana nazo hivyo tunalazimika kwapeleka TBS kujifunza zaidi,” amesema Bondo.
Amesema wamebaini wajasiriamali wengi hawana elimu ya namna gani viwango vinatakiwa viwekwe bidhaa zao.
“Hivyo ujio wa mafunzo haya utawawezesha kupata uelewa na kuwarahisishia namna ya kujiunga na TBS,” amesema.
Bondo amesema wajasiriamali wengi hawafahamu namna ya kujiunga na TBS, “lakini kwa mafunzo haya ambayo pia yamefadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), yatasaidia kuhakikisha wanajiunga kwa wingi na TBS.”
Kwa upande wake, Stefano Sedola, Mshauri Mkuu Mradi wa QUALITAN unaotekelezwa na UNIDO kwa kishirikiana na TBS kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya amesema wanajisikia fahari kuona wajasiriamali Watanzania wanajua namna ya kutengeneza bidhaa zenye ubora unaotakiwa sokoni.
“Mradi huu ambao tunaudhamini pia, unalenga kuisaidia Tanzania kufikia maendeleo ya kweli kupitia bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wake.
“Tunaamini mradi huu ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania kwa kuwa tunaangazia kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa zinabaki kuwa bora kwa lengo la kupata soko ndani na nje ya nchi,” amesema Bondo.
Hata hivyo, Bondo amesema changamoto waliyonayo sasa ni ya namna ya kuwafikia wajasiriamali wadogo ambao wanazalisha bidhaa zao na zinahitaji kuongezewa ubora.
“Ndiyo maana tumeona tuwafundishe watu kutoka TBS na Sido kwa sababu wao ni rahisi kuwafikia wajasiriamali ambao sio rahisi sisi kuwafikia,” amesema.
Anasema wanaamini elimu ikiwafikia wazalishaji wote wa bidhaa nchini, lengo la Tanzania kuwa na uchumi mkubwa, litafikiwa pia.