Wakunga wa jadi washtukiwa ukeketaji wa watoto wachanga

Tarime. Baadhi ya wakunga wa jadi wilayani Tarime Mkoa wa Mara, wanadaiwa kuanza kujihusisha na vitendo vya ukeketaji wa watoto wachanga baada ya kuwazalisha wajawazito wanaokwenda kujifungulia kwao.

Wakunga hao wanadaiwa kukeketa watoto wachanga baada ya baadhi ya mangariba kuacha kufanya shughuli hizo kutokana na kampeni mbalimbali zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa mapambano dhidi ya ukeketaji wilayani humo.

Hayo yamesema na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Maulidi Surumbu leo Jumatano Juni 26, 2024  alipokuwa akitoa taarifa kwa mkuu wa mkoa wa Mara aliyefanya ziara ya kukagua maendeleo  ya mradi wa ujenzi wa kituo jumuishi cha huduma kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wilayani humo.

“Utafiti umefanywa na mashirika na wadau wa kupinga ukeketaji, imebainika mangariba baada ya kubanwa sana na Serikali kwa kushirikiana na wadau wamebadili mbinu na sasa wanawatumia wakunga wa jadi kutimiza malengo yao,” amesema Surumbu.

Amesema kutokana na hali hiyo, ameiagiza idara ya afya wilayani humo uhakikisha wakunga wa jadi wanaotoa huduma ya kuzalisha wajawazito wanafanya shughuli zao kwa kufuata taratibu za kitabibu wakati wakitoa huduma.

Amesema ili kukomesha vitendo hivyo, mkunga wa jadi atakayebainika kukeketa watoto wachanga atachukulia hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.

Amesema utafiti pia umebaini ukeketeji hivi sasa unafaywa kwa watoto chini ya miaka mitano, tofauti na awali ambapo vitendo hivyo vilikuwa vikifanywa kwa mabinti wenye umri wa miaka 12 na kuendelea.

“Kwa sababu sasa hivi ukeketaji sio ule wa jamii nzima bali unafanyika kati ya familia na familia, sisi tumeligundua hilo hivyo jitihada zetu na sisi tunazielekeza huko huko kwenye ngazi ya  familia,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amemuagiza mkuu huyo wa wilaya pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kufanya msako na kuwakamata watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ukatili kwa watoto, ikiwemo ukeketaji.

Pia amewataka wakazi wa Wilaya ya Tarime na Mkoa wa Mara kwa ujumla kuachana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwa maelezo kuwa mbali na kuwa ni aibu,  pia vinarudisha nyuma maendeleo katika jamii.

Amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh189 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho katika hospitali ya halmashauri ya Nyamwaga, fedha ambazo anamaanini zingeweza kutumika kuleta maendeleo endelevu endapo kusingekuwa na vitendo hivyo vya ukatili.

Ofisa ustawi wa Jamii Hospitali ya Nyamwaga, Adeodatha Joseph amesema ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 95 na kwamba utakapokamilika kituo hicho kitawaondolea adha wanayokutana nayo waathirika wa vitendo hivyo ambao  sasa wanatumia muda mrefu  kupata huduma hasa za matibabu, kwani wanalazimika kwenda maeneo  tofauti, ikiwemo polisi kabla ya kufika hospitalini kwa matibabu.

Kuhusu hali ya ukatili kwa watoto, amesema wastani wa watoto watano wanafikishwa hospitalini hapo kila wiki wakiwa wamefanyiwa vitendo vya ukatili, ukiwepo ukatili wa kingono na vipigo.

Mkunga kutoka katika Kijiji cha Manga, Peres Mtatiro ametoa rai kwa mamlaka husika kufanya uchunguzi na kuwawajibisha wale wote watakabianika kujihusisha na vitendo hivyo.

Related Posts