Dodoma. Serikali imetangaza habari njema kwa wastaafu waliostaafu kuanzia Julai mwaka 2022, ambao ni 17,068 kuwa watalipwa mapunjo yao ya mafao ya mkupuo kulingana na kikotoo kilichotangazwa Juni 13, 2024.
Kiasi cha mafao ya mkupuo kiliongezwa kutoka asilimia 33 hadi 40 kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na 33 watapata asilimia 35 kwa wale wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Hayo yamesemwa leo Juni 26, 2024 na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Deogratius Ndejembi wakati akijibu hoja zilizotolewa na wabunge wakati wa mjadala wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25.
“Suala la kikotoo linaonyesha ni namna gani Rais wetu (Rais Samia Suluhu Hassan), anawajali wafanyakazi wake. Julai 2022 kuna mabadiliko yawekwa kuhusu kikokotoo, ambapo watumishi wa umma walitoka kulipwa asilimia 50 wakaenda 33 na wale waliokuwa asilimia 25 walipanda kwenda asilimia 33,”amesema.
Amesema jambo hilo lilikuwa ni kilio kikubwa kwa wafanyakazi ambao mishahara yao ya chini na wengine husubiria mkupuo wa fedha hizi kuanza maisha yao pale wanapoona kuwa wamestaafu.
Amesema Rais Samia kama alivyosikia kilio cha madaraja, kilio cha madeni na aliagiza kikotoo kiweze kuangaliwa na kwamba baada ya Waziri wa Fedha kukaa na ofisi yake waliangalia namna nzuri zaidi ya kutatua changamoto hiyo kwa kutenga Sh155 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/25.
Amesema fedha hizo zinakwenda kutumika katika kunyanyua kiwango cha mikopo kutoka asilimia 33 hadi 40 kabla ya Julai 2022 na kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35.
Amesema wamesikia kilio cha wabunge na vyama vya wafanya kunyanyua kiwango hicho kwenda pale kilipokuwa lakini kadri ya utengamavu wa mifuko ya jamii inavyoendelea na kila uhimilifu unavyofanyika Serikali itaendelea kuangalia ni namna gani inarejea katika asilimia 50.
“Hao wanaokwenda kulipwa si wale wanaokwenda kustaafu Julai mwaka 2024, wanakwenda kulipwa wote hata wale waliostaafu Julai 2022,”amesema.
Amesema wastaafu 17,068 waliostaafu kuanzia Julai 2022, wanakwenda kulipwa mapunjo yao ya asilimia saba na wale waliokuwa wakipata asilimia 33 watalipwa mapunjo yao ya asilimia mbili.
Ndejembi amesema wanatarajia kuona wengi wakienda kudai mapunjo ya mafao yao ya mkupuo.
Baada ya maelezo hayo, Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amesema kwa kuwa hao waliopunjwa wanafahamika, Serikali iwalipe bila kusubiri waende kudai.
“Nafikiri hiyo ni lugha tu ya mazungumzo lakini walipeni tu lasivyo maombi yatakuwa ni mengi sana,”amesema.
Uamuzi wa kupandisha kikotoo baada ya kelele za wabunge na vyama vya wafanyakazi, ulitangazwa na Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2024/25, Juni 13,2024.
Katika uamuzi huo alisema wastaafu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), waliokuwa wanapata mafao ya mkupuo asilimia 33 watapata asilimia 40 na wale wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wataongezewa kutoka asilimia 33 hadi 35.