WAZIRI GWAJIMA ATOA WITO VIONGOZI,WAJUMBE WA NaCoNGO KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA UADILIFU

WAZIRI  wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima,akizungumza wakati akizindua Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya  Kiserikali (NaCoNGO) lililozinduliwa leo Juni 26,2024 jijini Dodoma.

WAZIRI  wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima,akifafanua jambo wakati akizindua Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya  Kiserikali (NaCoNGO) lililozinduliwa leo Juni 26,2024 jijini Dodoma.

WAZIRI  wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzindua  Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya  Kiserikali (NaCoNGO) lililozinduliwa leo Juni 26,2024 jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI  wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima,ametoa wito kwa Viongozi na Wajumbe wote wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya  Kiserikali (NaCoNGO) kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na  uzalendo wa hali ya juu.

Waziri Gwajima ametoa wito huo leo Juni 26,2024  wakati akizindua Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya  Kiserikali (NaCoNGO) jijini Dodoma.

Waziri Gwajima amewapongeza Viongozi wote 30 wa Baraza hilo waliochaguliwa kwa kuaminiwa na Wajumbe katika Wilaya na Mikoa yote ya Tanzania Bara na Makundi  Maalum.

“Sasa mmechaguliwa na kuaminiwa nendeni mkafanye kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo ili kukidhi  matarajio ya waliowachagua na jamii ya Watanzania kwa ujumla.”amesema Waziri Gwajima

Viongozi hao waliochagulia ni  Ndugu Japser Lazaro Makala Mwenyekiti wa Baraza, Ndugu Adamson Richard Nsimba – Katibu Mkuu  wa Baraza, Ndugu Prisca Matiwili – Mweka Hazina wa Baraza, Mwenyeviti wa Kamati  mbalimbali, pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. 

“Nimepokea kwa mikono miwili taarifa  ya Kamati ya Mpito. Katika taarifa hiyo, nimesikia mapendekezo ya Kamati ambayo  mengine utekelezaji wake unahitaji kujitoa kwenu kwa hali na mali, lakini mengine ni ya  kwetu upande wa Wizara.”amesema

Aidha amesema kuwa Masuala ya uwakilishi wa kikanda, upatikanaji wa rasilimali  fedha na mapitio ya Kanuni za Uchaguzi wa Baraza, ni masuala ambayo mnaweza  kuyajadili kupitia mifumo yenu ya ndani na kuchukua hatua, lakini kwa kuzingatia sheria,  kanuni na miongozo inayoratibu shughuli za Baraza. 

Waziri Gwajima amesema kuwa  tayari walishaanza  mchakato wa kutoa mafunzo kwa Wasajili Wasadizi na zoezi hilo ni  endelevu. 

Aidha, kuhusu kuwajengea uwezo Wajumbe wapya wa Baraza, amewahakikishia kuwa suala hilo lipo ndani ya uwezo wao na milango ya Wizara iko wazi  wakati wowote.

Hata hivyo ameishukuru  Kamati ya Mpito kwa kuratibu Uchaguzi huo kwa weledi, viongozi na Wajumbe wote wa  Baraza kwa kuaminiwa na kuchaguliwa kuliongoza Baraza kwa kipindi cha miaka mitatu . Naomba mfanyia kazi marekebisho ya Kanuni za Uendeshaji na Uchaguzi wa Baraza.

“Nendeni mkatekeleza agizo la Serikali la kuzifanyia marekebisho kanuni za uendeshaji na uchaguzi  ili uchaguzi ujao usimamiwe na mifumo ya NaCoNGO badala ya kuendeshwa chini ya bodi ya uratibu wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali”amesisitiza

Kwa upande wake Msajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’S) Bi.Vickness Mayao,ametoa wito kwa NaCoNGO kutumia nafasi yao kuishauri Serikali kwenye masuala ambayo wanaona kwamba yanajenga kwani mashirika yasiyo ya Kiserikali yanafanya kazi katika Sekta zote.

“Wao wakiweza kujiratibu wenyewe na kuangalia mapungufu yaliyopo na kuishauri Serikali vizuri kuhusiana na changamoto mbalimbali ambazo inapaswa kuzichukua na kuzifanyia kazi”,amesema Mayao

Naye Mwenyekiti Mpya wa NaCoNGO Bw.Japser Lazaro Makala,amesema wamejipanga kuanza kazi mara baada ya Baraza kuzinduliwa ambapo watakuwa na vikao vya kujadili namna ambavyo watajipanga kufanya kazi ikiwemo kuandaa mpango kazi mzuri.

“Kwasababu sisi ni baraza la Taifa pia tupo huru tutaishauri Serikali tuweze kutengeneza kikosi kazi ambapo kitakuwa kinaratibu zoezi zima la kupata kanuni mpya za Baraza la mashirika yasiyo ya Kiserikali “,amesema Bw.Makala

Related Posts