KUNA kifaa kipya kinashushwa na Yanga leo Jumatano kutoka nchini Uganda kwa ajili ya mchakato wa kujiunga na timu hiyo msimu ujao. Huyu si mwingine bali ni Hassan Ssenyonjo.
Uamuzi huo ni katika kuimarisha kikosi cha mabingwa wa Ligi Kuu Bara ambao wamepanga kuanza kukutana Julai Mosi, mwaka huu kwa ajili ya kuanza kambi.
Kifaa kinachokuja kinatoka katika kikosi cha Wakiso Giants, Uganda ambapo ujio wake ni pendekezo la kiungo mkabaji wa Yanga, Khalid Aucho ambaye pia ni Mganda.
Ipo hivi; Yanga inapambana kusaka mchezaji wa kusaidiana na Aucho eneo la kiungo kama Kocha Miguel Gamondi alivyosisitiza hivyo leo watakuwa na ugeni wa kiungo huyo anayetajwa kutazamwa kwenye mchezo wa kirafiki utakaochezwa Jumamosi, wiki hii.
Kiungo huyo anatarajiwa kutua jioni kwa ndege ya Uganda kisha ataungana na mastaa wengine wa Yanga kwa ajili ya mchezo huo wa kirafiki utakaopigwa Jumamosi usiku kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Yanga kabla ya kutua kwa kiungo huyo ilifanya mazungumzo na kiungo wa Singida Fountain Gate, Yusufu Kagoma ambaye tayari amemalizana na Simba kwa mkataba wa miaka miwili.
Hivyo ujio wa Ssenyonjo huenda likawa chaguo sahihi na mchezaji huyo akabaki baada ya mchezo huo kwa ajili ya kusaini mkataba kwani ana uwezo wa kukaba na kuanzisha mashambulizi kwa wakati mmoja kitu ambacho Gamondi anakihitaji kutoka kwa kiungo ajaye.
Licha ya ujio wa kiungo huyo, Yanga tayari eneo la kiungo cha kati ina Jonas Mkude na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ ambao wamekuwa wakicheza mara chache mbele ya Aucho aliyejihakikishia namba kikosi cha kwanza chini ya makocha ndani ya timu hiyo na kuipa mafanikio. Wengine ni Mudathir Yahya na Jonas Mkude.
Inaelezwa kwamba, Yanga kuna wachezaji saba wa kimataifa wanaokwenda nao msimu ujao na waliokuwepo uliopita ambao ni Djigui Diarra, Yao Attohoula, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Stephen Aziz Ki, Pacome Zouzoua na Kennedy Musonda. Wanaodaiwa kuwa wataondoka ni Joyce Lomalisa, Gift Fred, Skudu Makudubela, Augustine Okrah na Joseph Guede. Warithi wao wanatajwa kuwa ni Chadrack Boka, Prince Dube, Clatous Chama na Hassan Ssenyonjo.