Baadhi wafunga, wengine wafungua maduka Kariakoo

Dar es Salaam. Unaweza kusema kauli ya Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo jijini Dar es Salaam, Martin Mbwana ya kuacha uamuzi wa kufunga au kufungua maduka katika eneo hilo imetekelezwa kwa vitendo.

Hiyo ni baada ya baadhi ya wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao kama kawaida huku wengine wakiendelea kufunga. Ni mgomo ulioanza Jumatatu ya Juni 24, 2024.

Gari la matangazo lilionekana likipita mitaa tofauti ya Kariakoo leo kuhamasisha watu kufungua maduka yao, huku msisitizo ukiwekwa kuwa kero mbalimbali zinaendelea kufanyiwa kazi kama ilivyoelezwa na viongozi wa wafanyabiashara.

Mtaa wa Aggrey na Nyamwezi maduka wafanyabiashara wameendelea kufunga maduka yao.

Hili linafanyika ikiwa ni mwendelezo wa kuishinikiza Serikali kutatua kero zao ikiwemo utitiri wa kodi wanaolalamikia jambo ambalo lilifanya kuwapo kwa mgogo katika eneo la Kariakoo kabla ya wafanyabiashara wa mikoa Mwanza, Mbeya, Iringa, Arusha, Ruvuma, Mwanza, Songwe na Morogoro kuunga mkono mgomo huo.

Mwananchi Digital imefika katika eneo la Karikoo na kukuta biashara zikiendelea kama kawaida katika baadhi ya maeneo huku sehemu nyingine maduka yakiwa yamefungwa na hakuna watu wanaopita.

Akizungumza mmoja wa wafanyabiashara waliokutwa wamefungua duka, Naiman Msangi amesema hakuna kitu kilichofanyiwa kazi ila ada za watoto ndiyo zimefanya wafungue.

Akiwa anauza vitenge, katika Mtaa wa Nyamwezi na Raha ambapo maduka mengi yalikuwa bado yamefungwa huku pekee akiwa yuko wazi.

“Jumatatu watoto wanakwenda shuleni, ada hakuna, tumefungua si kwa sababu mambo yote yamekaa sawa, hapana ila shida ndiyo zimetusukuma,” amesema Naiman.

Richard Mwema ambaye ni mfanyabiashara Mtaa wa Congo amesema ameamua kufungua duka wakati akiendelea kufuatilia maboresho yaliyoahidiwa kufanyika bandarini hasa katika ukadiriaji wa kodi ya forodha.

“Si walisema tuwape muda tumewapa muda, tunaangalia mambo yakiwa bado hayako vizuri tutakuwa na nafasi nyingine ya kupaza sauti zetu,” amesema Mwema.

Kufunguliwa kwa baadhi ya maduka katika eneo hili imekuwa ni ahueni kwa wachuuzi wa mikoani na kutoka nchi jirani kwani baadhi wameweza kupata mzigo waliokuwa wakiutafuta.

“Nilipopita hapa na kukuta maduka baadhi yamefunguliwa sikutaka kuhangaika kutafuta tena sijui bei rahisi, nimenunua tu mzigo japo inaweza kuwa si kwa bei niliyotarajia ila kuendelea kukaa hapa ni gharama zaidi,” amesema Charles Mwakalinga, mkazi wa Mbeya.

Mgomo huo umemfanya Mwakalinga kutumia siku mbili zaidi ya ilivyokuwa matarajio yake jambo ambalo analiita kama hasara kutokana na kupoteza muda ambao angeweza kuutumia kufanya biashara fedha zilizoongezeka katika malazi.

Wakati baadhi wakiendelea na biashara, wengine wamefunga maduka yao huku kilio kikiwa ni kilekile.

“Tuliyoyataka hayajafanyiwa kazi, acha tuendelee kufunga kwa sababu mitaji ni yetu, hatuna hasara tunayopata kwa sababu nguo haziharibiki hasara ipo kwao wanaokusanya kodi,” amesema mmoja wa wafanyabiashara Kariakoo.

Woga na kusikiliziana nayo ni moja ya kitu kinachofanya baadhi washindwe kufungua maduka yao hasa katika maeneo ambayo wengi hawajafungua.

“Mimi sijui watu wanaogopa nini, kuna mzee hapo alikuwa amefungua sasa hivi amefunga tena, ukiuliza anaogopa kupigwa, wewe umesikia nani kapigwa tangu mgomo uanze halipo hilo suala,” amesema mmoja wa wafanybiashara.

Hatahivyo, Jeshi la Polisi limeendelea kuimarisha ulinzi katika eneo la Kariakoo ambapo askari walikuwa wakipita huku na kule kuhakikisha hakuna mtu anapata tatizo kwa namna yoyote ile.

Haya yanajiri ikiwa ni siku moja tangu mwenyekiti wa wafanyabiashara eneo la Kariakoo kuwataka kurudi katika shughuli zao za kila siku huku akiweka bayana kuwa hatowalazimisha.

Mbwana aliyasema hayo jana Jumatano wakati akiwapatia mrejesho wa kile kilichojadiliwa katika mkutano baina ya viongozi wa wafanyabiashara na wale wa Serikali uliofanyika jijini Dodoma.

Katika mkutano huo, Mbwana alisema nguvu ya kuwalazimisha kufungua maduka kwani mfanyabishara anapoamua kufunga duka lake na kukaa pembeni inamaanisha kuwa amevurugwa na kukata tamaa kwani anategemea duka lake na kuendesha maisha yake hivyo ni vyema nguvu kutotumika na badala yake kukaa mezani ndiyo suluhisho.

Hata hivyo, amesema ikiwa wafanyabiashara hao wakifungua maduka watakuwa wamemuonyesha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa walikuwa na shida hiyo na endapo wataendelea kufanya hivyo pia ni hiyari kwani ni dhamana yao.

“Siwalazimishi mkiridhia kufungua maduka sina tatizo na mkifungua mtakuwa mmeniheshimisha mwenyekiti na kuonyesha mnaimani na mimi,” amesema Mbwana.

Hata hivyo amesema kama wataamua kuendelea na msimamo wa kufunga maduka yao hana tatizo kwenye hilo huku akiwaomba wanapozungumza na Serikali wawe na weledi, hekima na busara kwani ni taasisi si ya mtu mmoja.

Related Posts