Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amezikaribisha juhudi za Rais William Ruto wa Kenya za kutuliza ghasia zilizosababisha vifo na uharibifu wa mali lakini akahimiza kujiuzuia na kufanyika uchunguzi kuhusu madai ya unyanyasaji. Katika mazungumzo, Blinken amemshukuru Ruto kwa kuchukua hatua za kutuliza mivutano na kuahidi kufanya mazungumzi na waandamanaji na asasi za kiraia.
Ruto amesema Jumatano jioni kuwa anaondoa kabisa mswada wa fedha unaopendekeza nyongeza mpya za kodi ambao ulisababisha maandamano makubwa yalisosababisha vifo vya zaidi ya watu 20, na waandamanaji kulivamia bunge. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Mathew Miller amesema Blinken amesisitiza umuhimu wa vikosi vya usalama kujiuzuia na kujiepusha na vurugu. Aidha ametangaza uungwaji mkono wa Marekani wakati Wakenya wakizishughulikia changamoto zao za kiuchumi. Kenya ni mshirika muhimu wa Marekani barani Afrika.
Vijana nchini Kenya wanadai kuwa nyongeza mpya za ushuru zilizoainishwa kwenye mswaada wa fedha wa mwaka 2024 zitawaongezea mzigo.
Soma pia: Waandamanaji Kenya waapa kurudi tena barabarani
Rais Ruto ametangaza hatua za kubana matumizi ili kuweza kumudu mahitaji ya serikali na taifa kwa jumla. Ruto aliyebadili kauli na kuwa mpole, alitoa pia rambirambi kwa jamaa za waandamanaji waliopoteza maisha kwenye purukushani za hapo jana.
Kiongozi wa taifa alisisitiza kuwa bado azma ya kufanya majadiliano na vijana iko palepale kwani anajali maslahi yao.
Gachagua ailaumu idara ya ujasusi
Naibu rais wa Kenya Rigathi Gachagua amemtolea wito mkuu wa intelijensia nchini mwake Nurdin Haji ajiuzulu na awajibishwe kutokana na maafa yaliyotokea nchini Kenya yaliyofungamana na maandamano ya kupinga muswada wa fedha wa mwaka 2024.
Kulingana na Gachagua idara ya ujasusi nchini Kenya haikumpa rais ushauri muafaka kwamba Wakenya hawakuutaka mswada huo wa fedha.
Katika hotuba yake aliyoitoa moja kwa moja kupitia Televisheni ya kitaifa, naibu rais huyo wa Kenya amesema vifo vya raia, uharibifu wa mali na hata uvamizi wa taasisi muhimu za serikali vingeepukika iwapo rais angelipata ushauri muafaka kutoka kwa idara ya intelijensia, aliyoielezea kuyumba huku akimtaka Nurdin Haji kuwajibika kwa kulifelisha taifa la kenya kwa kutofanya kazi yake ipasavyo.
Gachagua Ameongeza kuwa Rais Ruto anapaswa kuwa na Idara imara ya intelijensia pamoja na viongozi wa intelijensia wanaoweza kutathimini hali kwa haraka na kumfahamisha kile kinachoendelea nchini.
Akiwa mjini Mombasa alikotoa hotuba hiyo, Gachagua amewaomba vijana kufutilia mbali maandamano yao kwa sababu tayari rais amewasikiliza na kufanya kile kilichohitajika kwa kuutupilia mbali muswada huo tete.
Amewataka vijana hao kuokoa maisha, kuzuwia umwagikaji damu na kuzuwia uharibifu wa mali kwa kuachana na mipango yao hiyo ili kutoa nafasi kwa serikali kuwa na mazungumzo na vijana kupata suluhu ya kisiasa.
Soma pia: Rais wa Kenya aapa kuchukua hatua kali dhidi ya maandamano ya vurugu
Amekiri kwamba serikali imewafelisha watu wake huku akitoa wito wa mpango wa kuzisaidia familia zilizoathirika kufuatia maandamano ya kuupinga muswada huo tata yaliyosababisha mauaji ya watu zaidi ya 20 huku wengine wengi wakijeruhiwa.
Amewataka pia vijana kutowaadhibu wabunge kufuatia misimamo waliyochukua.