Bunge Kenya kutoitisha kikao maalumu kujadili Sheria ya Fedha

Nairobi. Bunge la Kitaifa la Kenya halitaitishwa kwa kikao maalumu kujadili upya Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2024 ambao Rais Rais William Ruto ameamua kutousaini.

Muswada huo umeibua maandamano nchini humo kwa vijana maarufu Gen Z kuvamiwa kwa majengo ya Bunge Jumanne, Juni 25, 2024.

Spika wa Bunge hilo, Moses Wetangula, ambaye amepokea taarifa ya Rais Ruto kuhusu uamuzi wa kutosaini Muswada wa Fedha, atawataarifu wabunge wote 349 kuhusu matokeo ya hatua hiyo ya Rais.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, iwapo ujumbe kutoka kwa Rais umepokelewa wakati ambao Bunge halijakaa, Spika atalazimika mara moja kufikisha ujumbe huo kwa kila mbunge na kutangaza ujumbe huo katika kikao cha Bunge kinachofuata.

Hii inamaanisha kuwa muda mwafaka kwa Bunge kuzingatia taarifa ya Rais ya kuwataka wabunge waondoe vifungu vyote vya Muswada wa Fedha wa 2024 ni Julai 22, kufuatia mapumziko ya Bunge ya Alhamisi.

“Ujumbe wa Rais unaposomwa, ujumbe huo utahesabiwa kuwa umewasilishwa mbele ya Bunge na Spika anaweza kuagiza kwamba ujumbe huo ushughulikiwe mara moja, au kuteua siku ya kujadiliwa kwa ujumbe huo, au kuelekeza ujumbe kwa kamati husika ya Bunge ili kuujadili,” Kanuni ya Kudumu ya 42(3) inaeleza.

Bunge limekwenda mapumziko ya mwezi mmoja kuanzia Alhamisi baada ya wabunge kupitisha hoja ya kutumwa kwa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kusaidia Polisi kuzima machafuko baada ya maandamano yaliyoongozwa na vijana kusababisha uvamizi wa Bunge.

Jumatano iliyopita, Rais Ruto alikubali shinikizo kutoka kwa waandamanaji vijana na wasiwasi wa Wakenya na kuomba Bunge la Kitaifa liondoe muswada huo wote.

Ruto alikataa kuidhinisha Muswada wa Fedha wa 2024 na kutuma ujumbe kwa Bunge la Kitaifa akipendekeza wabunge kufuta vifungu vyote vinavyolalamikiwa kwenye muswada huo.

Muswada huo ungekuwa sheria moja kwa moja ndani ya siku 14 endapo Rais asingeurudisha bungeni.

Mapendekezo ya Rais kurudisha muswada huo pamoja na mapendekezo ya kufuta vifungu vyote ina maana kwamba muswada huo kitaalamu umekufa.

Ujumbe wa Rais, ambao ulipokelewa na Wetangula Jumatano jioni, umepelekwa kwenye Kamati ya Idara ya Fedha na Mipango ya Kitaifa ili kujadiliwa.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Molo, Kuria Kimani inatarajiwa kujadili ujumbe wa Rais na kuwasilisha ripoti Bunge litakapokaa tena Julai 22, 2024.

Wabunge watatakiwa kupigia kura mapendekezo ya Rais ya kufuta muswada huo wote kwa kuupigia kura kifungu baada ya kifungu.

Mbunge anayetaka kuhifadhi kipengele katika muswada au kubatilisha ujumbe wa Rais, atatakiwa kupata kura za wabunge 233 au theluthi mbili ya kura.

Pindi vifungu vyote vya muswada vikifutwa, vinaweza kuletwa tena baada ya miezi sita.

Muswada huo ulipaswa kuwa sheria ifikapo Juni 30, 2024 na kuanza kutumika kuanzia Julai 1, 2024 na kuendelea hadi Juni 30, 2025.

“Ninakataa kuidhinisha Muswada wa Fedha wa 2024, na kupeleka muswada huo kuchunguzwa upya na Bunge la Kitaifa na pendekezo la kufutwa kwa vipengele vyake vyote,” Rais Ruto alisema kwenye ujumbe wake kwa Bunge kuhusu uamuzi wake wa kutaka muswada huo uondolewe.

Serikali ilikuwa imelenga, kupitia muswada huo, kukusanya Ksh347 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/25 ili kuziba nakisi ya bajeti ya Serikali ya Ksh3.92 trilioni.

Ikiwa wabunge watapiga kura kufuta vipengele vyote vya Muswada wa Fedha wa 2024 kama ilivyopendekezwa na Rais Ruto, serikali itaendelea na hatua za kuongeza mapato zilizopitishwa mwaka wa fedha 2023/24.

Vijana wa Kenya wameingia mitaani tangu wiki iliyopita katika kampeni kubwa ya kuwataka wabunge kutoidhinisha muswada ambao ulipendekeza ongezeko la kodi na tozo kwa watu binafsi na wafanyabiashara, lakini wabunge hao hawakujali, walipitisha muswada huo Jumanne wakati kukiwa na maandamano katika kaunti 35 kati ya 47.

Related Posts