Chama la Wana lasaka makocha

BAADA ya kubaki Ligi ya Championship na kuachana na kocha wake, Seleman Kitunda mwishoni mwa msimu, Klabu ya Stand United inasaka kocha mkuu mpya na kocha wa makipa ili kuboresha benchi lake la ufundi na kufanya vizuri msimu ujao.

Timu hiyo yenye maskani yake mkoani Shinyanga ilinusurika kushuka daraja kutoka Championship baada ya kushinda mchezo wa mtoano dhidi ya Copco FC iliyoshuka kwenda First League, huku ikiachana na kocha mkuu, Seleman Kitunda aliyeiongoza kwenye mechi tatu za mwisho.

Katibu Msaidizi wa klabu hiyo, Fredy Masai, alisema watalifanyia maboresho benchi lao la ufundi kwa kumleta kocha mkuu na kocha wa makipa, huku wakijiandaa na usajili wa dirisha kubwa ili wafanye vyema na kuipandisha daraja kwenda Ligi Kuu.

Alisema tayari makocha wanne wameshatuma maombi ya nafasi ya kocha mkuu huku wakiendelea kupokea wengine ambapo kamati itakaa kuyapitia na kupitisha jina la mkuu wa benchi la ufundi atakayewaongoza msimu ujao kwa mafanikio.

“Kwenye benchi tutaongeza watu wawili tunasubiri kamati ikae itapendekeza watu gani tuwachukue, kuna majina watu wengi wameshaomba tumewaambia watulie tukamilishe taratibu kamati ikikaa tupeleke majina yao,” alisema Masai na kuongeza;

“Hatuwezi kuwa na haraka kwenye usajili tunasubiri tukifanya tafakari na kufanya mipango. Malengo ni kuwa na timu ya Ligi Kuu tunaangalia wapi tulipojikwaa turekebishe tufanye vizuri tupandishe timu ili tuchangamshe mkoa.”

“Tunajiandaa na usajili wa dirisha kubwa mashabiki wakae mkao wa kula muda si mrefu watasikia. Pia kutakuwa na mabadiliko tunaendelea na mipango ya chini tutakuja kueleza kuhusu usajili na uendeshaji wa timu,” alisema.

Related Posts