Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC), Mkoa wa Dar es Salaam, Saad Mtambule ametoa wito kwa wadau wa nishati mbadala kubuni mbinu zitakazowavutia Watanzania wa makundi mbalimbali kutumia nishati safi ya gesi kupikia.
Mtambule ametoa wito huo leo Alhamisi, Juni 27, 2024 katika uzinduzi wa mpango maalum unaotoa punguzo la bei ya nishati hiyo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Uzinduzi wa mpango huo iliyofanyika eneo la Changanyikeni, wilayani humo iliambatana na uzinduzi wa duka maalum la Kampuni Taifa Gas litakalowahudumia wanafunzi hao kwa punguzo hilo la bei.
Hafla hiyo imeenda sambamba na ugawaji bure wa mitungi ya gesi 300 kutoka Taifa Gas kwenda kwa baadhi ya wanafunzi hao kutoka vyuo vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Takwimu, Chuo cha Ardhi na Chuo cha Maji na wakazi wa maeneo jirani ili kuchochea hamasa ya mpango huo.
Mtambule amesema huduma hiyo imekuja katika kipindi ambacho Serikali inapambana kuwasaidia na kuwawezesha wananchi kupitia makundi mbalimbali kuifikia nishati hiyo kwa urahisi.
“Ni faraja kubwa zaidi kwetu kama Serikali kuona wakati tunaendelea kufanikisha mkakati wa kufikia nishati safi ifikapo 2034 tayari wadau kama Taifa Gas wameanza kubuni mbinu mbalimbali za kijamii na kimasoko zitakazotusaidia kama taifa kufanikisha adhma hiyo.
Kupitia huduma hii ya punguzo la bei kwenye kila mtungi wa gesi wanafunzi wa vyuo vikuu watavutiwa zaidi na kuona matumizi ya gesi kama suluhisho sahihi la nishati ya kupikia…hongereni sana Taifa Gas,’’ amesema.
Awali, akifafanua kuhusu mpango huo, Meneja Mauzo wa Taifa Gas, Joseph Nzumbi amesema unahusisha wanafunzi wa vyuo vikuu jijini Dar es Salaam wenye vitambulisho halali ambao watapata mapunguzo tofauti kulingana na uzito wa mitungi ya gesi watakayonunua.
“Kwa mfano bei ya kujaza mtungi wa gesi wenye uzito wa kg 6 badala ya wanafunzi kuuziwa kwa Sh 23,000 kupitia mpango huu watauziwa kwa Sh20,000 na kwenye mtungi wenye uzito wa kg 15 wanafunzi watajaziwa gesi kwa Sh50,000 badala ya Sh55,000. Tumeanza na Dar es Salaam na tutaendelea kwenye vyuo vingine zaidi maeneo mengine,’’ amesema.
Nzumbi amesema kampuni hiyo imejipanga kuhakikisha kwamba kila Mtanzania mwenye nia ya kutumia nishati safi ya gesi anapata fursa hiyo kupitia mikakati mbalimbali inayoendelea kubuniwa na kampuni hiyo kwa kuzingatia mahitaji ya makundi tofauti ya kijamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitivo Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Wenslaus Richard amesema:” Wanafunzi ni kundi ambalo bado halijaanza kujitengenezea kipato chao wao wenyewe hivyo wapo makini sana na masuala ya bei ya bidhaa wanazotumia hususani kwa wale wanaojipikia kwenye maeneo yao.”
Richard amesema ujio wa mpango huo wa punguzo la bei utakuwa kimbilio kwao ili waweze kuokoa fedha zao.