WAKATI Simba na Coastal Union zikiendelea kuvutana kuhusu usajili wa beki, Lameck Lawi aliyefanya vizuri msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Bara, Klabu ya Copco imejivunia kumzalisha na kumkuza nyota huyo huku akiwapa mzuka wa kuzalisha vijana wengine.
Lawi ambaye siku chache zilizopita alitangazwa kusajiliwa na Simba akitokea Coastal Union, ni zao la Copco ya Mwanza kwani alikuwa sehemu ya kikosi kilichoipandisha daraja kutoka First League kwenda Ligi ya Championship mwaka 2022.
Nyota huyo alidumu kwa msimu mmoja Championship akiwa na Copco kabla ya kusajiliwa na Coastal msimu uliofuata akifanya vizuri na kuzivutia timu nyingi. Copco FC ambayo itashiriki First League msimu ujao, imeamua kujikita kwa vijana na kuwapa fursa ya kuendeleza vipaji vyao.
Kocha wa timu hiyo ambaye alimkuza beki huyo, Feisal Hau, alisema klabu yao iliingia makubaliano na Coastal Union ya kunufaika na mauzo ya Lameck Lawi, hivyo wanasubiri mvutano huo umalizike wavune chao.
Alisema kwa sasa wanajipanga na First League wakishiriki mashindano mbalimbali ya mchangani na kucheza michezo ya kirafiki kuwaona vijana wao chipukizi ambao watawatumia kwenye michuano hiyo.
“Tulimtoa Lawi, leo amekuwa lulu wanamgombea hiyo ni hela na kuna makubaliano tuliyafanya na Coastal naamini wakimaliza mvutano, mambo yatakuwa sawa. Vijana wanalipa na hilo ndilo lengo la timu yetu msimu ujao wataonekana wengi,” alisema Hau na kuongeza;
“Timu yetu ipo haitauzwa na tunajiandaa kushiriki ligi tunacheza mechi za kirafiki, tunashiriki mashindano wilayani Magu na tuna timu yetu ya vijana kwenye ligi ya Championship, kwahiyo tumeamua tutawatumia zaidi vijana wetu ili watusaidie.”