Gamondi awaita Chama, Dube fasta

KUNA ujumbe ambao Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ameutuma kwa viongozi na wachezaji bila kujali wale wapya ambao wanatajwa kusajiliwa Prince Dube, kiungo Clatous Chama kila mmoja anatakiwa kufanya hivyo.

Ujumbe ambao Gamondi ameutuma kisha fasta mabosi wa Yanga kuufikisha kwa mastaa hao ni kila mchezaji anatakiwa ahakikishe ikifika Julai Mosi awe hapa nchini kuanza maandalizi ya kuelekea msimu mpya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema kutokana na kalenda ya kimashindano aliyoipata maandalizi yao yatawahi kuanza kuhakikisha wanakuwa tayari kabla ya muda wa mashindano kuanza.

Gamondi alisema ukiacha ratiba ya kuandaa kikosi na hata mechi za kirafiki, timu  hiyo itakuwa na mechi za Ngao ya Jamii ambapo mchezo wa kwanza utakuwa kati yao na watani wao Simba wanaoshikilia taji hilo, ililotwaa Agosti 13 mwaka huu katika fainali iliyopigwa jijini Tanga na Yanga kulala kwa penalti 3-1.

Kocha huyo, anayevizia tuzo ya kocha bora wa msimu baada ya kuipa Yanga mataji mawili alisema ametaka kila mchezaji kuwepo mapema kwa wale wapya na hata wale ambao wamesalia.

“Tuna ratiba ngumu sana mashindano mengi yamekuwa karibu kulingana na kalenda ambayo nimepatiwa, hapa lazima tuanze kujiandaa haraka ili kila kitu kiwe sawa,” alisema Gamondi.

“Kila mchezaji anatakiwa kuwahi ili ratiba iwe kwa pamoja, nadhani viongozi watalifanya hili kwa weledi, kuna faida kubwa kama maandalizi ya mwanzo ya msimu yakafanyika kwa kila mtu kuwa hapa.

Hadi sasa Yanga inaelezwa imeshamalizana na kipa Abubakar Khomeiny, beki Chadrack Boka, kiungo Clatous Chama na mshambuliaji Prince Dube.

Bado Yanga haijathibitisha kambi ya maandalizi kwa ajili ya msimu ujao itakuwa wapi, huku ikitajwa huenda ikawa kati ya Russia, Afrika Kusini na sasa inatajwa Uturuki. 

Related Posts