Kinachoendelea mgomo wa wafanyabiashara Dar, mikoani

Mikoani. Ikiwa ni siku ya nne tangu kutangazwa kwa mgomo wa wafanyabiashara nchi nzima, baadhi yao wameamua kufungua maduka na kuendelea na biashara kama kawaida huku wengine wakiendelea kuyafunga.

Wafanyabiashara hao wameamua kugoma kuishinikiza Serikali kufanyia kazi malalamiko yao ambayo ni pamoja na kupunguza utitiri wa kodi na ushuru wanazolipa, unyanyasaji unaofanywa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati wakikagua mashine za kielektroniki za kodi (EFD) na ritani za kodi.

Leo Alhamisi Juni 27, 2024 Mwananchi Digital limefika katika masoko mbalimbali nchini na kushuhudia baadhi ya wafanyabiashara wakiendelea na shughuli zao wakati wengine wakiendelea kugoma kama ilivyotangazwa awali.

Katika eneo la Kariakoo mkoani Dar es Salaam ambalo wafanyabiashara ndiyo walioanzisha mgomo huo tangu Jumatatu Juni 24, 2024, baadhi yao wamefungua maduka yao na kuendelea na biashara huku maduka mengine yakiwa yamefungwa kama ilivyokuwa jana.

Mwananchi Digital limeshuhudia maduka yakiwa yamefungwa katika eneo hilo maarufu kwa biashara wakisubiri Serikali kutatua kero walizozibainisha ndipo waendelee kufanya biashara kama kawaida.

Katika Jiji la Arusha, wafanyabiashara wamefungua maduka yao wakiendelea na shughuli zao kama kawaida wakati wenzao katika mikoa mingine wakiendelea kugoma kuishinikiza Serikali kufanyia kazi madai yao.

Hata hivyo, wenzao wa Songea Mjini mkoani Ruvuma, wafanyabiashara wamefunga maduka yao wakishinikiza Serikali kupunguza utitiri wa kodi.

Huko jijini Mbeya, baadhi ya wafanyabiashara wameanza kutumia “njia za panya” kuuza bidhaa zao huku wengine wakifungua.

Mgomo huo ambao ulianza kutikisa tangu Juni 25, 2024 hadi sasa haujasitishwa ikiwa maduka mengi yameendelea kufungwa, huku athari zikitajwa kwa baadhi ya wananchi na wajasiriamali kwa kukosa mzunguko wa fedha pamoja na bei za bidhaa kupanda.

Wafanyabiashara soko la Sido jijini Mbeya wakifungua rasmi maduka baada ya kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao kufuatia mgomo wao uliodumu kwa takribani siku tatu.

Mwananchi Digital imefika katika Soko la Sido jijini humo na kushuhudia idadi kubwa ya vibanda vya machinga kuongezeka, huku wafanyabiashara wakifungua maduka yao kutoa mizigo kutandaza nje bidhaa kisha kuyafunga maduka.

Pia, wengine wameonekana kubuni mbinu mpya ya kupanga bidhaa zao kwenye ukuta wa maduka na kuendelea na shughuli zao wakisubiri wateja.

Mwananchi imeshudia moja ya duka kubwa maarufu la wauzaji wa mabegi na mikoba ya kike “Sharifu Makoba” likiwa wazi huku wateja wakiwa wamelizunguka wakichukua mzigo.

Wengine waliofungua maduka yao ni wafanyabiashara wa viatu ambapo takribani maduka saba yako wazi katika soko hilo huku wengine wakifungua nusu mlango.

Hata hivyo, idadi ya watu wanaoingia na kutoka kwenye soko hilo asubuhi hii ya Juni 27, 2024 ikiwa ndogo ikilinganishwa na siku za nyuma kabla ya kuwapo mgomo huo.

Mjini Morogoro, baadhi ya wafanyabiashara wa maduka ya bidhaa za jumla na rejareja katika Mtaa wa Nunge wamefanya mgomo wa kutofungua maduka kwa madai ya kutozwa kodi kuwa kubwa ikiwemo tozo ya huduma ambayo imekuwa kero na changamoto kwao katika manispaa ya Morogoro.

Baadhi ya Maduka yaliyopo Mtaa wa Kindemile Na mtaa wa Sultan Manispaa ya Morogoro wakiwa wamefunga Maduka yao.

Mmoja wa wafanyabiashara wa nafaka, Sundeo Sume amesema wamefunga maduka leo Juni 27, 2024 wakishinikiza Serikali kuondoa tozo ya huduma, wakiungana na wafanyabiashara wenzao nchi mzima kutokana na utitiri wa kodi.

“Kama kodi ikiwa kubwa maana yake mfanyabiashara anapata harasa na kudidimia kimaendeleo kutokana na kodi kubwa tunayotozwa wafanyabiashara,” amesema Sume.

Sume amesema wamewataka viongozi wao Mkoa wa Morogoro kulishughulisha suala hilo kwa kuondoa kodi na tozo ambazo zimekuwa zikiwaumiza.

Related Posts