Kipre Jr wa Azam huyooo USM Alger

BAADA ya kung’ara katika msimu wa pili wa kucheza katika Ligi Kuu Bara akihusika na mabao 18 akiwa na Azam FC, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Kipre Jr hatakuwa sehemu ya kikosi msimu ujao baada ya uongozi wa timu hiyo kumuuza USM Alger kwa dau nono.

Kiungo huyo aliyefunga mabao tisa na kuasisti tisa vile vile inaelezwa ameuzwa kwa mabingwa hao wa zamani wa Kombe la Shirikisho  kwa dau linalokadiliwa kuwa zaidi ya Sh500 Milioni.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Azam kililiambia Mwanaspoti ni kweli biashara hiyo imefanyika na Azam FC wameweka kipengere cha endapo staa huyo atatakiwa kurudi Tanzania basi ni lazima aanzie hapo kama watakuwa na uhitaji naye.

Kilisema mazungumzo ya mwanzo walishindwa kufikia mwafaka kutokana na dau dogo lililopendekezwa na timu hiyo lakini sasa mambo yamekwenda vizuri baada ya makubaliano ya pande zote kwenda sawa.

“Mwanzo yalikuwa ni mazungumzo na hatukufikia muafaka ndio maana nilikwambia dili hilo halipo, lakini sasa mambo yamekwenda sawa kati yetu mchezaji na USM Alger hivyo Kipre hatakuwa sehemu ya kikosi chetu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Tunatamba ubora na umuhimu aliokuwa nao ndani ya kikosi chetu na kufanya biashara hiyo haina maana sisi hatakuwa na mpango naye hapana tumefanya hivyo kwasababu ilikuwa ni biashara nzuri kwetu na tuna imani na wachezaji waliopo kuwa wanaweza kuziba pengo lake na muda wa kusajili bado upo.”

Chanzo hicho kiliongeza kuwa bado kutakuwa na biashara ya mastaa wengine wengi ambao wamepokea ofa zao kutoka timu za ndani na nje hivyo mashabiki wa timu hiyo na wadau wa soka watarajie taarifa nyingine nyingi kama mambo yaraenda sawa.

“Mpira ni biashara, Kipre Jr alibakiza mwaka mmoja na hakutaka kuongeza mkataba mwingine, hivyo endapo tungebania biashara hiyo kufanyika basi msimu ujao tungemtoa bure ni mchezaji mzuri lakini tunaamini tutapata wengine wazuri ambao wataipambania Azam kimataifa na michuano ya ndani,” kiliongeza chanzo hicho.

Kipre alisajiliwa na Azam misimu miwili iliyopita akisainishwa mkataba wa miaka mitatu akitokea klabu ya Sol FC ya Ivory Coast anakotokea mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 na aliyekuwemo kwenye kikosi bora cha msimu huu cha Ligi Kuu ya Ivory Coast (Ligue 1) 2021-2022, amewahi kusajiliwa na miamba ya Ufaransa, Strarsbourg msimu wa 2017-2018.

Kiungo mshambuliaji huyo mwenye kipaji cha hali ya juu pia aliwahi kuwatumikia vigogo wa Ivory Coast, Asec Mimosas, 2018-2020 na ubora ulimbeba na kuichezea timu za taifa za vijana za Ivory Coast U-15 na U-17, pamoja na kikosi cha wachezaji wa ndani (CHAN) 2020.

Msimu wa kwanza ndani ya Azam FC haukuwa mzuri kwa Kipre Jr, kwani alifunga mabao mawili tu na kuasisti mara nne, lakini msimu wa pili ambao umemalizika hivi karibuni alikuwa kwenye kiwango bora akishirikiana na kiungo Feisal Salum’Fei Toto’ na Jibril Sillah na kuiwezesha Azam kumaliza nafasi ya pili Ligi Kuu Bara na kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika miaka 10 tangu iliposhiriki mara ya mwisho 2014.

Licha ya kufunga mabao manane, lakini ni mmoja kati ya wachezaji waliofunga hat trick kwa msimu uliomalizika hivi karibuni akiwa sambamba na Stephane Aziz KI wa Yanga aliyefunga mara mbili, Fei Toto aliyefunga moja, kama ilivyokuwa kwa Jean Baleke (Simba), Waziri Junior (KMC) na Ismail Mgunda (Ihefu).

Related Posts