Maandamano zaidi yanukia Kenya, vijana wabadili kaulimbiu

Dar es Salaam. Licha ya Rais William Ruto kurudisha Muswada wa Fedha, 2024 bungeni, maandamano zaidi yanatarajiwa nchini Kenya leo Juni 27, 2024, huku waandamanaji wakitaka kwenda Ikulu kushinikiza kiongozi wa nchi hiyo ajiuzulu.

Hiyo ni kutokana na hali ya hasira na kutoridhika miongoni mwa wananchi kuhusu hali mbaya ya kiuchumi na ongezeko la ushuru.

Tayari waandamanaji wameonekana jijini Nairobi na wengine mji wa Eldoret wakiandamana, huku Jeshi la Polisi likiwadhibiti.

Jana Juni 26, Rais Ruto alieleza hatua zilizochukuliwa na Serikali kukwamua uchumi ikiwa pamoja na kupunguza deni la Serikali.

Aliutetea muswada uliokataliwa akisema ulilenga kuongeza walimu, kuongeza fedha kwenye kilimo, afya na ujenzi wa barabara.

Hata hivyo, watu wengi wanasema kuwa kurudishwa kwa muswada huo hakutoshi kwani bado kuna masuala mengi ya kiuchumi ambayo hayajashughulikiwa.

Viongozi wa upinzani na wanaharakati wameendelea kushinikiza Serikali kuchukua hatua madhubuti za kupunguza mzigo wa kiuchumi kwa wananchi.

Bado Rais Ruto na serikali yake wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kurejesha imani ya wananchi huku wakitafuta suluhu za kudumu za matatizo ya kiuchumi.

Wakenya wanahisi kusalitiwa

Katika kampeni yake ya urais, Ruto alijieleza kama mgombea wa kupinga mfumo uliopo na akaahidi kutekeleza sera za kuweka pesa zaidi kwenye mifuko ya Wakenya.

Lakini wafuasi wake walivunjika moyo wakati Serikali yake ilipoondoa ruzuku muhimu za mafuta na unga wa mahindi. Wakenya wengi waliona hili kama usaliti.

Ruto mara kwa mara anawataka Wakenya kubana mikanda. Lakini ziara yake rasmi nchini Marekani mwezi Mei ilizua utata alipokodi ndege ya kifahari badala ya kutumia ndege ya rais au shirika la ndege la kitaifa la Kenya.

Baadaye, Ruto alisema kuwa ndege hiyo iliyokodiwa ililipiwa na marafiki ambao hakuwataja.

Kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu inayofadhiliwa na serikali ya Kenya, idadi ya vifo ilikuwa 22 siku ya Jumatano, na 19 kati ya hao waliripotiwa jijini Nairobi.

Wakati huohuo, Jeshi la Polisi lilisema vifo vilikuwa vimefikia 30 na vilirekodiwa Githurai pekee, nje ya Nairobi, kulingana na ripoti.

Mbunge wa Congress ya Marekani, Ilhan Omar, amesema matumizi ya nguvu hatari yaliyoonekana wakati wa maandamano yaliyofanyika Kenya “yanadhoofisha misingi ya kidemokrasia ya Kenya”.

Akiandika kupitia ukurasa wake wa X, Omar pia alisema ni “lazima waandamanaji wabaki na amani”.

Akijadili suala hilo, mtafiti katika Taasisi ya Masomo ya Usalama (ISS), Willis Okumu amesema Rais Ruto anachelewesha muda.

“Nadhani [Ruto] anachelewesha muda tu,” alisema, alipokuwa akizungumza na Al Jazeera kuhusu tangazo la Rais wa Kenya la kuondoa muswada huo.

“Nadhani ameambiwa kuwa hii ina madhara kisiasa. Inawezekana shinikizo kutoka kwa mataifa ya Magharibi limechangia. Alikuwa anahitaji kutuliza hali baada ya kufanya makosa na anajaribu kuwaridhisha vijana. Amegundua atapoteza nchi.

“Siamini kuwa ni ya kweli; mambo hayo yote, sidhani kama atayatekeleza. Amekuwa rais kwa miaka miwili na hajatimiza chochote kati ya alichoahidi.”

Watu wengi nchini Kenya wanasema hawajawahi kuona jambo kama hili hapo awali. Kilichoanza kama maandamano ya amani Jumanne kiligeuka haraka na kuwa vurugu wakati mamia ya waandamanaji walipovamia Bunge.

Polisi walitumia mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na risasi za moto. Watu kadhaa waliuawa na wengi walijeruhiwa.

Mama wa mwandamanaji aliyekufa baada ya kupigwa risasi kifuani alisema kuwa licha ya Ruto kutoa uamuzi, haitamrudisha mwanawe mwenye umri wa miaka 20. Wakenya wengi wanaaminika kuunga mkono maandamano dhidi ya muswada huo.

IMF yasema ‘inachunguza hali kwa karibu’

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linasema kuwa lina wasiwasi kuhusu matukio zaidi ya kusikitisha nchini Kenya wakati wa maandamano na linafuatilia kwa karibu.

“Lengo letu kuu katika kusaidia Kenya ni kuiwezesha kushinda changamoto ngumu za kiuchumi inazokabiliana nazo na kuboresha matarajio yake ya kiuchumi na ustawi wa watu wake,” imesema taarifa ya IMF.

Jana kabla ya Rais Ruto kutoa hotuba yake ya kurudisha muswada wa fedha bungeni, kulikuwa na majadiliano makali na ya dharura kati yake na timu yake ya washauri pamoja na wanadiplomasia.

Kwa mujibu wa mtandao wa Nation, watu walioshiriki na waliokuwa na habari kuhusu mikutano hiyo, walifichua juhudi za usiku kucha za kupunguza mvutano nchini baada ya waandamanaji kuvamia majengo ya Bunge na kuapa kuandamana hadi Ikulu.

Rais alitafuta ushauri kuhusu jinsi ya kushughulikia mgogoro wa kitaifa uliokuwa ukiendelea na kuchunguza hali mbalimbali zilizojitokeza kutoka kuendeleza muswada huo.

Baadhi wamekuwa na msimamo kuongeza shinikizo wakitaka utawala kujiondoa madarakani. Wengine wanaona ni hoja dhaifu ambayo haipaswi kuhusishwa na kiongozi wa nchi.

Mikutano hiyo iliitishwa kabla na baada ya hotuba ya Rais kwa taifa iliyotolewa muda mfupi baada ya saa tatu usiku.

Akitangaza uamuzi wake wa kukataa kutia saini Muswada wa Fedha, 2024, Rais siku ya Jumatano, Juni 26, aligusia mikutano hiyo ya muda mrefu aliposema: “Nimejadili na wadau wengi, nitakutana na baadhi yao muda mfupi baada ya hii, kuamua njia ya mbele na kuhakikisha tunachukua taifa zima katika safari hii muhimu  tunapoendelea kama nchi.”

Watu waliohudhuria mikutano hiyo walielezea jinsi Rais alivyokuwa katikati ya makundi mawili; wenye msimamo mkali waliouona mgogoro wa kitaifa kama fursa kwa Rais kuthibitisha mamlaka yake kwa kutumia vikosi vya usalama kukandamiza waandamanaji na kushughulikia matokeo ya kisiasa.

Kwa upande mwingine kulikuwa na maoni kwamba huu ulikuwa wakati mwafaka wa kuonyesha uimara katika uongozi na kuongoza nchi.

Nation imebainisha kuwa Idara ya Usalama wa Taifa (NIS) ilimshauri Rais kabla na baada ya maandamano ya Jumanne kuupitia upya Muswada wa Fedha na kutafuta njia za kujumuisha umma, hata kama ingeusimamisha kwa muda mchakato huo.

Imeelezwa kwamba ushauri kutoka NIS, hata hivyo, haukukubaliwa na watu wenye msimamo mkali ndani ya Baraza la Mawaziri na wanachama wakuu wa washauri wake wa kiusalama na kiuchumi.

“Rais yuko kweli kwenye shoka la msalaba, na mashauriano bado yanaendelea. Kwa sauti za busara kushinda, kuna matumaini kwamba atachukua msimamo utakaouondoa nchi kutoka kwenye njia ya machafuko, vifo na uharibifu ulioshuhudiwa Jumanne,” walisema vyanzo hivyo.

Wale waliopinga kuachana na muswada walidai kuwa itakuwa vigumu kujua wapi vijana wataishia wakati mwingine watakapokasirishwa na suala la kitaifa.

Baadhi ya wabunge pia walimfikishia maoni Rais wakisema kuwa tayari wamewekeza mtaji mkubwa wa kisiasa kwa serikali kuachana na muswada huo wa Fedha, 2024.

Mataifa yenye nguvu za Magharibi

Taarifa za ndani zinaeleza kwamba Rais Ruto pia alipokea simu Jumanne na Jumatano kutoka kwa wawakilishi wa kidiplomasia wakimtaka aachane na msimamo mkali na kugeukia kutafuta njia ya maridhiano.

Katika taarifa zao za umma, Balozi na Tume za Juu za Uingereza, Ubelgiji, Kanada, Denmark, Finland, Ujerumani, Ireland, Uholanzi, Norway, Estonia, Sweden, Romania, na Marekani walihimiza: “Wahusika wote wana jukumu la kuheshimu, kutekeleza, kukuza, na kutimiza kanuni za demokrasia na utawala wa sheria, hasa kwa kuhakikisha majibu ya kiusalama yanayofaa.”

“Tunakaribisha ushiriki wa raia na Wakenya wote, hasa vijana, katika kushughulikia masuala ya umma yaliyo muhimu. Tunatoa wito kwa pande zote na kuhimiza viongozi wote kupata suluhisho la amani kupitia mazungumzo,” sehemu ya taarifa ilieleza.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema katika taarifa: “Nimehuzunishwa na ripoti za vifo na majeruhi ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari na pia hali ya watoa huduma za afya nchini Kenya.

“Nawataka viongozi wa Kenya kuwa na kiasi na kutoa wito kwa maandamano yote kufanyika kwa Amani,”  alisisitiza.

Hata hivyo inaelezwa kwamba, kurudishwa muswada huo bungeni kunatarajiwa kuruhusu majadiliano zaidi na pia kutasaidia kupunguza mvutano uliolikumba taifa hilo.

Imeandikwa na Mashirika ya habari

Related Posts