Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Kongamano Mahakama linalohusisha Majaji wa Tanzania, Majaji kutoka Mahakama ya Uingereza na Kenya, Naibu Wasajili na Mahakimu wa Mahakama ya Tanzania. Kongamano linalofanyika jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Juni 26, 2024.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Eva Nkya akizungumza wakati wa kongamano la Mahakama linalofanyika jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Juni 26, 2024.
JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema Shirika la Haki Miliki Bunifu Duniani (WIPO) limesadia mahakama kupiga hatua kubwa katika kuboresha utoaji haki kwenye eneo la mashauri yanayohusu umiliki wa haki bunifu.
Hayo ameyasema wakati wa ufunguzi wa kongamano la kimataifa kuhusu miliki bunifu, usimamizi wa mashauri ya haki miliki na alama za biashara lililoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na WIPO,. Kongamano hilo linaendelea kufanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Juilius Nyerere jijini Dar es Salaam. Amesema kongamano hilo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano yaliyosaniwa kati ya mahakama na WIPO mwaka 2021.
Ameongeza kuwa kongamano hilo litawarahisishia mahakimu na majaji kufanya rejea ya maamuzi ya mahakama kwa wepesi ili kuwawezesha kufanya tafiti za kisheria zinazohusiana na mashauri ya miliki bunifu.
“Kuanzia mwaka 2022-2023, Shirika la Miliki Bunifu Duniani limekuwa likitoa ufadhili wa mafunzo kwa majaji na mahakimu kwa njia ya masafa yakilenga kuwajengea uwelewa eneo la miliki bunifu.” Ameeleza
Kwa Upande wa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Eva Nkya Katika kipindi hiki cha siku mbili za Kongamano, mada mbalimbali zaitawasilishwa na wawezeshaji mahiri waliobobea katika maeneo ya haki miliki ni miongoni mwa mada hizi ni hali ya uendeshaji wa mashauri ya Miliki Bunifu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Kanuni za Ulinzi wa Alama za Biashara; Uvunjifu wa Alama za Biashara; Kanuni za Ulinzi wa Haki Miliki; Uvunjifu wa Haki Miliki, Mahitaji ya Kiushahidi, Ushahidi wa Kidijitali katika Mashauri ya Alama za Biashara, Hatua za Nafuu za Dharura, Mbinu za Usimamizi wa Mashauri ya Miliki Bunifu, Namna ya Kuharakisha Usikilizaji wa Mashauri ya Miliki Bunifu kwa kuangalia nchi zinazofanya vizuri kama Uingereza na Fursa na Changamoto katika Kuimarisha Usimamizi wa Mashauri ya Miliki Bunifu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Licha ya hayo amesema katika kipindi cha miaka mitano Mahakama ya Tanzania, imepiga hatua kubwa sana katika kuboresha utoaji haki katika eneo la mashauri yanayohusu Miliki Bunifu kwa kushirikiana na Shirika la Miliki Bunifu Duniani ‘World Intellectual Property Organisation (WIPO)’.
Miongoni mwa mafanikio yanayotokana na ushirikiano huo ni pamoja na kuandaa miongozo juu ya haki miliki (Copyright), alama za biashara (trademarks), hataza (patent) na maumbo bunifu (Industrial design). Miongozo hiyo inatumiwa na waheshimiwa Majaji na Mahakimu kama rejea pale wanapokuwa wanaendesha na mashauri yanayohusu miliki ubunifu.
Akiishukuru Mahakama Afisa Mtendaji Mkuu Ofisi ya Haki Miliki Tanzania (COSOTA), Dorine Sinare amesema mafunzo hayo yamekuja wakati mwafaka kwani wadau mbalimbali wakiwemo wasanii wataweza kupata haki zao miliki za biashara kupitia mhimili wa mahakama.
Kufanyika kwa Kongamano hilo Tanzania ni moja ya juhudi zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania ili kuimarisha utoaji wa haki katika Haki Miliki, Alama za Biashara na Usimamizi wa Mashauri.
“Nashukuru Mahakama na Shirika la hakimiliki bunifu duniani (WIPO) kwa jitihada za kutoa mafunzo haya na kuwafikia watanzania.”
Amesema COSOTA, imesema mafunzo hayo ni muhimu kwasababu kulikuwa na ukiukwaji wa haki miliki, kuzulumiwa haki kimziki, kwenye filamu, kwenye vitabu, kwenye sanaa za ufundi, softwere zinazotengenezwa sasa anaweza kupeleka Mahakamani.
Amesema mahakama kupata mafunzo maana yake kesi zitakwenda vizuri na wadau watanufaika na kupata haki zao kupitia mahakama zilizopo hapa nchini.
Kongamano hilo la siku mbili limehudhuriwa na watendaji mbalimbali wa mahakama zaidi ya 200 ambao ni Majaji wa Tanzania, Majaji kutoka Mahakama ya Uingereza na Kenya, Naibu Wasajili na Mahakimu wa Mahakama ya Tanzania pamoja na wadau wengine.