MAKATIBU WAKUU WAKAMILISHA MAANDALIZI YA MKUTANO WA 45 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC

Makatatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana jijini Arusha kwa mkutano wa siku tatu (3) kuanzia tarehe 25 hadi 27 Juni, 2024 ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa 45 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 28 Juni 2024.

Mkutano huo wa Makatibu Wakuu ulitanguliwa na mkutano wa wataalam uliofanyika tarehe 22 hadi 24 Juni, 2024 umepokea na kupitia taarifa na mapendekezo yaliyowasilishwa na Mkutano wa wataalam kuhusu masuala mbalimbali ya kikanda yatakayowasilishwa kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri.

Masuala ya kikanda yaliyojadiliwa ni taarifa ya utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa na baraza hilo kwenye vikao vilivyopita, taarifa kuhusu masuala ya forodha na biashara na taarifa ya miundombinu, sekta za uzalishaji, sekta za jamii na masuala ya kisiasa.

Taarifa nyingine ni taarifa ya kamati na fedha, taarifa ya kamati ya rasilimali watu, taarifa ya mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 17 Mei, 2024 pamoja na taarifa ya ratiba za matukio ya jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba, 2024.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa Makatibu Wakuu umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki – anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi ambaye ameambatana na, Naibu Katibu Mkuu, Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji (Uchumi na Uwekezaji) Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Rashid Ali Salim, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Dkt. John Simbachawene

Viongozi wengine ni, Mkurugenzi wa Uendelezaji Sera kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cyrus Kapinga, Kamishna Msaidizi Utafiti kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Kanali Bonus Nombo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uwekezaji Sekta Binafsi Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Bw. Fadhili Chilumba na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Kijamii, Mhandisi Abdillah Mataka.





Related Posts