Malejendi watangaza kurudi mbio za magari

MADEREVA na waongozaji (navigators) wa timu Stado wametangaza kurudi mchezoni baada ya miaka saba ya ukimya na kutojihusha na mchezo huu pendwa.

Samir Nahdi Shanto, mmoja wa madereva wa timu hiyo, akiongea na Mwanaspoti kutoka mjini Morogoro, alisema wanarudi tena mchezoni na safari hii wanakuja na mashine ya kisasa iitwao Ford Proto.

“Stado Team wote tunarudi kikamalifu kusaidia kuufanya mchezo wa mbio za magari kurudi katika ubora wake wa miaka ya 2000,” alieleza. 

Shanto alimtaja dereva kutoka Iringa, Ahmed Huwel Mkwawa, madereva waongozaji Maisam Fazal na Rahim Suleiman kutoka Dar es Salaam kama wanachama wa timu ya Stado ambao wanarudi nyuma ya usukani na kuufufua mchezo huo ambao umeonekana kudorora miaka ya karibuni.

Akiwa na gari ya kisasa aina ya Ford Proto, Shanto amesema atashirikiana na Rahim Suleiman kama dereva mwongozaji, wakati Ahmed Huwel atakuwa na Maisam Fazal.

Hata hivyo, Shanto alisema timu yake haitashiriki katika mashindano ya ufunguzi wa msimu ya Advent Rally ya mjini Tanga lakini watakuwa tayari kwa raundi nyingine zitakazofanyika Iringa, Morogoro na Dar es Salaam. 

“Mchezo wa mbio za magari umepoteza mvuto wake kitaifa na hata kimataifa. Wakati wa zama za timu ya Stado tulicheza  mashindano mengi ya ngazi ya Afrika (African Rally Championship) Kenya, Uganda, Afrika Kusini na nyumbani Tanzania,” alikumbushia.

Ubora wa timu ya Stado, kwa mujibu ya Shanto, ulichangia  kwa kiasi kikubwa kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi nane Afrika kupewa heshima ya kuandaa moja ya raundi nane za ubingwa wa bara hili.

Stado timu kwa mujibu wa Shanto ni jina linalojumuisha majina ya madereva watano yakianza na Shanto, Twalib, Ahmed, Davis Mosha na Omary Bakhressa, kabla ya dereva mkongwe Pano Calavria kujiunga nao baadaye.

“Siamini kama mchezo huu umefikia hatua hii Tanzania. Nakumbuka mwaka 2006, Watanzania tuliwapa Wakenya wakati mgumu tukiwa na gari mpya za Subaru Impreza N10 na N11 zilizokuwa bora sana miaka hiyo. Alisema Huwel aliyeshinda Super Specaial Stage ya KBC Rally 2006, wakati Pano, Navraj Hans na Kirit Pandya wakiwa ni madereva waliowahi kufanya vizuri nje ya Tanzania enzi zao.

Related Posts