Moshi. Mwanaharakati na Mkurugenzi wa GH Foundation, Godlisten Malisa ameendelea kuripoti katika ofisi za Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kilimanjaro (RCO) kutokana na tuhuma za uchochezi zinazomkabili.
Malisa amesema amejipanga kukabiliana na tuhuma hizo na anataka kesi yake ipelekwe mahakamani.
Ikiwa ni mara ya pili sasa, leo Juni 27, 2024, Malisa ameripoti kituoni hapo baada ya kupewa dhamana Juni 8, mwaka huu.
Malisa alikamatwa Juni 6, 2024 muda mfupi baada ya kesi inayomkabili yeye na Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob, kuahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoani Kilimanjaro akikabiliwa na tuhuma tatu.
Anakabiliwa na tuhuma tatu za kuchapisha taarifa za uchochezi kuhusu mauaji ya Beatrice Minja, mkazi wa Rombo anayedaiwa kuuawa na mtu aliyefahamika kwa jina la Paul Tarimo, na tukio la mwanafunzi anayedaiwa kuuawa kwa kichapo Moshi.
Tuhuma nyingine ni kutoa taarifa bila kibali kwenye akaunti yake ya Instagram kuhusu walimu waliokuwa wakisahihisha mitihani ya kidato cha nne Januari mwaka huu kuhusu kutolipwa posho zao.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuripoti kituoni hapo leo, Malisa amesema kama polisi waliweza kumkamata na kumfungulia mashitaka, anaamini wamefanya upelelezi wa kutosha, hivyo akataka shauri lake lipelekwe mahakamani.
“Tangu tumefika Polisi tumekuwa tukipewa muda wa kuja kuripoti kwa sababu upelelezi wanasema bado unaendelea. Kwa hiyo leo nimefika polisi kuripoti ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kilimanjaro (RCO) na baada ya mazungumzo wametupa tena muda wa wiki mbili kwamba tuje turipoti tena,” amesema Malisa.
Amesema wanataka sheria ifuatwe kama utaratibu wa kisheria unavyeleza kwamba Polisi anapomkamata mtuhumiwa, ni vizuri wakampeleka mahakamani kwa sababu huwezi kumkamata mtuhumiwa halafu ndio uanze upelelezi.
“Kwa hiyo mashauri yote matatu ambayo nakabiliana nayo bado hayajapelekwa mahakamani na maelezo ni kwamba upelelezi haujakamilika. Tunaamini polisi wana mafunzo na wanatekeleza sheria, kwa sababu wana mafunzo hatuamini kwamba wanaweza kumkamata mtu halafu ndio wakaanza kupeleleza,” amesema Malisa na kuongeza;
“Tunaamini wamefanya upelelezi wa kutosha kwa hiyo watupeleke mahakamani na sisi tupo tayari kukabiliana nao mahakamani. Tulitarajia leo upelelezi umekamilika na tuende mahakamani maana tulikuwa tumeshajipanga na kujiandaa kwa ajili ya kwenda kukabiliana nao mahakamani,” amesema Malisa.
Akizungumza mmoja wa mawakili wake, Dickson Matata ameliomba Jeshi la Polisi kupeleka kesi hiyo mahakamani hatua ambayo amedai itaondoa usumbufu kwa mteja wake kuripoti polisi kila baada ya wiki mbili.
“Tulitegemea wakati wanamkamata wangekuwa wameshakamilisha upelelezi na kumfikisha mahakamani lakini cha kushangaza na leo tena tumepewa ngonjera ile ile upelelezi haujakamilika na tunatakiwa kuripoti Julai 11, 2024,” amesema Matata.
Amesema; “Sisi tupo tayari tutakuja kuripoti lakini leo tumeondoka tukiwa tumewasisitiza na kuwaomba polisi kwa kufuata weledi wa kipolisi wahakikishe ndani ya huu muda ambao wametupa wa wiki mbili, wawe wamekamilisha upelelezi na tutakapokuja tuweze kwenda mahakamani.”
Aidha, amesema Polisi kwa sasa ndio wenye kesi na wao hawana uwezo wa kuwalazimisha kuipeleka mahakamani, lakini watakaporudi Julai 11 wataona cha kufanya ili kuweza kuvuka.
“Tutakapofika siku hiyo kama watakuwa bado wanaendelea na hii ngonjera ya upelelezi haujakamilika tutaona nini cha kufanya kwa sababu huyu ana dhamana na haki ya dhamana ni ili mtu aendelee kufurahia uhuru wake mpaka pale mahakama itakapothibitisha tofauti. Lakini hiki kitendo cha kuja kuripoti kila mara baada ya wiki mbili ni kama vile amekuwa mfungwa na kinaondoa ile maana halisi ya dhamana, hivyo tutajua ni namna gani tutavuka mto itakapofika hiyo Julai,” amesema Matata.