MOJA ya kumbukumbu zitakazokaa muda mrefu kuhusu msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara 2023-2024 ni mchezo wa kwanza wa Azam FC dhidi ya Tabora United.
Katika mchezo huo, Tabora United ikiwa chini ya zuio la Fifa kutumia baadhi ya wachezaji ilijikuta ikianza mchezo na wachezaji wanane tu na hivyo mchezo kutofika mwisho baada ya wachezaji wawili ‘kuumia’, hivyo timu hiyo ikakosa akidi ya wachezaji saba wanaotakiwa ili mchezo uendelee, matokeo yake ikafungwa mabao 4-0.
Jinamizi hili la mikataba ya wachezaji halikuikumba Tabora United peke yake, hata timu nyingine ikiwamo mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga na zilikutana na rungu la Fifa la kuzuiwa kufanya usajili kwa sababu ya madai ya mishahara au stahiki nyingine za wachezaji na watumishi wa ufundi.
Nimetoa mfano wa Tabora kuonyesha jinsi migogoro ya usajili au masilahi ya wachezaji na benchi la ufundi inavyoweza kuathiri matokeo uwanjani.
Kwa historia, soka na michezo kwa jumla hazikuwa shughuli ya kulipwa. Utamaduni huo umejikita katika akili za baadhi ya waendesha shughuli za michezo kiasi cha kuwachukulia poa wachezaji au makocha.
Inasemekana mwaka 1885 Chama cha Soka cha England (FA) kiliviagiza vilabu kuanza kulipa mishahara kwa wachezaji kama njia ya kuhakikisha wanaweka muda wao mwingi katika kazi hiyo.
Hata hivyo, bado wachezaji na walimu wao waliendelea kuwa na kazi zao nyingine. Malipo yaliyotokana na soka yalikuwa ya kuongezea kipato nje ya kazi nyingine walizoajiriwa rasmi.
Kadri muda ulivyokwenda mazingira yalizilazimu timu kuwahitaji wachezaji kwa muda mrefu zaidi kwa ajili ya mazoezi, mashindano na safari na huku upande wa pili kwenye ajira zao za kudumu wachezaji hao wakihitajika. Hakukuwa na jinsi nyingine kwa klabu zilizokuwa na uwezo zikaanza kuajiri wachezaji na wataalam wa kudumu. Hata hivyo, kwa muda mrefu soka lilibaki kuwa ni shughuli ya burudani baada ya kazi.
Hapa kwetu hali haikuwa tofauti. Tangu soka lilipoletwa nchini na mabaharia na wamisionari, umekuwa ni mchezo wa kuwaburudisha wachezaji wenyewe na mashabiki pia.
Timu nyingi za soka zilitoka kwenye taasisi za elimu, majeshi na mashirika ya umma. Mamlaka kama za Bandari, Reli na zile za mazao ya kilimo kama Pamba, Tumbaku na Kahawa ziliongoza kwa kutengeneza timu za soka.
Wachezaji katika timu hizo walipewa mishahara kama wafanyakazi wengine wa taasisi hizo. Wanamichezo wazuri walianza kufuatiliwa kwenye timu zao za mtaani au kwenye michezo shuleni na kupewa ajira kama chambo cha kuwanasa.
Baada ya hapo mchezaji hakuwa na madai mengine nje ya ajira. Hata kwa klabu za mtaani kama Yanga, Simba, Cosmopolitan, Coastal Union na nyinginezo bado zilitumia chambo cha ajira kupata wachezaji wazuri.
Vigogo wapenzi wa klabu hizo walishawishi menejimenti za mashirika yao kuwaajiri wachezaji waliokuwa kwenye timu zao pendwa. Hadi hivi karibuni haikuwa ajabu kukuta mchezaji wa Yanga au Simba ameajiriwa bandarini, reli na mashirika mengine ya umma.
Wachezaji wengine waliajiriwa kwenye kampuni binafsi za ‘matajiri’ au mapatroni wa timu kama walivyoitwa huko nyuma.
Hali ya sasa imebadilika kwa wanamichezo na kwa taasisi zinazowaajiri. Wanamichezo wana mikataba kama ilivyo mikataba mingine ya ajira.
Mwajiri anapaswa kujua wajibu wake kwa mwajiriwa na mwajiriwa anapaswa kujua wajibu wake na haki yake.
Uhusiano huo hauishii kwenye kujua tu bali matendo ya kila siku ya mwajiri na mwajiriwa yanatakiwa kuakisi kile kilicho ndani ya mkataba.
Huko nyuma tulizoea kusikia wachezaji hata makocha wakilalamika waliahidiwa fedha au vitu kadhaa wakati wanaingia makubaliano na timu ila baada ya kuanza kazi hawajapewa fedha na vitu walivyoahidiwa.
Kuna wakati malalamiko hayo yalifuatiwa na migomo hata hujuma dhidi ya mwajiri. Mfano mzuri ni pale Simba ilipomchukua Mbwana Samatta kutoka Mbagala Market na kumwahidi angepewa usafiri yaani gari.
Kijana baada ya kufuatilia gari aliloahidiwa na kupigwa danadana aliamua kutojiunga na timu na shinikizo lake likawafanya Simba watimize ahadi yao. Matukio ya namna hii yalikuwa mengi kwa wachezaji wetu hata wale waliovuka mipaka kucheza nchi jirani na ughaibuni hasa maeneo ya Ghuba.
Ujanja haukuwa upande wa klabu tu; kuna wachezaji ‘waliziingiza klabu mjini’ kwa kusaini kandarasi zaidi ya moja.
Enzi zile mchezaji akisaini kandarasi zaidi ya moja anaambiwa na chama cha soka (FAT) achague timu anayoipenda yeye. Matokeo yake na kwa sababu mchezaji hawezi kuchezea timu mbili, timu moja ilikula hasara.
Baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na lile la Afrika (CAF) kuanzisha mifumo ya weledi katika ajira za wachezaji na mabenchi ya ufundi kesi hizi zimepungua kwa kiasi kikubwa na hata zinapojitokeza, kanuni zipo za kutolea maamuzi.
Klabu za Ligi Kuu Bara zimekuwa na matatizo katika namna zinavyotimiza majukumu yao kwa wachezaji na makocha wa kigeni. Yawezekana hata wachezaji na walimu wazawa wa wanapitia kadhia hiyo, labda wanayamaliza kifamilia kwani hatusikii kesi nyingi za wachezaji au makocha wazawa kuziburuza klabu Fifa au kwenye mahakama ya michezo ya CAS.
Yawezekana hata klabu zinadhulumiwa na wachezaji na wataalamu wa ufundi, lakini kwa sababu halijasikika sana basi tatizo kubwa tunaliona upande wa klabu.
Msimu wa usajili unapofika klabu hupigana vikumbo kupata wachezaji walio bora. Juhudi nyingi huwekwa kwenye kumpata mchezaji kuliko kenye kufikiria kitakachokuwa ndani ya mkataba wa mchezaji.
Wenzetu walioendelea hutumia muda mwingi kujadili kitakachokuwa kwenye mkataba kuliko suala la kumpata mchezaji. Mathalani kuna matajiri hujitolea kuisadia timu kumpata mchezaji fulani kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha ya usajili na klabu ikishampokea mchezaji basi kazi ya tajiri imekamilika.
Suala la mshahara au masilahi mengine hubaki mgongoni mwa klabu. Sasa umekuwa ugonjwa wa klabu za ligi kuu na hata za ligi ya Championship kusajili wachezaji wengi wa kigeni na kuwapa mikataba ambayo utekelezaji wake huja kuigharimu klabu.
Kutokana na ugumu huo au hata kutokana na mchezaji au mwalimu kuwa chini ya kiwango klabu hulazimika kuvunja mikataba huku kukiwa hakuna pesa ya kugharimia hilo.
Matokeo yake mchezaji mmoja ambaye ameachwa anaweza kuigharimu timu pesa nyingi kama fidia ya ukiukwaji wa taratibu za kuachana. Fedha ambazo zingetumika kugharimia mahitaji mengine ya timu.
Tuko kwenye kipindi cha usajili kwa ajili ya Ligi Kuu na zile za maraja ya chini. Ni wakati sasa klabu zikaepuka usajili wa kukurupuka au ule wa kukomoana. Kufanya vizuri kwa timu kunategemea sana umakini katika usajili wa wachezaji na benchi la ufundi.
Usajili mzuri ni pamoja na kuwa weledi katika namna ya kuachana na wachezaji na kuangalia ulali wa fedha zinazoingia na zinazotoka.
Usajili ni kama kuingia kwenye ndoa ukijua familia inavyopanuka na mahitaji yataongezeka na hautaweza kuvunja ndoa kwa sababu ya gharama za maisha au kutopendezwa na mwenza na kama utalazimika kufanya hivyo bado utalipa gharama za talaka.
Mwandishi wa makala haya ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).