Okwi achagiza mpango wa straika mpya Simba

STAA wa zamani wa Simba na Yanga, Emmanuel Okwi amehusika kwa kiasi kikubwa kumshawishi, Straika Mganda Steven Dese Mukwala (24) asaini Msimbazi, Mwanaspoti linajua.

Mukwala huenda akatambulishwa muda wowote kuanzia sasa kwani tayari yupo Jijini ametulia kwenye hoteli moja iliyoko kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi.

Okwi ambaye kwa sasa anaichezea Erbil SC ya Ligi Kuu ya Iraki, inaelezwa kwamba aliombwa Simba amlainishe mchezaji huyo kwani klabu ilikuwa ikimtaka kwa udi na uvumba na vilevile alikuwa na ofa kadhaa nje ya Afrika Mashariki mbali na klabu yake ya Asante Kotoko ya Ghana.

Simba imetumia zaidi ya Sh300 milioni kupata saini ya Mukwala ambaye alikuwa akiwaniwa na klabu mbalimbali ikiwemo FC Petrocub Hincesti ya Moldova.

Mwanaspoti lilikuwa la kwanza kukupa habari ya Simba na Mukwala kuwa kwenye mazungumzo yaliyoanza mwanzoni mwa mwezi huu na sasa amesaini mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mmoja zaidi kulingana na atakavyokiwasha uwanjani.

Mpaka jana tulivyokuwa tunakwenda mitamboni tayari alishatengeneza picha na video za utambulisho wake tangu Jumatano ya wiki hii.

Mukwala ni mshambuliaji wa kati mwenye miaka 24 na urefu wa futi 5.6 aliyezaliwa mjini Makindye nchini Uganda mwaka 1999.

Straika huyo anasifika zaidi kwa kutumia mguu wa kulia na uwezo mkubwa wa kufunga kwa kichwa, huku kasi na mabavu zikiwa sifa zake za ziada.

Msimu uliopita aliibuka mfungaji bora namba mbili wa Ligi Kuu ya Ghana kwa kufunga mabao 14 nyuma ya kinara Stephen Amankonah wa Berekum Chelsea aliyecheka na nyavu mara 16.

Aidha aliibuka mchezaji bora wa ligi ya Ghana kwa mwezi Desemba mwaka jana akiwa na Kotoko aliyojiunga nayo Agosti Agosti 2022 akitokea URA ya Uganda na katika msimu wake wa kwanza alifunga mabao 11 na kutoa asisti tano.

Akiwa URA Mukwala alicheza kwa misimu mitatu kuanzia mwaka 2020 ambapo msimu wa kwanza 2019/20 aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Uganda akifunga mabao 13. Msimu uliofuata wa 2020/21 akafunga mabao 14 na msimu wake wa mwisho kwa watoza ushuru hao yaani 2021/22 akacheka na nyavu mara 13 hivyo ana wastani wa kufunga mabao zaidi ya 10 kwa kila msimu.

Straika huyo alianza soka la ushindani mwaka 2017 alipojiunga na Vipers akitokea Masaza FC kisha Maroons kabla ya kurejea Vipers na baadaye URA, pia amepita kwenye timu zote za taifa za Uganda kwa vijana na sasa ni tegemeo kwa Uganda Cranes.

Mukwala anaungana na Lameck Lawi, Joshua Mutale, Yusuph Kagoma na Omary Omary kuwa wachezaji wapya wa Simba ambao usajili wao umekamilika na kama kila kitu kitaenda sawa wengine watakaosainiwa Simba ni pamoja na kiungo Debora Mavumbo kutokea Mutondo Stars ya Zambia, beki wa kati Idumba Fasika na Winga Elie Mpanzu wote kutoka DR Congo sambamba na kiungo Agustine Okejepha kutoka Rivers United, Nigeria.

Related Posts