RC SAID MTANDA AIPONGEZA MSD KWA MAGEUZI YA KIUTENDAJI

Na Mwandishi Wetu

MKUU wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda ameipongeza Bohari ya Dawa (MSD) kwa ugatuzi wa madaraka kwa Kanda zake nchini, kwani uamuazi huo utasaidia na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa wakati.

Mtanda ametoa pongezi hizo hapo jana, wakati akifunga kikao kazi baina ya MSD na Wateja wake wanaohudumiwa na Kanda ya Mwanza ambao ni kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu na Geita.

Ameeleza licha ya kuokoa muda wa manunuzi, ugatuzi huo madaraka kwa Kanda, utasaidia kupunguza mzigo wa majukumu kwa MSD Makao Makuu, na kuleta ufanisi.

Pia ameipongeza Mènejimenti ya MSD kwa utaratibu wake wa kukutana na wadau na wateja wake, kujadiliana na kutatua changamoto za upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.

Awali akifungua kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai ameeleza maboresho mbalimbali yanayofanyika ndani ya Bohari Ili kuleta tija katika kuwahudumia Wateja wake.

Amebainisha kwamba hivi sasa MSD imewekeza nguvu katika kuboresha maeneo yake ya Uhifadhi kwa kujenga maghala ya kisasa katika Kanda zake mbalimbali Ili kuongeza uwezo wa Kanda hizo kuhudumia wateja wake.

Aidha, amebainisha juu ya mabadiliko na maboresho ya mikataba ya manunuzi hali iliyopelekea kuongezeka kwa bidhaa ghalani na uwezo wa MSD kukidhi mahitaji ya Wateja.

Ameongeza kwamba Katika kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2023/24, mapato ya bidhaa za afya yameongezeka kutoka kiasi cha shilingi bilioni 266 na kufikia takribani shilingi bilioni 530, Sawa na ongezeko la takribani asilimia 100.

Kwa upande mwingine Mavere amegusia maboresho ya eneo la huduma kwa Wateja kwa kuimarisha mawasiliano na mahusiano na wateja, hivyo kuondoa malalamiko na misuguano isiyo ya lazima.

Naye Meneja wa MSD Kanda ya Mwanza Bw. Egidius Rwezaura amewashukuru Wadau hao kwa kuitikia wito wa kuhudhuria kikao hicho, na kuwataka kuendelea kushirikiana Ili kutatua kwa pamoja changamoto za Upatikanaji wa bidhaa za Afya.


 

Related Posts