Dodoma. Wizara ya Fedha imesema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaendelea kufanya utafiti kuhusu uanzishwaji na matumizi ya sarafu za kidijitali za Benki Kuu (Central Bank Digital Currency).Hayo yamesemwa leo Alhamisi Juni 27, 2024 na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile.Dk Ndugulile amehoji Serikali ina mpango gani wa kuanza matumizi ya sarafu za kidijitali nchini.Akijibu swali hilo, Chande amesema Benki Kuu ya Tanzania kwa sasa inaendelea na hatua ya utafiti wa uanzishwaji wa matumizi ya sarafu za kidijitali za Benki Kuu.Amesema Benki Kuu imebaini kama ilivyo kwa mataifa mengi, uanzishwaji wa sarafu hizo, unahitaji kuanzishwa kwa uangalifu na umakini bila kuleta athari hasi katika mifumo ya malipo iliyopo nchini.Pia amesema utaratibu huo huweze kutatua tatizo halisi la malipo, lakini kwa sasa mifumo iliyopo nchini bado inakidhi hali halisi ya uwezeshaji mwananchi kutuma fedha na kufanya malipo.Amesema soko la Tanzania bado linahitaji kuendelea kuboreshwa kwa kutumia vyanzo vinavyopatikana kwa urahisi na wananchi wengi (simu za kawaida), tofauti na sarafu za kidijitali zinazoitaji matumizi ya simu janja pekee.“Nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na majirani zetu na ukanda wetu, bado zipo katika hatua hizi za awali za utafiti na kuboresha mifumo ya malipo iliyopo,” amesema.Katika swali la nyongeza, Dk Ndugulile amesema sasa hivi nchini kuna biashara ya foreigh currency market (fedha za kigeni mtandaoni) inayofanyika mtandaoni na kuhoji nini mkakati wa Serikali wa kusimamia na kuratibu biashara hiyo.“Kuna Watanzania wengi wanafanya nje ya nchi na wengine walioko nchini wanafanya kazi nyingine za kisanii, biashara na ushauri, wanalipwa kupitia mitandao ambao hulipwa kwa fedha za kigeni na fedha zile kuingia nchini imekuwa changamoto kubwa kwa sababu ya gharama za makato wanazo pitia,” amesema.Amehoji kama kuna mpango wa kupunguza gharama ili Watanzania waweze kunufaika na jasho lao.Akijibu maswali hayo, Chande amesema moja ya mikakati ya Serikali ni kuimarisha mifumo ya utumaji na upokeaji wa fedha ili kupunguza gharama, ikiwa ni pamoja na kupunguza tozo na makato mbalimbali.“Serikali inaendelea kufuatilia suala hili na tumechukua ushauri wake (mbunge), tukiona ipo haja ya kufanya hivyo basi tutafanya,” amesema.Naye Mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichalwe amehoji “Serikali inaonaje ikimpa CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) kufanya ukaguzi kwenye miamala yote inayofanyika kwenye sarafu mtandao ili kujua ni kiasi gani inapoteza ili kulitumia eneo hilo kama chanzo cha mapato.”Akijenga msingi wa swali lake, amesema ili nchi iweze kujiendesha vizuri ni pamoja na kupata mapato na kwamba kwenye eneo la sarafu za kidijitali imeonekana kuna fursa nyingi na vijana wengi wa Kitanzania wanafanya biashara hiyo.Akijibu swali hilo, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaendelea utafiti wa sarafu zote za kidijitali, pamoja na matumizi ambayo yanaendelea na sarafu za kawaida, kama kuna faida na wanaweza kuhamia katika matumizi ya sarafu hizo.“Utafiti unaendelea na sasa tunaangalia uzoefu wa matumizi ya sarafu katika nchi mbalimbali zikiwemo nchi za Afrika, ambazo zimeshaenda katika digital currency (sarafu za kidijitali), kama Nigeria pamoja na nchi za Asia, ambazo zimeanza kutumia utaratibu huo. Baada ya kukamilika tutaanza hatua kwa hatua kama tutaona ni jambo lenye faida,” amesema.Juni 13, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan aliitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kujiandaa na matumizi ya sarafu za mtandao (Crypto-Currency) ili mabadiliko hayo yakija yakute nchi ipo tayari
Aliongeza kuwa nchi inaweza kuona haiko tayari lakini wananchi wakaitaka na wakawa wanaenda nje za nchi kupata huduma hiyo.