Dkt. Harrison Mwakyembe, Mwenyekiti wa Baraza la
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili akizungumza katika kongamano hilo
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili ( Muhas) Profesa Appolinary Kamuhabwa kizungumza mara baada kufunguliwa kwa kongamano la 12 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) linaloendela katika ukumbi wa kituo Mahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cja Afrika Mashariki Kampasi ya Mloganzila.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo akizungumza na wadau mbalimbali wa Afya na watafiti leo Juni 27, 2024 wakati wa akifungua kongamano la 12 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) linaloendela katika ukumbi wa kituo Mahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cja Afrika Mashariki Kampasi ya Mloganzila.
Na Karama Kenyunko Michuzi tv
SERIKALI yakitaka chuo cha muhas kutoa mapendekezo namna ya kushughulikia magonjwa yasiyoambukiza.
SERIKALI imekitaka Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kutoa mapendekezo mapya namna ya kushughulikia magonjwa yasioambukiza yakiwemo afya ya akili, magonjwa ya uzeeni, ajali, kisukari, magonjwa ya moyo saratani na mengineyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo ametoa mapendekezo hayo leo Juni 27,2024 wakati wa akifungua kongamano la 12 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) linaloendela katika ukumbi wa kituo Mahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cja Afrika Mashariki Kampasi ya Mloganzila.
Aidha amekitaka chuo hicho pia kujenga na kuimarisha maadili kwa watoa huduma za afya wanaozalishwa nchini na matumizi ya teknolojia upande wa akili bandia.
Kupitia kongamano hilo, Prof Nombo amewataka watafiti wa MUHAS kujadili changamoto mbalimbali za afya ikiwemo ya mama na mtoto, huduma za dawa za dharura, mabadiliko ya hali ya hewa na changamoto zingine.
Amesema, baadhi ya changamoto hizo zimekuwepo kwa muda mrefu na nyingine zimejitokeza hivi karibunii hivyo anaamini kuwa kongamano hilp litatoa majibu kwa changamoto hizi zinazotukabili hapa nchini.
Prof. Nombo amesema kuwa MUHAS kwa kushirikiana na Serikali wapo katika mkakati wa kuanzisha vituo vingine vya umahiri katika Kampasi ya Mloganzila ikiwepo Awamu ya Pili ya Ujenzi wa Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu na Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Afya ya Kinywa.
“Miundombinu hii pamoja na mingine itakayojengwa baadaye itawezesha kampasi ya MUHAS kuwa kitovu cha mafunzo ya ubobezi ya afya na sayansi shirikishi, tafiti, bunifu na huduma za kibingwa na kibobezi hapa nchini na ukanda wa Afrika Mashariki,” ameongeza Prof Nombo.
Sambamba na hilo ameipongeza Serikali ya Uswidi kupitia shirika la Sida kwa mchango mkubwa na endelevu katika utafiti kwa miaka mingi na kwa kuwa mfadhili mkuu wa makongamano hayo kwa miaka kumi na mbili mfululizo.
“Ninatoa shukrani za dhati pia kwa Serikali ya Korea Kusini kwa kutoa mkopo wa riba nafuu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mkopo uliowezesha kujenga hospitali ya kisasa ya mafunzo na kuweka vifaa vya kutosha na vya kisasa katika kampasi hii ya Mloganzila,” ameongeza Prof Nombo.
Prof Nombo amesema kuwa miongoni mwa majengo zaidi ya 130 ya elimu ya juu inayojenga na kukarabati nchini ni pamoja na ujenzi wa kampasi kubwa ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) mkoani Kigoma na Mloganzila.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Muhas Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa Kongamano hilo ni chachu ya suluhisho la magonjwa mbalimbali yakiwemo yale yasiyoambukiza ambayo yamekuwa tatizo kubwa nchini.
“Kupitia Kongamano hili tutapata fursa ya kujadili tafiti mbalimbali zitakazoleta ufanisi kwenye mapambano dhidi ya magonjwa hayo , tupendekeze namna bora ya kukabiliana” amesema Dkt. Mwakyembe.
Amesema kuwa magonjwa ya yasiyoambukiza yamekuwa tishio hivyo wataalam watumie vizuri kongamano hilo kuisaidia jamii.
Kwa upande wake Profesa Appolinary Kamuhabwa Makamu Mkuu wa Chuo hicho amesema kuwa wataalam wa masuala ya afya watajadili tafiti mbalimbali zitakazowasilishwa ili kupatikane majibu ya namna bora ya kukabiliana nayo.
Amesema kuwa wataalam watajidili magonjwa yasiyoambukiza, afya ya akili, lishe na upasuaji, magonjwa ya kuambukiza na usugu wa dawa dhidi ya vimelea , afya ya mama, mtoto na vijana rika, utunzaji wa afya ya kinywa, sikio, koo na pua, viamuzi vya afya kwa jamii, utafiti w mifumo ya afya na tiba mbadala , uvumbuzi wa dawa chanjo na matumizi ya akili bandia.