Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amekerwa na udhalilishaji unaofanywa na baadhi ya watu wanaotoa mikopo kwa njia ya mtandao kwa kuwashirikisha wasiohusika na mikopo hiyo.
Dk Tulia ameyasema hayo leo Alhamisi Juni 27, 2024 wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma.
“Mheshimiwa waziri kuna hili jambo ambalo linajadiliwa sana huko nje ya hii mikopo inayotolewa kwa njia ya mtandao na watu kudhalilishwa, sijui kama kuna mwongozo wowote na Serikali mnalipokea na mnalifanyia kazi, hilo limekuaje,” amesema.
Dk Tulia amesema hata yeye amepata ujumbe wa mtu ambaye anamwambia kuwa mtu huyo anadaiwa na kuhoji yeye anahusika nini kwenye yeye kudaiwa.
“Sasa hilo naona limelalamikiwa sana na wananchi sasa sijui kama kuna maelezo yoyote upande wenu Serikali kwa sababu tunazungumzia mambo yote ya mtandao,” amesema Dk Tulia.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo kwa muda ya watu ambao wanakopesheana mitandaoni lakini baadaye wanatuma taarifa za watu wanaozunguka yule waliomkopesha mtandaoni.
“Kwa maana ya namba za simu na kuanza kumsumbua pale ambapo wameshindwa kurudishiwa mkopo wao, hili jambo limetokea kwa wiki kadhaa kama sio miezi miwili mitatu na baada ya kuliona tumeagiza wenzetu wa TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania), lakini wakishirikiana na Cyber Crime Unit (kitengo cha kudhibiti wizi mtandaoni) ya Jeshi la Polisi wanalifanyia kazi,” amesema.
Amesema ni matumaini yake kuwa shughuli hiyo itakamilika mapema ili waone msingi wa jambo hilo kwa ukubwa wake na wapi wanapozipata hizo namba.
“Msingi mkubwa hapa ni ule udhalilishaji unaofanyika baada ya kushindwa kulipana baada ya kukopeshana maana ni jambo ambalo linatokea mtu anachukua namba za watu wengi sana wenye uhusiano na yule mtu waliyemkopesha,” amesema.
Amesema wanalitafuta hilo jambo linatokea wapi ili wachukue hatua na kulikomesha.
“Lakini hili jambo sio la kiungwana na ni kinyume cha sheria na hasa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kutumia taarifa za watu wengine kufanya chochote na hizo taarifa, hili jambo ni kinyume na sheria, ni nje ya utaratibu sio la kiungwana na linapaswak ukomeshwa,” amesema Nape.
Aprili 1, 2024, Mwananchi Digital liliripoti malalamiko ya baadhi ya watu wanaotumiwa ujumbe kuwataka kuwakumbusha waliokopa kulipa madeni yao na jinsi kampuni za zinavyopata namba hizo za simu.
Ujumbe huo umekuwa ukisomeka: “Ndugu wa karibu/jamaa /rafiki/jirani wa (jina la mkopaji na namba za simu)… aliyechukua mkopo kwa njia ya mtandao kupitia Application ya … unafahamishwa kuwa mtu huyu amekiuka makubalianao kwa kutolipa deni siku husika ya marejesho na kutopokea simu za ofisi, hivyo tutamchukulia hatua kwa kosa hilo.
“Unaombwa kumpigia simu muhusika na kumjulisha kuwa ana masaa mawili ya kulipa deni kabla hatua kali hazijachuliwa dhidi yake. Fanya hivyo kuepuka usumbufu.”
Ujumbe huu ni kinyume na kanuni za ukusanyaji madeni kwa mujibu wa Toleo la Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha 2019 ibara ya 56, kifungu cha 1, (c,d) kinachokataza “kumtisha au kutumia nguvu au njia zisizo halali katika kukusanya au kufuatilia deni; pia kutotumia lugha ya fedheha au isiyofaa.”
Vilevile, kuna tatizo jingine la kudukua taarifa za mteja na kutafuta namba za simu alizozihifadhi kwenye simu yake na kuzitumia ujumbe wa vitisho.
Mmoja wa viongozi wa kampuni moja inayotoa mikopo kwa njia ya mtandao ambaye hakutaka jina lake litajwe, anasema kudukua taarifa za mteja wao ikiwamo kuchukua namba za watu wake wa karibu, ni hatua ya mwisho baada ya kufanya jitihada za kumtafuta kwa mfumo wa kawaida kushindikana.
“Ikitokea mteja amekuwa sugu tunaangalia faili lake kuna namba mbili anaziandika za wadhamini tukiwatafuta hawapatikani au ni wasumbufu, tuna tumia mfumo wetu uliounganishwa na namba za mhusika na unawezesha kuona hadi namba za watu wake wa karibu anaowasililiana nao mara kwa mara, kisha tunawatumia ujumbe,” amesema.
Pia, amesema kwa sheria ya kampuni yao kufanya marejesho mwisho ni saa 05:00 asubuhi lakini muda huo hawajauweka wazi kwenye mitandao yao, lakini wanaochukua mikopo wanaelezwa sharti hilo kabla ya kupewa fedha.
“Tumeshindwa kuweka wazi kwenye mitandao kwa sababu mifumo yetu ina changamoto na bado tunajaribu kuangalia teknolojia ya kutuwezesha kila mmoja aone ili ukikopa fedha zirudi kwa wakati tuwakopeshe wengine.”
Amesema wamekuwa wakiwasisitiza wateja wao kufanya marejesho mapema na kuwa wanapochukua wanakubali lakini wakati wa kurejesha wamekuwa wakitoa visingizio vingi ikiwamo kudai wamefiwa au wanauguza.
“Muda ukifika kampuni huwa inahitaji fedha zake bila kujali mteja anapitia katika hali gani au kapatwa na msiba, tunachohitaji malipo yetu tupewe kwa wakati,”amesema kiongozi huyo.