‘Thank You’ Fountain zinasubiri kocha mpya

WAKATI timu nyingine za Ligi Kuu Bara zikianza heka heka za usajili na kuboresha vikosi vyao kuelekea msimu ujoa, uongozi wa Fountain Gate FC ya Mwanza inasubiri kutambulishwa kwa kocha mpya ambaye ndiye atatoa maoni ya mwisho kwa wachezaji watakaochwa na usajili mpya.

Timu hiyo ambayo awali ilijulikana kwa jila la Singida Fountain Gate Juni 15, mwaka huu ilifiki uamuzi wa kuvunja benchi lote la ufundi lililokuwa chini ya kocha wa muda, Ngawina Ngawina na msaidizi wake, Ally Mustafa ‘Barthez’.

Akizungumzia maboresho ya benchi la ufundi na kikosi, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Issa Mbuzi, alisema menejimenti ya klabu chini ya Mtendaji Mkuu, Thabita Kidawawa na Kamati ya Utendaji wanaendelea kukamilisha taratibu za kumtangaza kocha mpya.

Alidokeza kwamba tayari kocha mpya amekwishapatikana na mzawa (Mtanzania) ambaye atatangazwa wakati wowote taratibu zikikamilika, huku akisubiriwa kuja kutoa maoni ya mwisho kuhusu aina ya wachezaji watakaosajiliwa na kuachwa.

Baadhi ya wachezaji wa Fountain Gate wanaotajwa kuondoka ni Francy Kazadi, nahodha Beno Kakolanya ambaye alitibuana na viongozi kutokana na utovu wa nidhamu, Yusuph Kagoma na Habib Kyombo.

“Maboresho yatafanyika kwa sababu lazima wachezaji wengine waondoke na wengine wataingia lakini kwa sasa bado sijakabidhiwa majina ya wachezaji ambao klabu imefikia uamuzi wa kuachana nao. Menejimenti na kamati ya utendaji wanaendelea kuhakikisha mambo yanakamilika,” alisema Mbuzi na kuongeza;

“Suala la kocha mkuu limeshakamilika taratibu zikikamilika tutatangaza, kocha mkuu ni mzawa tunatamani kuwapa nafasi makocha wazawa ili waonyeshe uwezo wao. Suala la kuwaaga wachezaji tunasubiri kocha mpya aje atoe maoni yake kabla ya kuanza usajili mpya.”

Related Posts