Vyakula vyenye virutubisho lishe ndio kila kitu kuukabili udumavu

Iringa. Jamii imeshauriwa kuondoa mitazamo tofauti kuhusu vyakula na mafuta vinavyoongezwa virutubisho ili kuondokana na changamoto za lishe katika mikoa mbalimbali, hasa ya Nyanda za Juu Kusini zenye idadi kubwa ya watoto wenye utapiamlo na udumavu.

Ushauri huo umetolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Hellen Chisanga wakati akizungumza na wanahabari mjini Iringa akisema kwa sasa mkoa huo umeanza kufanya kampeni ya kuangalia hali ya lishe kwa watoto walio chini ya miaka mitano, ukilenga kuwafikia watoto zaidi 5,000 kujua hali ya udumavu.

Miongoni mwa hatua wanazochukua ni kukaa meza moja na wasindikaji wa vyakula na mafuta vilivyoongezwa virutubisho ili kujua changamoto wanazokabiliana nazo na kuzifanyia kazi.

Amesisitiza kwamba imewalazimu kufanya kampeni na kushirikiana na shirika la kimataifa linalojihusisha na uboreshaji wa lishe (GAIN) ili kusaidia katika kampeni hiyo.

Ofisa Lishe Mkoa wa Iringa, Anna Patrick amesema mitazamo inatofautiana kwenye jamii kuhusu vyakula vilivyoongezwa virutubisho, wapo wanaoelewa na kuvitumia lakini wapo ambao hawana uelewa wa kutosha, ambao wanapingana navyo wakidai watashindwa kuzaa au kupunguza nguvu za kiume.

“Wale ambao hawana elimu wanapingana navyo wakidai watashindwa kuzaa au kupunguza watu, lakini tukiwaelimisha wanaelewa.

“Tunashukuru kwa hatua tuliyofikia kwa juhudi za GAIN na Serikali, hasa kuwawezesha wasindikaji ambao walipokea vizuri na sasa tuna uhakika wananchi wanapata vyakula vilivyorutubishwa na hii ni hatua kubwa kama mkoa,” amesema Anna.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasindikaji Mkoa wa Iringa, Benedict Mnyema amesema walipewa elimu ya kuzalisha unga na nafaka ili bidhaa zao zikidhi ubora, kwa kuongeza virutubisho ili kuondoa changamoto za lishe.

Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto wanazokutana nazo, ikiwemo hofu kwa baadhi ya wateja kuhusu virutubisho hivyo.

Amesema Serikali bado haijawa na sheria rasmi ya kuwa na unga ambao haujaongezwa virutubisho, hivyo ameomba Serikali itunge sheria hiyo ili kuhakikisha jamii ya Iringa na maeneo mengine inatumia unga na mafuta yenye virutubisho ili kukabiliana na udumavu.

Dickson Minja, ofisa miradi na urutubishaji chakula wa GAIN, amesema lengo la mradi huo ni kuimarisha afua za lishe kwa kuongeza virutubisho muhimu kwenye unga wa mahindi.

Kupitia mradi huo, amesema imetengeneza vyama vitano vya ushirika vya wasindikaji kwa mikoa ya Kagera, Mara, Kilimanjaro, Manyara na Iringa.

Related Posts