WANANCHI NYASA WAISHUKURU TANROADS KUANZA MATENGENEZO YA BARABARA YA UNYONI-LIPARAMBA-MKENDA

 Na Mwandishi wetu,Nyasa


BAADHI ya wananchi wa vijiji vinavyopitiwa na barabara ya Unyoni
–Liparamba  hadi Mkenda mpakani mwa Tanzania na Msumbuji wilaya ya Nyasa
,wameishukuru Serikali kupitia wakala wa barabara Tanzania(TANROADS)kwa
kuanza ujenzi  wa barabara hiyo ambayo miundombinu yake imeharibiwa
vibaya na mvua za masika.


Leonald Kawonga mkazi wa Liparamba amesema,wakati wa masika barabara
hiyo  ilikuwa changamoto kubwa kutokana na utelezi na magari
kukwama,hivyo matengenezo hayo yatawezesha  kupitika kirahisi na
kutumika kwa ajili ya usafiri na usafirishaji wa mazao kutoka mashambani
kwenda sokoni.


Lenatha Haule,ameishukuru TANROADS kwa uamuzi wa kufanya matengenezo
barabara hiyo,kwani katika kipindi chote cha masika baadhi ya shughuli
nyingi  za kujiingizia kipato zilisimama kutokana na kukosekana kwa
mawasiliano ya uhakika.


Alisema,barabara hiyo ilikuwa haipitiki kirahisi baada ya kuharibika
vibaya na mvua zilizonyesha kwa wingi hasa katika wilaya ya Nyasa,hivyo
kusababisha baadhi ya maeneo ya barabara kukatika na wananchi hao
kutokuwa na uhakika wa mawasiliano pindi wanapotaka kusafiri kutoka
sehemu moja kwenda nyingine.


Mkazi wa kijiji cha Kingerikiti Zawadi Nyondo amesema, barabara hiyo ina
umuhimu mkubwa kwa sababu ndiyo inayotengeneza mapato makubwa katika
wilaya ya Nyasa kutokana na ukanda huo kuwa yenye uzalishaji mkubwa wa
mazao hasa  Kahawa,mahindi na maharage.


“barabara hii ni tegemeo kubwa kiuchumi kwetu sisi wananchi wa wilaya ya
Nyasa na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla,lakini miundombinu yake bado ni
dhaifu,tunaiomba serikali ione namna ya kuijenga kwa kiwango cha lami
badala ya kuendelea kufanya matengenezo mwaka hadi mwaka kwa kiwango cha
changarawe”alisema.


Kwa mujibu wa Nyondo,barabara hiyo ilipochukuliwa na TANROADS zaidi ya
miaka kumi iliyopita walikuwa na matumaini makubwa kwamba itejengwa kwa
kiwango cha lami ili kuwaondolea adha hasa wakati wa masika,lakini hadi
sasa  bado ya changarawe na wanaendelea kuteseka kutokana na ubovu wake.


Mkazi wa kijiji cha Lumeme Timoth Mapunda,ameiomba serikali kupitia
TANROADS kutengeneza upya baadhi ya madaraja yaliyopo kwenye barabara
hiyo ili kuruhusu maji kupita chini ya madaraja,badala ya juu ili
kuepuka madhara yanayoweza kutokea kwa watu kusombwa na maji.

Muonekano wa  barabara ya Unyoni-Liparamba-Mkenda inayofanyiwa matengenezo baada ya kuharibika na mvua za masika.

 Kazi ya matengenezo ya barabara hiyo ikiendelea.

Wahandisi kutoka wakala wa barabara Tanzania (TANROADS)) Mkoa  wa Ruvuma
Peter Ndalemya kushoto  na Juma  Mkela wakikagua ujenzi wa Reli katika
barabara ya Unyoni-Liparamba-Mkenda ambayo baadhi ya maeneo  ya barabara
hiyo imeharibika kutokana na mvua za masika.

Related Posts