Ajibu aikacha Coastal akimbilia jeshini

KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Simba, Yanga, Azam na Singida FG aliyekuwa akikipiga Coastal Union, Ibrahim Ajibu amesaini mkataba wa miaka miwili na maafande wa JKT Tanzania.

Ajibu aliyeichezea Coastal kwa mafanikio akiwa nahodha akisaidiana na wenzake waliifanya timu hiyo imalize ya nne katika Ligi Kuu Bara hivi karibuni na kukata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika, alishamaliza mkataba na Wagosi na anatua jeshini kama mchezaji huru.

Rafiki wa karibu wa nyota huyo amelithibitishia Mwanaspoti kuwa Ajibu ni mali ya JKT Tanzania kwa mkataba wa miaka miwili na muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa na timu hiyo.

“Ni kweli amesajiliwa na JKT Tanzania baada ya makubaliano na Coastal Union kushindwa kwenda kama walivyokubaliana, hivyo ameamua kubadili upepo kwa kumalizana na timu hiyo ya jeshi,” alisema rafiki huyo wa karibuni wa Ajibu na kuongeza:

“Ajibu alikuwa katika mazungumzo na Coastal kwa ajili ya kusaini mkataba mpya, lakini wameshindwana kwenye suala la maslahi lakini pia kocha aliyempeleka hapo baada ya kutimka hakuwa na furaha ndani ya timu hiyo.”

Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta Ajibu mwenyewe ili azungumzie suala hilo, lakini alisema yeye ni mchezaji mzuri na anaweza kucheza timu yoyote hapa nchini hivyo ni suala la muda tu kutambulishwa kwenye timu ambayo ataitumikia msimu ujao wa mashindano ya soka.

“Ni kweli nimemaliza mkataba na Coastal, lakini kuhusu ni timu gani nitacheza msimu ujao siwezi kuweka wazi kwa sasa, lakini mashabiki watarajie kuniona sana nikicheza kwani bado nina uwezo wa kufanya hivyo kwenye timu yoyote inayocheza Ligi Kuu Bara,” alisema Ajibu aliyewahi kuwa nahodha wa Yanga enzi za kocha Mwinyi Zahera.

Related Posts